018-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Adabu Za Kula: Kupiga “Bismil Laahi” Kabla Ya Kula

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

Alhidaaya.com

 

 

018-Adabu Za Kula: Kupiga “Bismil Laahi” Kabla Ya Kula  

 

 

 

 

Adabu Za Kula

 

Huu ni mjumuiko wa adabu za kisharia katika kula ambazo inatakikana tuzizingatie, kwani ndani yake kuna uhuisho wa Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Kadhalika, ndani yake kuna kumfukuza, kumweka mbali na kumzuia shaytwaan ambaye anakuwa na shime ya kushirikiana na Muislamu katika chakula chake, kinywaji chake, mavazi yake na malazi yake ili aweze kumpoteza na kuutawala moyo wake, akili yake na viungo vyake.  Vilevile, ndani yake kuna ufanikishaji wa maslaha ya kidini, kiuchumi na kijamii.

 

Kati ya adabu hizi ni:

 

1-  Kupiga “Bismil Laahi” Kabla Ya Kula:

 

Toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) amesema:  “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِذَا أَكَلَ أَحَدُكُمْ طَعَاماً فَلْيَقُلْ بِسْمِ اللَّهِ، فَإِنْ نَسِيَ فِي أَوَّلِهِ فَلْيَقُلْ بسْمِ اللَّهِ فِي أَوَّلِهِ وَآخِرِهِ"

 

“Anapokula mmoja wenu chakula chochote, basi aseme Bismil Laah.  Akisahau mwanzoni (kisha akakumbuka) basi aseme:  Bismil Laahi, katika mwanzo wake na mwisho wake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3767), At Tirmidhiy (1858) na Ahmad (6/143)].

 

Na toka kwa Hudhayfah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِنَّ الشَّيْطَانَ يَسْتَحِلُّ الطَّعَامَ أَنْ لَا يُذْكَرَ اسْمُ اللهِ عَلَيْهِ"

 

“Hakika shaytwaan kinakuwa halali kwake chakula ambacho hakikutajiwa Jina la Allaah.” [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2017) na Ahmad (5/383)].

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia pia ‘Amri bin Abiy Salamah:

 

"يَا غُلَامُ ! سَمِّ اَللَّهَ ، وَكُلْ بِيَمِيْنِكَ ، وَكُلْ مِمَّا يَلِيْكَ"

 

“Ee kijana mdogo!  Mtaje Allaah, kula na mkono wako wa kulia, na kula kilicho mbele yako”.  [Hadiyth Swahiyh].

 

Na ikiwa atasahau kusema “Bismil Laah” wakati anapoanza kula:

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) –akilizungumzia hili-amesema:

 

"مَنْ نَسِيَ أَنْ يَذْكُرَ اللَّهَ  عَزَّ وَجَلَّ فِي أَوَّلِ طَعَامِهِ فَلْيَقُلْ حِيْنَ يَذْكُرُ : بِسْمِ اللَّهِ أَوَّلَهُ وَآخِرَهُ، فَإِنَّهُ يَسْتَقْبِلُ طَعَامًا جَدِيْدًا، أَوْ يَمْتَنِعُ الخَبِيْثُ مِمَّا كَانَ يُصِيْبُ مِنْهُ".

 

“Anayesahau kulitaja Jina la Allaah ‘Azza wa Jalla mwanzoni anapokula, basi aseme anapokumbuka:  “Bismil Laah, mwanzo wake na mwisho wake”, kwani (kwa kusema hivyo) atakianza upya chakula chake, au khabithi (shaytwaan) ataiachia sehemu ya chakula aliyokuwa anaipata”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Ibn As-Sunniy katika kitabu chake “Amalul Yawm wal Laylah (461) kwa Sanad Swahiyh.  Ina Hadiyth mwenza toka kwa ‘Aaishah, nayo imetajwa nyuma].

 

Share