Uongofu (Alhidaaya)

 

Uongofu (Alhidaayah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Kulingania Kwa Allaah (ad-da’watul Ilaa Allaah)

 

Haja ya Watu katika Dini ni sawa na haja ya mwili kwa roho, kama ambavyo ikikosekana roho mwili unaharibika, hivyo hivyo Ummah utakapokosa Dini utaharibika.

 

Rehma ya Allaah imeenea katika kila kitu, na rehma Zake kwa waja Amewatumia Mitume na Akawashushia vitabu ili wawafundishe watu wamjue Mola wao mwenye kuwaruzuku, wawabainishie Anayoridhia na wawalinganie katika kumtii na kumuabudu Yeye peke Yake bila ya kumshirikisha na chochote. Pia wawafahamishe Aliyowaandalia Rabb katika Thawabu (Ujira) kwa atakayemtii na adhabu kwa atakayemuasi.

 
Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

 ۖ فَمِنْهُم مَّنْ هَدَى اللَّـهُ وَمِنْهُم مَّنْ حَقَّتْ عَلَيْهِ الضَّلَالَةُ ۚ

 

Basi miongoni mwao ambao Allaah Amewahidi, na miongoni mwao ambao umethibiti kwake upotofu. [An-Nahl: 36]

 

Kila walipodhoofika watu na kuingia katika shirki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alituma Rusuli wanaowalingania katika Tawhiyd na kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) peke Yake.

 

Walifuatana kuja Rusuli na kila mmoja alitumwa kwa watu wake maalum, mpaka alipotumwa mwisho wa Rusuli Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Alitumwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini ya haki kwa watu wote, akafikisha ujumbe, akatekeleza amana, akanasihi Ummah, akapigana katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), akaacha Ummah katika sehemu ya wazi hapotei ila mpotevu.

 

Alilingania Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) miaka 23 alianzia bara Arabu kulingania mwanzo nyumbani kwake, kisha ndugu wa karibu kisha kabila lake, kisha watu wa Makkah na pembezoni, kisha watu wote. Wakaingia watu katika Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) makundi kwa makundi.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٢٨﴾

 

Na Hatukukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa kwa watu wote uwe mbashiriaji na muonyaji, lakini watu wengi hawajui. [Sabaa: 28]

 

Pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٧﴾

 

Na Hatukukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa ni rahmah kwa walimwengu. [Al-Anbiyaa: 107]

 

 

Sababu Za Uongofu

 

Watu waliingia katika Uislaam enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuathirika na sababu nyingi, miongoni mwazo:

 

I.          Ulimi

 

Kulingania kwa ulimi, kama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomlingania Abu Bakr, Khadiyjah, ‘Aliy, (Radhwiya Allaah ‘anhum) na wengineo wakasilimu.

 

II.          Elimu

 

Kama alivyoongoka ‘Umar bin Al-Khatwaab alipoathirika na Qur-aan aliyoisoma katika nyumba ya dada yake Faatwimah alipowakuta wanasomeshwa na mumewe Sa’iyd bin Zayd.

 

 

III.          ‘Ibaadah

 

Alivyosilimu Hind bint ‘Utbah alipoona Waislamu wanaswali mwaka wa

Na kama alivyosilimu Thumaamah bin Athaal Al-Hanafiy katika msikiti wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipoathirika na ‘ibaadah.

 

 

IV.          Kutoa Na Ukarimu

 

Kama alivyompa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ‘Aaamul Fat-h Swafwaan bin Ummayah, Mu’aawiyah na wengineo mali nyingi, wakasilimu. Pia aliyepewa mbuzi baina ya majabali mawili ikawa sababu ya kusilimu yeye na watu wake.

 

Kwa wakati wetu wa sasa kuna njia nyingi za kufikia Uongofu mfano: Mtandao; tovuti za kila Lugha, Kanda za Mawaidha, Darsa, Mihadhara, Semina, Vitabu, Magazeti, Majarida n.k.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ameukirimu Ummah huu kwa kuwapa wadhifa wa Rusuli na Manabiy wa kulingania (Da’wah) katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) mpaka itakaposimama Qiyaamah.

 

Alijitahidi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) mpaka walifikia mambo mawili:

 

i.          Kusimamisha Dini katika maisha yao.

 

ii.         Kusimamisha Dini katika maisha ya watu.

 

Walikuwa wanaelewa kuwa Da’wah ni jukumu la Ummah, na kila Muislamu, atahesabiwa kwa kuaacha majukumu yake binafsi ya ‘ibaadah, na majukumu ya kijamii ya Da’wah.

 
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ ۗ وَلَوْ آمَنَ أَهْلُ الْكِتَابِ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُم ۚ مِّنْهُمُ الْمُؤْمِنُونَ وَأَكْثَرُهُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿١١٠﴾

 

Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah. Na lau wangeliamini Ahlul-Kitaabi ingelikuwa ni bora kwao, miongoni mwao wanaoamini na wengi wao ni mafasik. [Aal ‘Imraan: 110]

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفلِحُونَ ﴿١٠٤﴾

 

Na watokeze kutoka kwenu umati wa watu unaolingania khayr na unaoamrisha mema na unaokataza munkari. Na hao ndio waliofaulu. [Aal ‘Imraan: 104]

 

Na katika Suwrah Yuwsuf Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema: 

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٠٨﴾

 

Sema: Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah, juu ya nuru za elimu na umaizi, mimi na anayenifuata. Na Utakasifu ni wa Allaah, nami si miongoni mwa washirikina. [Yuwsuf: 108]

 

 

Uoni (Baswiyrah) Ni Katika Mambo Matatu

 

 

·       Elimu kabla ya Da’wah (Ulinganiaji)

 

·       Ulaini pamoja na Da’wah

 

·       Subra baada ya Da’wah

 

 

Walipokea Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) majukumu ya Da’wah na njia zake, wakaacha matamanio na raha zao, wakajitolea nafsi, mali na wakati wao kueneza Dini Ulimwenguni.

 

Ukaenea Uislaam mashariki na magharibi, miji ikafunguliwa, Tawhiyd ikaenea shirki ikaondoka. Wakadhihiri ‘ulamaa na Walinganiaji. Hao ni kheri ya karne Amewasifu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٠٠﴾

 

Na wale waliotangulia awali (katika Uislamu) miongoni mwa Muhajirina na Answaar na wale waliowafuata kwa ihsaan; Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo abadi. Huko ndiko kufuzu adhimu. [At-Tawbah: 100]

 

Ili Uongofu uenee inabidi waliobeba jukumu la Da’wah wawaige wema waliopita.

 

 

Kukosekana Uongofu

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walipotanguliza Juhudi na Da’wah kuliko kuchuma na kutafuta vitu vya halali, yalipungua katika maisha yao vitu na mali. Lakini Imani yao ilizidi na matendo mema, ikadhihiri uhakika wa Tabia njema, miji mingi ikafunguliwa (ikawa chini ya Uislaam).

 

Waislamu wa leo walipotanguliza kutafuta mali (kuchuma) kuliko Da’wah, ikawazidia vitu na mali wakadhoofika katika imani na matendo yakapungua.

 

Yakaja mambo mawili katika maisha yao:

 

a.     Kukazana (kufanya) bidii katika kukusanya mali kama Mayahudi.

 

b.     Kufuata matamanio kama Manaswara.

 

Ilipobadilika makusudio, ikapata nguvu upande wa Dunia, ikadhoofika Dini na roho, ikawa pupa ni ya dunia sio ya Dini. Dini ikawa Yatima apitaye kwa watu hapati wa kumlea kwani watu wameshughulishwa na dunia na matamanio.
 

Dini hii itabaki mpaka siku ya Qiyaamah, wanasimamia kundi Umati Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka itakapokuja amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Imekuja katika Hadiyth kutoka kwa Mu’aawiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema, nimemsikia Nabiy (Swalla Alaahu ‘alayhi wasallam) akisema:

 

“Halitoacha kundi katika Ummah wangu unasimamia jambo la Allaah, haitawadhuru wenye kuwapinga mpaka ije amri ya Allaah nao bado wapo wazi kwa watu.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Fadhila Za Kulingania Kwa Ajili Ya Allah Mtukufu

 

Kila mwenye kuamini na akasimamia ‘Ibaadah na kulingania kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), basi Allaah Atamkirimu, miongoni mwazo kutukuzwa hata kama hana sababu za kutukuzwa mfano Bilaal na Salmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa), na Atajaalia matendo ya Dini yote ni yenye kupendeza kwake anayatekeleza na kulingania, na Atajaalia Allaah mapenzi katika nyoyo za viumbe (wampende), na Atamuunga mkono, Atamjibu du’aa zake, Atamjaalia haiba, Atampa ujira mfano wa Aliowalingania na wakaongoka kupitia Kwake, Atamruzuku Msimamo (istiqaamah) na uongofu (alhidaaya).

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴿٣٣﴾

 

Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania kwa Allaah na akatenda mema na akasema: Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu. [Fusw-swilat: 33]

 
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa wasallam) amesema:

 

“Mwenye kulingania kheri atapata ujira mfano wa ujira wa wenye kufuata bila kupungua ujira wao chochote, na mwenye kulingania katika upotevu atapata madhambi mfano wa madhambi ya watakaomfuata bila kupunguziwa madhambi yao chochote.” [Muslim]

 
Amepokea Sahl bin Sa’ad (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuambia ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) siku ya Khaybar:

 

“…nenda taratibu mpaka uwafikie uwanjani mwao, kisha uwalinganie Uislam, na uwafahamishe yaliyo wajibu kwao katika haki za Allaah. Naapa kwa Allaah Akikuongozea Allaah mtu mmoja ni bora kwako kuliko kumiliki Ngamia mwekundu (waarabu zamani walikuwa wanaona ni mali ya thamani sana ni utajiri kuwa na ngamia).” [ Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Watu Katika Matendo Ni Namna Mbili

 

1.       Miongoni mwao yuko aliyejitahidi katika Dunia kisha akaondoka na kuiacha.

 
2.       Na yuko mwengine aliyejitahidi katika Akhera yake na akaikuta. Nao ni namna mbili:

 

a).     Aliyejishughulisha na ‘Ibaadah na Da’wah kwa ajili ya Allaah akajitolea kueneza neno la Allaah, huyu matendo yake ni yenye kuendelea, kwani kila aliyeongoka kwa sababu yake anapata ujira mpaka siku ya Qiyaamah.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 أَجَعَلْتُمْ سِقَايَةَ الْحَاجِّ وَعِمَارَةَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ كَمَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَجَاهَدَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ لَا يَسْتَوُونَ عِندَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ﴿١٩﴾ الَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ أَعْظَمُ دَرَجَةً عِندَ اللَّـهِ ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ﴿٢٠﴾ يُبَشِّرُهُمْ رَبُّهُم بِرَحْمَةٍ مِّنْهُ وَرِضْوَانٍ وَجَنَّاتٍ لَّهُمْ فِيهَا نَعِيمٌ مُّقِيمٌ﴿٢١﴾ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ﴿٢٢﴾

 

Je, mmefanya kunywesha maji Hujaji na kuamirisha Al-Masjid Al-Haraam kama sawasawa na (‘amali za) anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho, na akafanya jihaad katika njia ya Allaah? (Hapana!) Hawawi sawa mbele ya Allaah. Na Allaah Haongoi watu madhalimu. Wale walioamini na wakahajiri na wakafanya jihaad katika njia ya Allaah kwa mali zao na nafsi zao; wana daraja kuu kwa Allaah. Na hao ndio waliofuzu.  Rabb wao Anawabashiria kwa rahmah kutoka Kwake na radhi na Jannaat, watapata humo neema zenye kudumu. Ni wenye kudumu humo abadi. Hakika Allaah Kwake kuna ujira adhimu. [ At-Tawbah: 19-22]

 

b).     Aliyejishughulisha na ‘Ibaadah pekee, yanakatika matendo yake ila matatu:
Sadaka yenye kuendelea, elimu yenye manufaa, mtoto mwema anayemuombea du’aa baada ya kufa.

 

 

WabiLlaahi At-Tawfiyq.

 

Share