Wasifu Wa Ibn Sina (Avecenna) Na 'Aqiydah Yake

 

Wasifu Wa Ibn Sina (Avecenna) Na 'Aqiydah Yake 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Jina hasa la Ibn Sina ni Abu 'Ali Al-Husayn bin ‘Abdillaah bin Sina.

 

 

Alizaliwa mwaka 980 katika mji wa Afshana karibu na mji wa Bukhara. Na wengine wanasema alizaliwa mji wa Balkh huko Afghanistan, mamake alikuwa raia wa Fursi na babake mkusanyaji kodi kutoka Balkh chini ya Ibn Mansuwr, Amiri wa Bukhaara. Alifariki huko Khurasan, mwaka wa 1037 katika mji wa Hamdan.

 

 

Alikuwa akijulikana kwa jina la Kilatini kama Avicenna. Baada ya kuzaliwa kwa ndugu yake mdogo, familia yake ilihamia Bukhaara, mji mkubwa kati ya miji ya Kiislamu wakati huo.

 

 

Ibn Sina aliwekwa chini ya mwalimu, akili yake ilikuwa nzuri hivyo kuhifadhi Qur-aan akiwa na miaka kumi na pia kuhifadhi mashairi mengi ya Kiarabu. Kutoka kwa muuzaji duka alijifunza hesabu, na kujifunza mengi kwa mwanazuoni aliyekuwa akitanga tanga na kupata riziki yake kwa kutibu wagonjwa na kuwafundisha watoto. Hata hivyo, alisumbuliwa sana na matatizo ya metafizikia -metaphysical - (falsafa ya kuchunguza chanzo cha uhai na maarifa, udhanifu) na hasa kazi ya Aristotle ambaye ni mwanafalsafa wa ki-Giriki aliyekuwa mwanafunzi wa Plato na alikuwa huyo Aristotle ni mwalimu wa Alexander the Great. Kwa muda wa mwaka na nusu, alisoma falsafa, ambayo kwayo alipata vikwazo vingi. Katika hali hiyo alikuwa anaacha vitabu, anachukua wudhuu, kisha kuelekea Msikitini na kuendelea huko na Swalaah hadi Alfajiri. Katika nyakati za usiku alikuwa anaendelea na masomo, huku akiamsha hisia zake kwa vikombe vya mvinyo (pombe). Na hata usingizini shida zilikuwa zinamuandama na kutafuta suluhisho. Alisoma mara 40 metafizikia ya Aristotle kama inavyosemekana, mpaka akayahifadhi maneno yake, lakini maana yake hayakuwa wazi kwake mpaka alipopata mwangaza kwa sharh (ufafanuzi) ndogo ya kuhusu maudhui hiyo kutoka kwa al-Farabi (Alpharabius, ambaye alikuwa ni mwanasayansi na mwanafalsafa mkubwa).

 

 

Alianza kusoma utabibu (udaktari) akiwa na miaka 16 na kupata hadhi ya daktari akiwa na miaka 18. Alipata umaarufu mkubwa kwa muda mchache huku akiwatibu wagonjwa bure.

 

Alipata misukosuko katika vipindi tofauti. Alipokuwa na miaka 22 babake aliaga dunia. Alikataa ombi la Sultan Mahmuwd wa Ghazni, hivyo kuelekea Magharibi mpaka Urjensh na hapo waziri aliyetambulikana kama rafiki wa wanazuoni alimpatia usaidizi mdogo wa kifedha kila mwezi. Usaidizi huo ulikuwa mdogo hivyo kumfanya atangetange kutoka sehemu moja hadi nyingine katika wilaya za Nishapur na Merv mpaka akafika katika mipaka ya Khurasan akitafuta kazi kwa talanta zake alizokuwa nazo. Alipita Dailam ambako alitarajia kupata hifadhi lakini Amiri mwenyewe aliuliwa katika mapinduzi yaliyofanyika wakati huo. Mwishowe alifika Gorgan, karibu na Bahari ya Caspian ambako alikutana na rafiki aliyemnunulia nyumba karibu na yake, naye akaanza kusomesha mantiki na falaki.

 

Baadaye alihamia Rai karibu na Tehran (Iran), ambako Majd ad-Dawlah, mtoto wa Amiri wa mwisho aliyekuwa akiendeshwa na mamake. Kwa mapigano yaliyokuwepo, Ibn Sina alihamia Qazwin na kisha kuelekea Hamdan. Hapo alipatiwa cheo cha uwaziri lakini kwa sababu ya migongano katika jeshi alizuiliwa na kufukuzwa. Ibn Sina alijificha kwa siku 40 katika nyumba ya Shaykh mmoja, mpaka Amiri akashikwa na ugonjwa upya, pindi alipotibiwa alimrudisha tena katika cheo chake cha uwaziri. Aliendelea kufundisha wanafunzi wake na usiku alikuwa akijiliwaza na kujifurahisha kwa kutumbuizwa na kikosi cha waimbaji. Pindi Amiri alipofariki, alikosa cheo chake, hivyo kujificha katika nyumba ya mfamasia, pahali ambapo kwa uangalifu mkubwa sana aliendelea na utunzi wa kazi zake.

 

Wakati huo kulikuwa na mapambano makali baina ya dola ya Isfahan na Hamdan, hivyo kumfanya (Ibn Sina) kufungwa Hamdan. Baada ya Isfahan kushinda Ibn Sina alibaki Hamdan kwa muda lakini baadaye alikimbilia Isfahan. Kwa muda wa miaka 10 hadi 12, Ibn Sina alibaki katika utumishi wa Amiri wa Isfahan, Abu Ya‘far ‘Alaa ad-Dawlah kama daktari wake. 

 

Katika masomo yake Ibn Sina hakusahau mapenzi yake ya starehe. Mapenzi yake makubwa kwa unywaji pombe na wanawake yalikuwa mashuhuri kama usomi na ucheshi wake, kujigamba kwake na starehe. Starehe hizi zilimfanywa apatwe na ugonjwa wa msokoto wa tumbo (colic), hivyo kuaga dunia kwa maradhi hayo kushtadi.

 

 

Marafiki zake walimshauri aende polepole na anasa lakini alikataa katakata huku akisema: “Napendelea maisha mafupi ya upana kuliko membamba yenye urefu”. Akiwa kitandani alijuta, akatoa vitu vyake kwa masikini, akatoa vitu alivyopata kwa dhuluma, akaacha huru watumwa na kuanza kusikiliza kwa kisomo cha Qur-aan mpaka alipoaga dunia. Ibn Sina anafananishwa na waliobobea katika fani tofauti kama Abubakr Muhammad bin Zakariya ar-Razi.

 

Asili yake inasemwa na wengine ni mu-Uzbeki, wengine ni mu-Afghani, wengine ni Mfursi Shia na hata Ismailiya wanadai ni mfuasi wa itikadi yao ya Ushia Ismailiya. Alitangaa sana katika elimu ya falaki, kemia. Mantiki, hesabu, udaktari, ushairi, sayansi, theolojia, mzungumzaji hodari, mwanajeshi, na alikuwa amebobea zaidi katika udaktari na falsafa wakati wake.

 

 

Aliandika takriban vitabu 450 katika maudhui tofauti, lakini alijikita zaidi katika falsafa na utabibu. Kazi yake iliyo maarufu zaidi ni Kitabu cha Uponyo na Kanuni ya Tiba, ambavyo vilikuwa ni vitabu rejea vya udaktari katika Vyuo Vikuu katika nchi za Waislamu na Bara Ulaya mpaka katika karne ya 18. Ibn Sina alikuza mfumo wa utabibu uliochanganya uzoefu wake na ule wa utabibu wa Kiislamu, mfumo wa utabibu wa akina Galen, Aristotle na utabibu wa kale wa Kifursi, Kiarabu na wa Kihindi. Ibn Sina anachukuliwa kama baba wa udaktari wa sasa, hasa katika kuanzisha mfumo wa majaribio na kuchukua hima maalumu katika masomo ya fuzuilijia na kuvumbua kwake maumbile ya kuambukizana magonjwa.

 

 

George Sarton, baba wa historia ya sayansi ameandika katika Utangulizi wa Historia ya Sayansi: “Mmoja wa wasimamizi maarufu wa kilimwengu kati ya Waislamu na mtu mashuhuri katika masomo ya Kiislamu ni Ibn Sina, aliyejulikana Magharibi kama Avicenna (980 - 1037). Kwa muda wa miaka elfu moja amebaki katika umaarufu wa kiasili kama mwanafalsafa mkubwa zaidi na mwanachuoni wa utabibu katika historia. Kazi yake muhimu zaidi katika udaktari ni Qanun (Kanuni) na waraka kuhusu dawa za magonjwa ya moyo. Kitabu chake ‘Qanun Fiyt Twib’ (The Canon of Medicine) vikubwa sana katika mas-ala ya utabibu. Anaelezea fikra zilizo wazi na kung’ara kuhusu tofauti ya mediastinitis kutoka na pleurisy; maumbile ya maambukizo ya phthisis; kusambazwa kwa ugonjwa kupitia kwa maji na mchanga; uelezaji wa kimakini wa matatizo ya ngozi; magonjwa ya zinaa na uasherati na magonjwa ya mishipa” (George Sarton, Introduction to the History of Science. (cf. Dr. A. Zahoor and Dr. Z. Haq (1997). Quotations From Famous Historians of Science, Cyberistan.)

 

 

Huko Iran, anachukuliwa ni shujaa wa Kifursi. Anatambulika kama mmoja wa Wafursi wakubwa aliyeishi duniani. Taswira na sanamu zake nyingi zinapatikana Iran leo. Sanamu lake moja laonyesha maisha na kazi kwa mtu anayejulikana kama ‘daktari wa madaktari’ bado linasimama nje ya jumba la ukumbusho huko Bukhara na taswira yake inaning’inia katika ukumbi wa Kitengo cha Udaktari katika Chuo Kikuu cha Paris, Ufaransa.

 

 

Anachukuliwa kama mwanazuoni mkubwa kati ya wanazuoni wanne wakubwa wa Mu‘tazilah, wengine wakiwa ni al-Kindi, al-Farabi na Ibn Rushd. Japokuwa inasemekana kuwa alikuwa Mshia wa dhehebu la Ismailiyah (Agha Khan/ Makoja).

 

 

Falsafa

 

Ibn Sina aliandika sana katika masomo yafuatayo; falsafa, mantiki, adabu, Dini na nyanja nyingine tofauti. Vitabu vyake vingi viliandikwa kwa lugha ya Kiarabu – ambayo ilikuwa ni lugha ya kipekee ya kisayansi kwa wakati wake huo na kazi zake nyinginezo ziliandikwa kwa Kifursi. Tafsiri ya Ibn Sina kuhusu Aristotle mara nyingi ilikuwa ni kumkosoa na kumrekebisha, hivyo kuhimiza mjadala hai kwa roho ya Ijtihaad.

 

 

Itikadi za kifalsafa za Ibn Sina zimewafanya wahakiki wasomi wa Kimagharibi kuwa na hamu kubwa na pia wale walio katika nyanja ya falsafa za Kiislamu, kote Magharibi na Mashariki. Hata hivyo, Magharibi inashughulika tu na sehemu ya falsafa zake zinazojulikana kama Chuo cha Avicenna cha Kilatini. Mchango wa falsafa za Ibn Sina zimefunikwa na usomi wa Kiorientalisti (ubobezi katika mambo ya Wamashariki) kwa mfano zile za Henri Corbin, ambazo zimetaka kumuelezea kama mtawa wala sio mwana-falsafa wa falsafa ya Aristotle. Ile inayojulikana kama Hekima ya Kimashariki imebaki kuwa chimbuko la maudhi makubwa kwa wanazuoni wa Kiarabu hasa Reisman, Gutas, Street na Bertolacci.

 

 

Kazi asili iliyojulikana Wamashariki (al-Mashriqiyyuun), ilipotea katika uhai wake, Ibn Sina; Ibn Tufayl aliiunganisha katika kazi yake ya falsafa ya kimapenzi katika karne ya 20, ili kuufanya mfumo wake wa kifalsafa ukubalike. Pindi tu kazi hiyo ilipofasiriwa, pamoja na kiambatanisho, ilikubaliwa kama mfumo wa Ibn Sina, ambao aliuficha kwa maslahi kutoka kwa mahirimu wake.

 

 

Wengine wanajadili kuwa tafsiri hizo za hali halisi ya akili kwa Ibn Sina inapuuza kazi nyingi na kubwa alizoandika, kutoka nyaraka kuu muhimu kuwapaka matope maadui na mahasimu wake, zinamweleza vibaya kabisa. Pia zinageuza ile hamu, kwa uhakika kuwa falsafa ya Kiislamu ilinawiri katika karne kumi baada ya kuaga dunia Ibn Sina.

 

 

Itikadi za Kimetafizikia

 

Falsafa ya Kiislamu, iliyojazwa teolojia, ina tofauti ya wazi na falsafa ya Aristotle kwa ile tofauti baina ya asili na kuwepo. Ilhali kuwepo ni sehemu ya uwezekano wa kitu kutokea na bahati, asili ipo katika kiumbe zaidi ya bahati. Hata hivyo, tafsiri ya Ibn Sina hasa katika metafiziki inaonyesha wazi kuwa alikuwa ameshika ule ufahamu wa falsafa ya ulimwengu wa metafiziki zaidi kuliko teolojia. Falsafa ya Ibn Sina, hasa katika ile sehemu inayohusiana na metafiziki anachukua zaidi kutoka kwa Aristotle na al-Farabi. Upekuzi wa falsafa ya Kiislamu ya kweli yaweza kuonekana katika mabaki ya kazi zake zilizobakia nasi. 

 

Allaah kama sababu ya kila kitu:

 

 

Kwa Ibn Sina, asili ni kutowepo uwezekano. Kwa asili kutokea kwa wakati maalumu (kama kuwepo), kuwepo ni lazima kuwe ni mahitaji na asili yenyewe. Uhusiano huu wa sababu na athari ni kwa ajili ya sifa iliyopo ya asili, ambayo haipo. Kwa kuwepo kutokea kijumla, ni lazima kuwepo asili muhimu, ambayo yenyewe haina sababu – kiumbe au Muumbaji kuanzisha mfumo wa kuanzia.

 

Muono huu una athari kubwa kwa ufahamu wa umoja wa uumbaji. Kuwepo hakuonekani na Ibn Sina kama kazi ya Allaah, lakini wa kimungu, muundo wa fikra ya kujileta yenyewe. Uelekeaji wa hili hadi kuwepo ni muhimu, na sio amali ya kutaka tu. Ulimwengu umetoka kwa Muumbaji kwa ile sifa yake ya kuwa na akili nyingi – sababu isiyo ya kimada kama inavyopatikana kwa mfumo mpya wa kuanzia wa Plato (mwanafalsafa wa ki-Giriki). 

 

Ibn Sina alipata hima kwa muono huu wa kimetafizikia kwa kazi za al-Farabi lakini uzushi katika fikira yake moja na muhimu, sababu ya kwanza ya kuwepo kila kitu. Ikiwa muono huu unaweza kusawazishwa na Uislamu, hasa ukichukua swali la ubakio na hiari kwa jukumu la Muumba. Hiyo ikawa ni maudhui ya ubishani mkali kati ya mihadhara ya Kiislamu.

 

 

Akili kumi

 

Kwa fikra ya Ibn Sina kuhusu uumbaji (iliyotolewa zaidi kutoka kwa al-Farabi), kwa ile sababu yake ya kwanza (au Akili ya Mwanzo) inatokana ya uumbaji wa ulimwengu wa kimada.

 

 

Akili ya Kwanza, katika kutafakari umuhimu wa kuwepo, inaleta Akili ya Pili. Katika kutafakari kutokea kutoka kwa Mungu, inaleta Roho ya Kwanza, ambayo inaleta uhai katika ulimwengu. Katika kuitafakari yenyewe kama asili iliyojitokeza (hiyo ni, kama kitu ambacho kina uwezo wa kuwepo), kinaleta kutokea kwa kitu ambacho kinajaza ulimwengu wote, hivyo kutengeneza Sayari (Uwingu wa Kwanza katika al-Farabi).

 

 

Kutafakari huku kutatu kunaanzisha vituo vya mwanzo vya kuwepo. Inaendelea kukuuza akili muhimu zinazofanya baina yao misonge miwili ya mbinguni: Msonge wa Juu wa Cherubi (Malaika) na Msonge Duni, ulioitwa na Ibn Sina ‘Malaika Watukufu’. Malaika hawa wanaleta uhai mbinguni, lakini wanakoseshwa hisia zote za uoni, lakini wana utambuzi unaowaruhusu kutamani akili waliokuja kutoka kwayo. Utafutaji wao kujiunga na akili kunafanya mbingu daima kutembea. Pia wanasababisha ndoto za unabii kwa wanaadamu.

 

Malaika walioumbwa na kila moja ya akili saba zilizobakia zinahusishwa na Sayari tofauti. Hizo ni: Saturn, Jupiter (Sumbula), Mars, Sun (Jua), Venus (Zuhura), Mercury (Zebaki) na Moon (Mwezi). Ya mwisho ndio iliyo muhimu, kwa kule kufungamanishwa na Malaika Jibriyl.

 

 

Akili ya Tisa ipo katika sehemu iliyotolewa mbali na Akili ya Kwanza kwa kiasi ambacho kule kutoka unaopaa juu kutoka kwayo unalipuka vipande vipande, hivyo kutotengeneza mbingu nyingine lakini badala yake kutengeneza roho za wanaadamu, wenye hisia zilizokosekanwa na Malaika Watukufu.

 

 

Malaika na akili za Wanaadamu

 

Kwa Ibn Sina, akili za mwanaadamu hazikuwa ni zenye kutengenezwazo wenyewe kutoka kwa fikira ya dhana. Wanaadamu wana akili tu kwa uwezo, na ni mwangaza tu na Malaika unaowapatia uwezo wa kufanya hilo kuwa ni uwezo wa kihakika wa kufikiria. Hii ni Akili ya Kumi, iliyotambulika na ‘akili tendaji’ ya Aristotle De Anima.

 

 

Kiasi ambacho akili zinamulikwa na Malaika zinatofautiana. Manabii wanamulikwa kwa kiwango cha kuwafanya wao wasiwe ni wenye kuwa na akili ya mantiki tu, lakini pia utambuzi na uwezo unaowaruhusu kufikisha busara yao njema kwa wengine. Wengine wanapata kidogo, lakini inayotosha kuandika, kupitisha sheria na kuchangia katika kusambaza elimu. Wengine wanapata ya kutosha kwa matumizi yao tu, ilhali wengine wanapata kidogo zaidi.

 

 

Kwa muono huu, walimwengu wote wanashirikana kwa ajenti mmoja – akili, utambuzi na hisia za pamoja. Kiwango cha mwisho kwa maisha ya mwanaadamu, kulingana na Ibn Sina, ni muungano unaotokea kwa Malaika. Hivyo, Malaika anawapatia wenye akili uhakikisho wa maisha baada ya kifo. Kwa Ibn Sina, kama walivyo Waplato mamboleo waliomuathiri, udawama wa roho ni kwa ajili ya maumbile yake, na sio lengo kwayo kutekelezwa.

 

Mashairi

 

Takriban nusu ya kazi za Ibn Sina ni katika utungo wa mashairi. Mashairi yake yanapatikana kwa lugha zote mbili – Kiarabu na Kifursi.

 

 

Walivyosema wanazuoni kuhusu Ibn Sina

 

Itikadi tofauti za Ibn Sina, mfano itikadi yake kuwa ufufuo wa kimwili hauwezekani, ulimweka yeye dhidi ya wanazuoni wenye misimamo asilia wa wakati wake. Kukengeuka huku kutoka katika fikira ya Imani halisi, hilo lilimfanya mwanazuoni mashuhuri Imaam al-Ghazaaliy kutangaza kuwa Ibn Sina ni kafiri, na akashikilia ufaradhi wa kumchukulia hivyo. Amesema hayo katika kitabu chake ‘Munqidh minadh-Dhwalaal’ uk. 44-45.

 

Wapo wanazuoni wengi wengine waliomkufurisha kwa sababu ya Itikadi zake. Baadhi yao baada ya kumtaja Imaam al-Ghazaaliy ni kama wafuatao:

 

  • Imaam adh-Dhahabiy amesema yafuatayo katika kitabu chake Siyaar A‘alaam an-Nubalaa, “Yeye ana kitabu kwa jina ash-Shifaa’ (Ponyo), ambacho kina vitu visivyoweza kuvumilika, na al-Ghazaaliy amemkufurisha katika kitabu chake Munqidh Min Adh-Dhwalaal”. Katika kitabu chake kingine adh-Dhahabiy amesema, “Sina habari yake kuwa alihadithia chochote kuhusu sayansi za Kiislamu, na hata kama angefanya hivyo, haingefaa kupokea kutoka kwake kwani alikuwa mwana-falsafa aliyekengeuka na mpotovu” [Miyzaanul ‘Itidaal, 1/ 5391] 

 

  • Al-Haafidh Ibn Hajr amesema, “Mwanazuoni wa Ki-shaafi‘iy, Ibn Abi al-Hamuwiy amesema: Wanazuoni wamekubaliana kuwa Ibn Sina alikuwa anasema kuwa ulimwengu umekuwepo daima na kuwa watu hawatafufuliwa na miili yao Siku ya Qiyaama. Pia amesema kuwa Allaah Hana elimu ya kila kitu, bali Anajua tu yale yanayotokea kiujumla. Hivyo, wanazuoni wa wakati wake na wale baada yake, wanazuoni ambao kauli zao zina uzito katika mas-ala ya Fiqh na Misingi ya Fiqh kwa pamoja wamemtangaza yeye na al-Farabi kuwa makafiri kwa sababu ya itikadi kuhusu mambo hayo yanayokwenda kinyume na Imani ya Kiislamu” [Lisaanul Miyzaan, 2/293].

 

  • Naye Abul Faraj ‘Abdur-Rahmaan bin al-Jawziy amesema katika kitabu chake mashuhuri, Talbiys Ibliyis kukanusha ya Ibn Sina na Mu’tazilah: “….. Wengi wa wana-falsafa wamechukua ule muono kuwa Allaah Ta‘ala hana elimu isipokuwa ya Dhati Yake japokuwa inajulikana kuwa viumbe wana elimu ya nafsi zao na pia elimu ya Muumbaji hivyo wamepatia viumbe cheo kikubwa zaidi kuliko Muumbaji. Mwandishi Yahya bin Bishr Nihawandi amesema kuwa kwa kauli hii utwezo wa Itikadi upo wazi. Hakuna haja ya kuongeza kauli nyingine yoyote. Hii inahitaji kuzingatiwa juu ya hakika jinsi gani Iblisi anavyodanganya wajinga. Mbali na ile hakika kuwa watu hawa wanadai kuwa na elimu na akili timilifu. Ibn Sina yuko dhidi yao katika Itikadi hii. Yeye anasema, si hivyo bali Allaah Ana ilimu ya Nafsi Yake na pia elimu ya vitu vyote lakini Allaah Hana elimu ya ndani kuhusu hivyo. Madh-hab hii imechukuliwa na Mu’tazilah kutoka kwa watu hawa”.

 

  • Ibn Kathiyr amesema kuwa ni kwa sababu ya Itikadi zake ndipo al-Ghazaaliy akamkufurisha [Al-Bidaayah wan Nihaayah, 12/ 46].

 

  • Ibn Taymiyah naye amemkufurisha Ibn Sina kwa zile Itikadi zake alizokuwa nazo.

 

  • Shaykh ‘Abdul-‘Aziz bin ‘Abdallah Ar-Raajihiy naye ameweka wazi ukafiri wa Ibn Sina.

 

 

Hata hivyo, kuna baadhi ya wanazuoni wachache kama Ibn Hajar katika kitabu chake cha Liysaanul Miyzaan ambacho kinazungumzia watu mbalimbali katika upande wa kujeruhi, ambacho kimepangwa kwa mfumo wa ‘Alifbaaiyah’ (mpangilio wa ki-Alfabeti) amemuelezea kuwa mwisho wa uhai wake alipozidiwa sana na ugonjwa alioga akatubu na kuomba sana. Pia inasemekana Ibn Khalduun katika kitabu chake cha ‘Muqadimah Ibn Khalduun’ au cha ‘Taariykh Ibn Khalduun’ (ingawa hatukuweza kuona kipengele hicho kwa haraka) ni miongoni mwa waliosema kuwa alitubu mwisho wa maisha yake.

 

 

 

 

Share