01-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Zuhd Yake: Kauli Zake Kuhusu Zuhd (Kuipa Mgongo Dunia)

Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

01-Zuhd Yake: Kauli Zake Kuhusu Zuhd (Kuipa Mgongo Dunia)

 

Alhidaaya.com

 

 

Juu ya kuwa yeye Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa ndiye mtu mtukufu kabisa mbele ya Swahaba zake, na ndio kiongozi wao, lakini hali na maisha yake yalikuwa ni ya Zuhd ya ajabu; kwani ukitambua jinsi alivyoishi katika nyumba duni kabisa na kutokuwa na vifaa na fanicha za kifakhari nyumbani mwake, au  kutokuwa na nguo za kifakhari, au kutokuwa na mali yoyote ile hadi kufariki kwake. Bali la ajabu zaidi ni kufikia hadi miezi ya kutokuwa na chakula nyumbani mwake.  

 

Na hayo ni mafunzo na kigezo kizuri kwetu katika zama hizi kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alitambua lengo la kuumbwa kwake, kwahiyo akaelewa kuwa nyenzo hizo ni za kumpelekea yeye kumwabudu Rabb wake na kutafuta Aakhirah yake, na wala havikuwa ni vitu vya kuvipapia na kuvikusanya katika maisha ya dunia. Na ndio maana katika kauli zake kuhusu Zuhd, amedhihirisha na kufundisha kuwa maisha haya ya duniani ni ya muda mfupi tu wa kupita, hivyo hajataka kumiliki mafao au vitu vya kumstarehesha wala hakutaka anasa za maisha mafupi ya dunia bali alipendelea maisha ya Aakhirah ambayo ndio ya maisha ya kudumu milele. Akaamini na kufuata kauli kadhaa za Rabb Allaah (سبحانه وتعالى) wake Anazosema:

 

وَمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ ۚ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٦٤﴾

Na huu uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni pumbao na mchezo; na hakika Nyumba ya Aakhirah bila shaka hiyo ndiyo yenye uhai wa kweli hasa (wa milele), lau wangelikuwa wanajua! [Al-‘Ankabuwt: 64]

 

 

Na pia Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

اعْلَمُوا أَنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَزِينَةٌ وَتَفَاخُرٌ بَيْنَكُمْ وَتَكَاثُرٌ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ ۖ كَمَثَلِ غَيْثٍ أَعْجَبَ الْكُفَّارَ نَبَاتُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَكُونُ حُطَامًا ۖ وَفِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَغْفِرَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانٌ ۚ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿٢٠﴾

Jueni kwamba uhai wa dunia ni mchezo na pumbao na mapambo, na kufakharishana baina yenu na kushindana kukithiri katika mali na watoto; ni kama mfano wa mvua inayowafurahisha wakulima mimea yake, kisha yananyweya, basi utayaona yamepiga manjano, kisha yanakuwa mabua yaliyonyauka na kupondekapondeka.  Na Aakhirah kuna adhabu kali, na maghfirah kutoka kwa Allaah na radhi. Na uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni sterehe fupi za kughuri. [Al-Hadiyd: 20]

 

 

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ﴿٢٠﴾

Yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya Aakhirah Tunamzidishia katika mavuno yake; na yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya dunia, Tutampa humo, lakini Aakhirah hatokuwa na fungu lolote. [Ash-Shuwraa (42: 20)]

 

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 بَلْ تُؤْثِرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿١٦﴾

Bali mnakhiari uhai wa dunia.

 

وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٧﴾

Na hali Aakhirah ni bora zaidi ya kudumu. [Al-A’laa (87: 16-17).

 

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَزِينَتُهَا ۚ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٦٠﴾

Na chochote mlichopewa katika vitu, basi ni starehe za uhai wa dunia na mapambo yake. Na yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi na yakubakia. Je, basi hamtii akilini? [Al-Qaswasw (28: 60)]

 

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ﴿٢٠﴾

Yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya Aakhirah Tunamzidishia katika mavuno yake; na yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya dunia, Tutampa humo, lakini Aakhirah hatokuwa na fungu lolote. [Ash-Shuwraa (42: 20)]

 

 

Naye (صلى الله عليه وآله وسلم) kuli zake:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ابن مسعود (رضي الله عنه)  قَال:  نَامَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَى حَصِيرٍ فَقَامَ وَقَدْ أَثَّرَ فِي جَنْبِهِ، فَقُلْنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ! لَوْ اتَّخَذْنَا لَكَ وِطَاءً.  فَقَالَ:  ((مَا لِي وَمَا لِلدُّنْيَا؟ مَا أَنَا فِي الدُّنْيَا إِلاَّ كَرَاكِبٍ اسْتَظَلَّ تَحْتَ شَجَرَةٍ ثُمَّ رَاحَ وَتَرَكَهَا))  الترمذي وقال: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alilala kwenye jamvi la mtende likamfanyia alama ubavuni mwake tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Tukufanyie godoro laini?  Akasema: ((Mimi na dunia wapi? Mfano wangu na dunia ni kama mpandaji (anayesafiri kwa mnyama) aliyepumzika kivulini chini ya mti, [muda mfupi tu] kisha akaondoka na kukiacha)). [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Na pia,

 

 

عن المُسْتَوْرِد بن شَدَّاد رضي الله عنه، قَالَ: قَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم: (( مَا الدُّنْيَا في الآخِرَةِ إِلاَّ مِثْلُ مَا يَجْعَلُ أَحَدُكُمْ أُصْبُعَهُ في اليَمِّ، فَلْيَنْظُرْ بِمَ يَرْجِعُ ! )) رواه مسلم.

Imepokewa kutoka kwa Al-Mustawrid bin Shaddaad (رضي الله عنه)    kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)   amesema: "Dunia si chochote katika Aakhirah isipokuwa ni kama mfano wa mtu anayetia kidole chake (Yahyaa aliashiria kidole cha Shahaada) katika bahari, basi naangalie kiasi gani cha maji kimechota."  [Muslim na wengineo. Hadiyth imesimuliwa kwa Isnaad mbalimbali na zote zimesimuliwa na Al-Mustawrid bin Shaddaad ndugu wa Baniy Fihr]

 

 

Na pia,

 

 

عن أنس رضي الله عنه : أن النبي صلى الله عليه وسلم، قَالَ: (( اللَّهُمَّ لاَ عَيْشَ إِلاَّ عَيْشَ الآخِرَةِ )) متفقٌ عَلَيْهِ .

Na imepokewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه)  kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Ee Allaah! Hakuna maisha isipokuwa maisha ya Aakhirah  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na pia,

 

عن جابر رضي الله عنه : أنَّ رسول الله صلى الله عليه وسلم مَرَّ بالسُّوقِ وَالنَّاسُ كَنَفَتَيْهِ ، فَمَرَّ بِجَدْيٍ أَسَكَّ مَيِّتٍ ، فَتَنَاوَلَهُ فَأَخَذَ بِأُذُنِهِ ، ثُمَّ قَالَ : (( أَيُّكُم يُحِبُّ أنْ يَكُونَ هَذَا لَهُ بِدرْهَم ؟ )) فقالوا : مَا نُحِبُّ أنَّهُ لَنَا بِشَيْءٍ وَمَا نَصْنَعُ بِهِ ؟ ثُمَّ قَالَ : (( أَتُحِبُّونَ أَنَّهُ لَكُمْ ؟ )) قَالُوا : وَاللهِ لَوْ كَانَ حَيّاً كَانَ عَيْباً ، إنَّهُ أسَكُّ فَكَيْفَ وَهُوَ ميِّتٌ ! فقال : (( فوَاللهِ للدُّنْيَا أهْوَنُ عَلَى اللهِ مِنْ هَذَا عَلَيْكُمْ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Jaabir (رضي الله عنه)  kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipita sokoni pamoja na Swahaba zake alimuona mbuzi mdogo amekufa na masikio yake yamekatwa. Alikishika katika masikio na kuuliza: "Nani anayemtaka (huyu mbuzi aliyekufa) kwa dirhamu moja?" Wakasema: "Hatutaki huyo awe ni wetu kwa chochote (hata bure). Na je, tutamfanya nini? " Kisha akasema: "Je, mngependa awe wenu bure?" Wakasema: "Wa-Allaahi! Hata kama angekuwa hai angekuwa na kasoro, vipi akiwa maiti?" Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم) "Wa-Allaahu! dunia ni duni zaidi mbele ya Allaah kuliko huyu juu yenu." [Muslim]

 

Na pia,

 

عن أَبي العباس سهل بن سعد الساعدي رضي الله عنه ، قَالَ : جَاءَ رَجُلٌ إِلَى النبي صلى الله عليه وسلم ، فقال : يَا رسولَ الله ، دُلَّنِي عَلَى عَمَلٍ إِذَا عَمِلْتُهُ أحَبَّنِي اللهُ وَأحَبَّنِي  النَّاسُ ، فقال : (( ازْهَدْ في الدُّنْيَا يُحِبّك اللهُ ، وَازْهَدْ فِيمَا عِنْدَ النَّاسِ يُحِبّك   النَّاسُ )) حديث حسن رواه ابن ماجه وغيره بأسانيد حسنة .

Imepokewa kutoka kwa Abu Al-'Abbaas Sahl bin Sa'd As-Saa'idiy (رضي الله عنه)  kuwa: Alikuja mtu kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: "Ee Rasuli wa Allaah, nijulishe mimi amali ambayo nikiifanya Allaah atanipenda na watu watanipenda." Akasema: "Kuwa na Zuhd (Upe nyongo ulimwengu) atakupenda Allaah, na vipe nyongo viliomo mikononi mwa watu watakupenda watu." [Hadiyth Hasan - Ibn Maajah na wengineo kwa Isnaad nzuri]

 

Na pia,

 

عن سهلِ بن سعد الساعدي رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم: (( لَوْ كَانَت الدُّنْيَا تَعْدِلُ عِنْدَ الله جَنَاحَ بَعُوضَةٍ ، مَا سَقَى كَافِراً مِنْهَا شَرْبَةَ مَاءٍ )) رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن صحيح )) .

Imepokewa kutoka kwa Sahl bin Sa'ad As-Saa'idiy (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Lau kama uliwengu ungekuwa na thamani sawa na bawa la mbu mbele ya Allaah, hangempatia kafiri maji ya kunywa hata kiasi cha mkono mmoja." [At-Tirmidhy, na akasema ni Hadiyth Hasan Sahiyh]

 

Na pia,

 

 عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم: (( لاَ تَتَّخِذُوا الضَّيْعَةَ فَتَرْغَبُوا في الدُّنْيَا )) رواه الترمذي ، وقال : (( حديثٌ حسنٌ )) .

Imepokewa kutoka kwa Ibn Mas-'uwd (رضي الله عنه) kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)   amesema: "Msiwe ni wenye kupapia raslimali (zisizohamishika) na hivyo kupendelea dunia." [At-Tirmidhy, na akasema ni Hasan]

 

 

Akawakhofia sana Swahaaba zake wasije kughilibiwa na anasa za dunia wakaacha Zuhd:

 

عن أَبي سعيد الخدري رضي الله عنه ، قَالَ : جلس رسولُ الله صلى الله عليه وسلم عَلَى    الْمِنْبَرِ ، وَجَلَسْنَا حَوْلَهُ ، فقال : (( إنَّ ممَّا أخَافُ عَلَيْكُمْ مِنْ بَعْدِي مَا يُفْتَحُ عَلَيْكُمْ مِنْ زَهْرَةِ الدُّنْيَا وَزِينَتِهَا )) متفقٌ عَلَيْهِ .

Imepokewa kutoka kwa Abu Sa'iyd al-Khudriy (رضي الله عنه)   amesema: Alikaa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwenye mimbar nasi tukakaa duara (tukiwa tumemzunguka), akasema: "Kwa hakika yale ninayowaogopea nyinyi baada yangu ni kufunguliwa kwenu utajiri na kuvutiwa na dunia na mapambo yake." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Share