Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Katika Uislam - 02

 

Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Katika Uislaam- 02

 

Imefasiriwa na: Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Suala Nambari 2 Linaloeleweka Vibaya.

 

Ndani ya Uislaam, hakuna tatizo kukataa haki za binaadamu kwa sababu:

 

  • Uislaam unapingana na demokrasia iliyo safi.​

 

  • Uislaam unakubaliana Na utumwa.

 

Jibu

 

Suala hilo haliendani na hoja zilizotolewa, na hoja hizo zinaacha habari zilizo nyingi kabisa.

 

Kama ilivyoelezwa awali, Uislaam ni njia iliyokamilika ya maisha. Kwa hili, sio jambo la kushangaa kwamba Allaah Ametuchagulia mwenendo ambao tutahitaji kujitawala. Kanuni kuu ambayo Taifa la Kiislamu ni lazima kuichunguza inaelezwa ndani ya Qur-aan:

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

 

Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. [An-Nisaa: 59]

 

Kutokana na Aayah hii, ni wazi kwamba lengo la taifa katika utiifu kwa Allaah ni muhimu kama ambavyo ulivyo unyenyekevu kwa kila mtu. Hivyo, ni lazima kwa Taifa la Kiislamu kutunga sheria zake kutokana na Qur-aan na Sunnah. Kanuni hii inazuia Taifa la Kiislamu kuwa na hiari ya kuchagua mfumo wa siasa na uchumi, kama vile demokrasia safi, ubepari usiokuwa na kizuizi, ukomunisti, ujamaa, n.k. Kwa mfano, demokrasia safi inawaweka watu juu ya Qur-aan na Sunnah, na hili ni utomvu wa utiifu kwa Allaah. Hata hivyo, mbadala bora kwa demokrasia safi ni demokrasia ambayo inasimamisha na kutilia nguvu Shari’ah (Sheria ya Kiislamu).

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pia Anaeleza ndani ya Qur-aan:

 

 

فَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٣٦﴾وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُونَ﴿٣٧﴾وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣٨﴾

 

Basi chochote mlichopewa katika kitu ni starehe ndogo za uhai wa dunia.  Na yale yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi na ni ya kudumu kwa wale walioamini na kwa Rabb wao wanatawakali. Na wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu na wanapoghadhibika wao wanasamehe. Na wale waliomuitikia Rabb wao, wakasimamisha Swalaah, na jambo lao hushauriana baina yao, na kutokana na vile Tulivyowaruzuku wanatoa. [Ash-Shuwraa: 36-38]

 

Allaah Anatuamirisha ndani ya Aayah hii kufanya mambo yetu kwa kuchukua ushauri kutoka miongoni mwetu, au kwa mmoja kushauriana na mwengine. Huu ni utaratibu wa Taifa la Kiislamu; kushauriana, lakini ni lazima kuiweka Qur-aan na Sunnah kileleni. Sheria yoyote ambayo inapingana na Qur-aan au Sunnah ni batili. Kanuni hii iliyo pana ya kushauriana, hakika ni pana kabisa kuingiza mfumo wa serikali ambapo watu wote wana pata haki ya kusikilizwa, ingawa ukweli ni kwamba wanahamasishwa kusikilizwa. Mataifa ya kale ya Kiislamu yalikuwa katika mfumo huu. Leo, serikali nyingi zilizo dhaifu za “nchi za Waislamu” hazitumii kanuni hii na ukweli wanatenda makosa mengi ya jinai dhidi ya watu.

 

Ama kwa utumwa, Uislaam upo tofauti kabisa miongoni mwa dini nyengine; Uislaam una azma iliyojikita ndani kabisa, ya kuondosha utumwa kwa njia za salama. Kabla ya kuingia Uislaam, utumwa ulienea duniani kote. Nabiy wa Uislaam ametufundisha kwamba kuwaachia huru watumwa lilikuwa ni tendo bora kwa uoni wa Allaah. Kutokana na Sunnah, hususan ndani ya somo la Sunnah linaloitwa [Sahih Al-Bukhaariy], tunaona:

 

Amesimulia Abuu Hurayrah: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Yeyote anayeacha huru mtumwa aliye Muislamu, Allaah Ataviokoa viungo vyote vya mwili wake kutokana na Moto kama alivyoviachia huru viungo vya mtumwa.” Sa'iyd bin Marjana amesema kwamba ameisimulia Hadiyth hiyo kwa ‘Aliy bin Al-Hussain na kuachia huru mtumwa ambaye ‘Abdullaah bin Ja’far alikwishataka kumpatia Dirhaam alfu kumi au Dinaar alfu moja. [3:46:693]

 

Halikadhalika kutokana na Muwattwa ya Maalik, tunanukuu Hadiyth iliyosimuliwa na Mama yetu Ummul Mu’miniyn Aisha (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

 

Amesimulia Ummul Mu’miniyn 'Aaishah: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa ni mtumwa gani aliye bora kumuachia huru. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alijibu: “Mtumwa aliye ghali na mwenye thamani zaidi kwa bwana wake.” [Muwattwa Maalik: 38:9:15]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pia Amelifanya zoezi la kuwapatia uhuru wao watumwa, kuwa ni jepesi. Kutoka kwenye [Sahih al-Bukhaariy]:

 

Amesimulia Abuu Hurayrah: Nabiy amesema, “Yeyote anayesamehe sehemu ya mtumwa wake aliye muhimu basi amsamehe mtumwa huyo moja kwa moja kwa kulipa thamani yake iliyobaki kutoka kwenye pesa zake kama anazo pesa zinazotosha; ikiwa si hivyo, thamani ya mtumwa itakisiwa na mtumwa asaidiwe kufanya kazi bila ya uzito hadi atakapolipa thamani iliyobaki” [3:46:704]

 

Masharti ya utumwa ni tofauti kabisa ndani ya Uislaam kuliko yale masharti mazito yaliyolazimishwa na wasio kuwa Waislamu au Waislamu wasio watiifu. Kutoka katika [Sunan Abuu-Daawuud]:

 

Amesimulia Abuu Hurayrah: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asiseme miongoni mwenu: “Mtumwa wangu” (abdi) na “Mtumwa wangu wa kike” (amaati), na mtumwa asiseme: “Mtawala wangu” (rabbi au rabbati). Bwana (wa mtumwa) aseme: “Kijana wangu wa kiume” (fataya) na “Kijana wangu wa kike” (fataati), na mtumwa aseme: “Bwana wangu” (sayyidi) na “Bibi yangu” (sayyidati), kwani nyote ni watumwa (wa Allaah) na Mtawala ndie Allaah, Aliye Mkuu.” [41:4957]

 

Ama kutoka kwenye [Sahih l-Bukhaariy], tunaona katika hadiyth nyengine:

 

Amesimuliwa Al-Ma’ruur bin Suwaid: Nimemuona Abuu Dhar Al-Ghifari amevaa joho, na mtumwa wake pia, alikuwa amevaa joho. Tulimuuliza kuhusu hilo (yaani kwanini wote walikuwa wamevaa majoho yaliyofanana). Alijibu, “Mara moja nilimvunjia heshima mtumwa mmoja na alinishtakia kwa Nabiy. Nabiy akaniuliza, “Umemvunjia heshima kwa kumtukana mama yake?” Akaongeza,“Watumwa wenu ni ndugu zenu ambamo Allaah Amekupeni uongozi. Hivyo, kama mmoja ana ndugu mmoja chini ya uongozi wake, mmoja wenu awalishe kama ambavyo anavyokula, na kuwavisha namna ambavyo anavyovaa. Usiwakalifishe kwa yale ambayo hawawezi kuyahimili, na kama mkifanya hivyo, wasaidieni (kwenye kazi zao ngumu).” [3:46:721]

 

Matokeo ya mafundisho haya ya Uislaam ni kuwa; utumwa kwa kiwango kikubwa ulikaribia kuondoshwa moja kwa moja kutoka sehemu nyingi za Waislamu ulimwenguni, kwa amani na bila ya kumwaga damu.

 

 

.../3

 

 

 

Share