04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Udhwhiyah: Kasoro Zinazomfanya Mnyama Asifae Kwa Kudhwahi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

الأُضْحِيَةُ

 

 Udhwhiyah  

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

04-Udhwhiyah: Kasoro Zinazomfanya Mnyama Asifae Kwa Kudhwahi:

 

Kasoro anazokuwa nazo mnyama wa kudhwahi zinagawanyika vigawanyo vitatu:

 

Cha kwanza:  Ni kasoro zinazomfanya mnyama akataliwe na asifae, nazo ni nne.  Kasoro hizi Hadiyth imezielezea kuwa hazimpasishi mnyama kuweza kuchinjwa.  Wanyama hao ni wenye kasoro hizi:

 

 

1-  Mwenye chongo linaloonekana wazi.  Ikiwa weupe utafunika sehemu kubwa ya jicho lake na kubaki sehemu ndogo tu, basi atakuwa hafai.  Na kipofu ndiye hafai kabisa.

 

 

2-   Mgonjwa ambaye ugonjwa wake unaonekana bayana.  Kama ugonjwa wake ni hafifu, basi atafaa.

 

 

3-  Mwenye kuchechemea mchechemeo dhahiri.  Na aliyekatwa au aliyevunjika miguu atakuwa hafai kabisa.

 

 

4-  Aliyedhoofu kutokana na udhaifu wa mifupa yake.

 

Toka kwa Al-Baraa bin ‘Aazib kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

"أَرْبَعَةٌ لاَ يَجْزِينَ فِي الأَضَاحِي : الْعَوْرَاءُ الْبَيِّنُ عَوَرُهَا  ، وَالْمَرِيضَةُ الْبَيِّنُ مَرَضُهَا ، وَالْعَرْجَاءُ الْبَيِّنُ ظَلْعُهَا ، وَالْكَسِيرَةُ الَّتِي لاَ تُنْقِي"

 

“Wanne hawakidhi vigezo vya kuwa wanyama wa kudhwahi.  Mwenye chongo la wazi linaloonekana, mgonjwa anayeonekana wazi kuwa mgonjwa,  anayechechemea ambaye mbavu zake zimetokeza, na mdhoofu anayejikokota”. [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na An-Nasaaiy (7/215), Ibn Maajah (3144) na Ahmad (4/284)].   

 

Kwa kasoro hizi, mnyama anakuwa hafai na hana sifa za kudhwahi kwa makubaliano ya ‘Ulamaa.  [At-Tamhiyd (20/167), Al-Mughniy (9/349), na Al-Majmuw’u (8/404)].

 

Cha pili:  Ni kasoro ambazo hazipendezi mnyama huyu kuwa nazo, lakini hazizuii kupata sifa ya kufaa.  Kasoro zenyewe ni:

 

 

1-  Kukatwa sikio lote au sehemu ya sikio.

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba mnyama mwenye hali hii hafai kwa kudhwahi.  Lakini kauli yao hiyo ina walakini, kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameainisha kasoro nne tu kwa mnyama akiwa nazo kuwa hafai kwa kudhwahi katika Hadiyth iliyotangulia.  Bali ‘Aliy (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:

 

"أَمَرَنَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ نَسْتَشْرِفَ الْعَيْنَ وَالْأُذُنَ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamuru tukague macho (kama mazima yanaona) na masikio (kama mazima hayajaguswa)”.  [Hadiyth Hasan Bitwuruqih.  Imekharijiwa na An-Nasaaiy (7/217), Ahmad (1/95), At-Tirmidhiy (1498), Abu Daawuwd (284), Ibn Maajah (3142) na wengineo].

 

Hadiyth hii ya ‘Aliy inatufahamisha kwamba mnyama anayeepukwa ni yule aliyetobolewa, au aliyepasuliwa, au aliyekatwa sikio, lakini pamoja na hivyo, haimaanishi kwamba hafai au hatoshelezi vigezo vikuu.  

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana pia kuhusu mnyama ambaye kimaumbile amezaliwa bila masikio mawili.  Abu Haniyfah, Maalik na Ash-Shaafi’iy wanaona kwamba kama hana masikio kabisa, basi huyo atakuwa hafai, lakini kama atakuwa na masikio angalau madogo, basi atafaa.  [Al-Istidhkaar (15/128), Ibn ‘Aabidiyna (9/467), na Al-Majmuw’u (8/401)].

 

 

2-  Kuvunjika pembe kidogo au sehemu yake kubwa.

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema inajuzu kudhwahi mnyama aliyevunjika pembe lakini asiwe anatokwa damu.  Kwa upande wa Maalik, yeye anasema itakuwa ni makruhu tu.   

 

Ninasema:  Limekuja katika baadhi ya riwaayah za Hadiyth iliyotangulia ya ‘Aliy katazo kwa mnyama aliyevunjika pembe.  Lakini riwaayah hizo ni Dhwa’iyf.

 

Cha tatu:  Ni kasoro ambazo hazina athari.  Hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh iliyokataza au kugusia hilo, ingawa kasoro hizi zinapunguza ukamilifu wa vigezo vinavyotakiwa.  Mnyama mwenye kasoro hizi anatosheleza katika kudhwahi na wala hakataliwi, ingawa kuna baadhi ya ‘Ulamaa waliomkataa.  Ni kama asiye na meno kabisa, aliyekatwa mkia au tako, aliyekatwa pua, aliyehasiwa na kadhalika.   

 

                                                           

 

Share