008-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Nyama Ya Nguruwe

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

Alhidaaya.com

 

008- Vyakula Vilivyoharamishwa Na Kitabu Cha Allaah (08): Nyama Ya Nguruwe (03) 

 

 

 

3-  Nyama Ya Nguruwe 

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنزِيرِ"

 

“Mmeharamishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe”.  [Al-Maaidah: 03].

 

Na Amesema tena ‘Azza wa Jalla:

 

"قُل لَّا أَجِدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلَّا أَنْ يَكُوْنَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوْحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ"

“Sema:  Sipati katika yale niliyofunuliwa Wahyi kwangu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni chafu yenye madhara”.  [Al-An’aam: 145].

 

Hakuna makhitilifiano yoyote kati ya ‘Ulamaa kuhusiana na kuharamishwa nguruwe kuanzia nyama yake, shahamu (mafuta) yake na sehemu zake zote.  Nyama yake imetajwa mahususi katika Aayah kwa kuwa ndio sehemu kubwa inayoliwa ya mnyama, ama sehemu nyinginezo, hizo ni kama vifuatilizi tu. Kadhalika, imetajwa mahususi ili kuweka wazi ubaya na uharamu wa nyama hii ambayo baadhi ya watu wanaiona kuwa ni nzuri na bora zaidi kuliko nyama nyinginezo zote bila kujali uzito wa katazo la Allaah.

 

Na kiwakilishi nomino katika Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"أَوْ لَحْمَ خِنزِيْرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ"

 

“au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni chafu yenye madhara”, kwa mujibu wa Lugha ya Kiarabu ambayo Qur-aan imeshuka kwayo, kinarejelea kitajwa kilicho karibu zaidi nacho, naye ni nguruwe mwenyewe.  Na kwa matamshi haya bayana  ya Qur-aan hii, nguruwe kwa kiini chake ni mchafu asiyefaa kuliwa, na yeye wote mzima ni najisi, na najisi ni haramu ambayo ni lazima kuiepuka. Hivyo basi, nguruwe kwa ujumla wake wote ni haramu, haitolewi hata nywele yake au kingine chake chochote kikawa ni halali.

 

 

·        Faida:

 

Mwandishi wa Tafsiyrul Manaar (2/98) amesema katika kubainisha hikma ya sharia katika kuharamisha nguruwe:

 

“Allaah Ameharamisha nyama ya nguruwe kwa kuwa ni chafu isiyo salama, na hii ni kwa vile chakula anachokipenda zaidi nguruwe ni taka, vinyesi na najisi. Nyama hii ina madhara kwenye nchi zote kama ilivyothibiti kwa njia ya majaribio.  Kula nyama yake ni katika sababu za kupatwa na minyoo hatari inayoua.  Na inasemekana pia kuwa nyama yake ina athari hasi na mbaya kwa tabia takasifu na wivu wa mtu kwa mkewe na banati zake”.

 

Share