006-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Vyakula Vilivyoharamishwa Na Kitabu Cha Allaah: Mfu

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

Alhidaaya.com

 

006-Vyakula Vilivyoharamishwa Na Kitabu Cha Allaah   Mfu (01)

 

 

 

Vyakula Vilivyoharamishwa Na Kitabu Cha Allaah   Mfu (01)

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ وَالْمُنْخَنِقَةُ وَالْمَوْقُوذَةُ وَالْمُتَرَدِّيَةُ وَالنَّطِيحَةُ وَمَا أَكَلَ السَّبُعُ إِلَّا مَا ذَكَّيْتُمْ وَمَا ذُبِحَ عَلَى النُّصُبِ"

 

03: “Mmeharamishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na kilichotajiwa asiyekuwa Allaah katika kuchinjwa kwake, na (pia)  mnyama aliyekufa kwa kukosa hewa au aliyepigwa akafa, au aliyeporomoka toka juu, au aliyepigwa pembe, na aliyeliwa na mnyama mwitu, isipokuwa mliyewahi kumchinja kihalali (kabla ya kufa), na waliochinjwa kwa ajili ya ‘ibaadah ya waabudiwa”. [Al-Maaidah: 03].

 

Aayah hii imetaja kwa mpangilio baadhi ya vilivyoharamishwa ambavyo ni:

 

Cha Kwanza:

 

Mnyama mfu. Naye ni kila mnyama aliyejifia mwenyewe tu bila kuuliwa au kwa chinjo la kisharia.  Nao ni:

 

(a) "الْمُنْخَنِقَةُ". : Ni mnyama aliyenyongwa au kufungiwa sehemu isiyo na hewa akafa.

 

(b) "الْمَوْقُوْذَةُ" : Ni mnyama aliyepigwa kwa fimbo au mfano wake akafa.

 

(c)  "الْمُتَرَدِّيَةُ" : Ni mnyama aliyeanguka toka sehemu ya juu akafa.

 

(d) "النَّطِيْحَةُ" : Ni mnyama aliyepigwa pembe na mwenzake akafa kutokana na pigo hilo.

 

(e) " مَا أَكَلَ السَّبُعُ" : Ni mnyama aliyekufa kwa kujeruhiwa na mnyama mkali na akamla sehemu.

 

 

Mnyama yeyote kati ya hawa akiwahiwa kabla hajafa akachinjwa, basi anakuwa ni halali.  Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

"إِلَّا مَا ذَكَّيْتُمْ"

 

“Isipokuwa mliyewahi kumchinja kihalali (kabla ya kufa)”.  [Al-Maaidah: 03].

 

 

·        Sehemu Ya Mnyama Iliyokatwa Akiwa Hai Inaingia Kwenye Duara La Mfu.

 

Ni kwa neno la Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"مَا قُطِعَ مِنَ الْبَهِيْمَةِ وَهِيَ حَيَّةٌ فَهُوَ مَيْتَةٌ" 

 

“Kipande (cha nyama) kilichokatwa cha mnyama aliye hai, basi hicho ni mfu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2841) na Ibn Maajah (3216)].

 

Na kwa msingi huu, haifai kula kipande cha kiungo cha mnyama aliye hai.

 

·        Mfu Anayetoka Nje Ya Duara La Uharamu

 

Kila mtu anajua kwamba ni haramu kula mfu kwa aina zake zote.  Lakini Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) imewatoa wafu wawili toka kwenye wigo wa uharamu na kuwaingiza ndani ya duara la uhalali wa kuliwa.  Wafu hao ni samaki na nzige.  Na hii ni kutokana na Hadiyth iliyopokelewa na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) toka kwa Rasuli aliyesema:

 

"أُحِلَّتْ لَنَا مَيْتَتَانِ وَدَمَانِ: أَمَّا الْمَيْتَتَانِ: فالْحُوْتُ وَالْجَرَادُ ، وَأَمَّا الدَّمَانِ: فَالْكَبِدُ وَالطِّحَالُ"

 

“Tumehalalishiwa maiti mbili na damu mbili. Ama maiti mbili, ni samaki na nzige.  Ama damu mbili, ni ini na wengu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Ibn Maajah (3314), Ahmad (5690) na wengineo.  Angalia As-Swahiyhah (1118). Hadiyth hii ina hukmu ya Raf-‘u].

 

·        Faida Mbili:

 

Faida Ya Kwanza:

 

Hukmu Ya Kula Chenye Kuelea Juu Ya Maji Kama Samaki Au Wanyama Wengineo Wa Baharini.

 

‘Ulamaa wana kauli mbili kuhusu hili:

[Al-Badaai’u (5/35), Al-Muhallaa (7/393), Al-Mughniy (9/35) na Naylul Awtwaar (8/170)].

 

Kauli Ya Kwanza:

 

Ni halali kula.  Ni madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Adh-Dhwaahiriyyah, ‘Atwaa, Mak-huwl, An-Nakh-’iy na Abu Thawr.  Ni kauli iliyosimuliwa toka kwa Abu Bakr na Abu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa).

 

Dalili zao ni:

 

1-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَمَا يَسْتَوِي الْبَحْرَانِ هَـٰذَا عَذْبٌ فُرَاتٌ سَائِغٌ شَرَابُهُ وَهَـٰذَا مِلْحٌ أُجَاجٌ ۖ وَمِنْ كُلٍّ تَأْكُلُونَ لَحْمًا طَرِيًّا"

 

“Na bahari mbili hazilingani sawa; haya ni (maji) matamu ladha yake, yenye kukata kiu, anisi kinywaji chake, na haya ni ya chumvi kali. Na katika kila moja mnakula nyama laini safi”.  [Faatwir: 12].

 

2-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

"أُحِلَّ لَكُمْ صَيْدُ الْبَحْرِ وَطَعَامُهُ مَتَاعًا لَّكُمْ وَلِلسَّيَّارَةِ"

 

“Mmehalalishiwa mawindo ya bahari,  na chakula chake ni manufaa kwenu na kwa wasafiri”.  [Al-Maaidah: 96].

 

Ibn ‘Abbaas na wengineo wamesema:  “Mawindo yake ni kile mlichokivua, na chakula chake ni kile kilichotupwa nje (ya maji)”.

 

Aayah hizi mbili kwa ujumla wake zinaashiria uhalali wa mawindo yote ya baharini na vinavyovuliwa toka humo, na Allaah Ta’aalaa Hakukihusisha au kuainisha chochote katika hivi kuwa hiki ni halali na kingine si halali.

 

"وَمَا كَانَ رَبُّكَ نَسِيًّا"

 

“Na Rabb wako Si Mwenye Kusahau kamwe”.  [Maryam: 64].

 

 

3-  Ni kutokana na ujumuishi wa kauli yake Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipoulizwa kuhusu maji ya bahari pale alipojibu akisema:

 

"هُوَ الطَّهُورُ مَاؤُهُ الْحَلاَلُ مَيْتَتُهُ"

 

“Bahari maji yake ni twahara, na maiti yake ni halali”.   [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (83), At-Tirmidhiy (69) na An-Nasaaiy (1/176)].

 

Hii inajumuisha vyote vilivyofia baharini kwa aina zake zote.

 

 

4-  Kuhusiana na vilivyotolewa nje ya duara la mfu, Ibn ‘Umar (akitumia Hadiyth ya Rasuli) anasema:

 

" أُحِلَّتْ لَنَا مَيْتَتَانِ  …الْحُوْتُ وَالْجَرَادُ "

 

“Tumehalalishiwa mfu mbili … samaki na nzige.”  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma kidogo].

 

5-  (Kauli ya Ibn ‘Umar) inatiliwa nguvu na Hadiyth ya Jaabir aliyesema:

 

"أنً الْبَحْرَ قَذَفَ إِلَى السًاحِلِ بِدَابًةٍ ضَخْمَةٍ تُدْعَى العَنْبَرُ ، فَأكَلُوْا مِنْهَا ، وَلَمًا قَدِمُوْا إلَى المدِيْنَةِ سَألُوْا رَسُوْلَ اللهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْهَا ، فَقَالَ: "هُوَ رِزْقٌ أَخْرَجَهُ اللهُ لَكُمْ ، فَهَلْ مَعَكُمْ مِنْ لَحْمِهِ شَيْئًا فَتُطْعِمُوْنَا؟" قَالَ جَابِرٌ: فَأَرْسَلْنَا إِلَى رَسُوْلِ اللهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ مِنْهُ فَأَكَلَهُ".

 

“Kwamba bahari ilitema ufukweni samaki mkubwa sana aitwaye anbar, na watu wakamla sehemu.  Walipofika Madiynah, walimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kumla kwao samaki huyo, na Rasuli akawaambia:  “Huyo ni rizki ambayo Allaah Amewatoleeni.  Je, mna nyama yake kidogo mkatupa na sisi tukala?”  Jaabir anasema:  Tukampelekea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sehemu ya nyama hiyo naye akaila”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4362), Muslim (1935) na Ibn Maajah].

 

Kauli Ya Pili:

 

Si halali kumla samaki au mnyama wa baharini anayeelea.  Ni kauli ya Abu Haniyfah na maswahibu zake.  Dalili zao ni:

 

1-  Hadiyth Marfuw’u iliyosimuliwa na Jaabir isemayo:

 

"مَا أَلْقَاهُ الْبَحْرُ أَوْ جَزَرَ عَنْهُ فَكُلُوْهُ ، وَمَا مَاتَ فِيْهِ فَطَافَ فَلَا تَأْكُلُوْهُ"

 

“Kilichotemwa na bahari, au ilichokiacha baada ya kupwa, basi kileni, na kilichofia humo kikaelea, basi msikile”.  [Hadiyth Dhwa’iyf.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3815) na Ibn Maajah].

 

Dalili hii imejibiwa kwa jibu lisemalo kuwa Hadiyth hii ni Dhwa’iyf kwa makubaliano ya wabobezi wa Hadiyth.

 

2-  Baadhi ya aathaar toka kwa Jaabir, ‘Aliy, na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhum) zinazokataza kula chenye kuelea, na zote ni dhwa’iyf.  [Angalia Al-Muhallaa cha Ibn Hazm (7/394)].

 

Kauli Yenye Nguvu:

 

Hakuna shaka yoyote kwamba dalili za Jumhuwr ndizo zenye nguvu zaidi. Lakini, ikiwa itathibiti kitiba kwamba samaki anayeelea anakuwa ameharibika na anaweza kuleta madhara kwa mwili na hususan ikiwa umepita muda baada ya kufa, basi hapo, kutomla kutaendana vizuri zaidi na qawaaid za sharia zilizoharamisha vibaya vyenye madhara.   Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Faida Ya Pili:

 

‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu kula nzige

[Al-Majmuw’u (9/24), Al-Mughniy (9/315), na Subulus Salaam (4/1390)].

 

Jamaahiyr ya ‘Ulamaa kati ya watangu wema na waliowafuatia –kinyume na Maalik- wanasema nzige ni halali, ni sawa akiwa amekufa kwa kuwindwa au kwa kujifia tu mwenyewe.  Na hii ni kwa dalili zifuatazo:

 

1-  Ni kauli iliyotangulia ya Ibn ‘Umar:

 

" أُحِلَّتْ لَنَا مَيْتَتَانِ  …الْحُوتُ وَالْجَرَادُ "

 

“Tumehalalishiwa nyamafu mbili … samaki na nzige.”

 

 

2-  Ni Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Abiy Awfaa:

 

"غَزَوْنَا مَعَ رَسُوْلِ اللهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلًمَ سَبْعَ غَزَوَاتٍ نَأْكُلُ الْجَرَادَ"

 

“Tulipigana vita saba tukiwa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku tunakula nzige”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5495) na Muslim (1952)].

 

Maalik (Rahimahul Laah) ameshurutisha kwamba ili nzige awezekanike kuliwa ni kuwa afe kutokana na sababu, nayo ni ima akatwe sehemu ya mwili wake, au achemshwe, au akaangwe akiwa hai au achomwe.  Ama akijifia hivi tu mwenyewe, basi hafai kuliwa!!

 

Kauli ya kwanza ndio yenye nguvu zaidi.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

 

Share