03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Udhwhiyah: Wanyama Wanaochinjwa

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الأُضْحِيَةُ

 

 Udhwhiyah  

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

03-Udhwhiyah: Wanyama Wanaochinjwa:

 

 

1-  Haitoshelezi katika kuchinja isipokuwa wanyama wa miguu minne wa mifugo ambao ni ngamia, ng’ombe, kondoo na mbuzi.  Ni kwa Neno Lake Ta’alaa:

 

"لِّيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ"

 

“Ili walitaje Jina la Allaah kwa yale Aliyowaruzuku ya wanyama wa miguu minne wa mifugo”.  [Al-Hajj : 34].

 

Jopo la ‘Ulamaa limenukuu Ijma’a ya kwamba kudhwahi hakufai isipokuwa kwa wanyama hawa.  Lakini, Ibn Al-Mundhir ameeleza kutoka kwa Hasan bin Swaaleh kwamba inajuzu kudhwahi nyati na mburukenge.  Daawuwd pia kasema hivyo hivyo kuhusu nyati.  Ama Ibn Hazm, yeye amejuzisha wanyama wote wanaoliwa wenye miguu minne au ndege!!  Ametoa hoja kwa kauli ya Bilaal (Radhwiya Allaah ‘anhu) aliyesema:

 

"مَاكُنْتُ أُبَالِي لَوْ ضَحَّيْتُ بِدِيْكٍ.."

 

“Sikuwa nikijali hata nikichinja jogoo…”.  [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Abdur Razzaaq (8156) na Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (7/358)].

 

Ninasema:  “Madhehebu ya Jumhuwr ndiyo yenye kulazimiana na Aayah Tukufu, na pia kwa vile haikupokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alidhwahi mnyama mwingine zaidi ya ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo”.

 

(a,b) -  Ngamia na ng’ombe

 

Imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba zake, walidhwahi wanyama hawa wawili (ngamia na ng’ombe), mbali na kwamba inajuzu watu saba kushirikiana ng’ombe mmoja au ngamia mmoja ambaye atawatosheleza wote.  Na hii ni kwa vielelezo vifuatavyo:

 

 

1-  Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah:   

 

"نحَرْنا مَعَ رَسولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَامَ الْحُدَيْبِيَةِ الْبَدَنَةَ عَنْ سَبْعَةٍ وَالْبَقَرَةَ عَنْ سَبْعَةٍ"

 

“Tulichinja pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwaka wa Al-Hudaybiyah ngamia mmoja kwa watu saba, na ng’ombe mmoja kwa watu saba”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1318), Abu Daawuwd (2809), At-Tirmidhiy (903), na Ibn Maajah (3132)].

 

2-  Pia Jaabir kasema:

 

"كُنَّا نَتَمَتَّعُ مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِالْعُمْرَةِ فَنَذْبَحُ الْبَقَرَةَ عَنْ سَبْعَةٍ نَشْتَرِكُ فِيهَا"

 

“Tulifanya Hajji Tamattu (‘Umrah kabla ya Hijja) pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tukashirikiana watu saba kuchinja ng’ombe mmoja”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1318), Abu Daawuwd (2807) na An-Nasaaiy (7/222)].

 

Faida mbalimbali:

 

Ya kwanza:  Is-haaq, Ibn Khuzaymah na wengineo wana mwelekeo usemao kuwa ngamia mmoja anatosheleza watu kumi.  Na hii ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema:

 

"كُنَّا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي سَفَرٍ فَحَضَرَ الْأَضْحَى فَاشْتَرَكْنَا فِي الْبَقَرَةِ سَبْعَةٌ وَفِي الْبَعِيرِ عَشَرَةٌ"

 

“Tulikuwa safarini pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Adhwhaa ikatukutia huko.  Tukashirikiana watu saba ng’ombe mmoja, na watu kumi ngamia mmoja”.  [Isnaad yake ni Hasan.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1501), An-Nasaaiy (7/222) na Ibn Maajah (3131)].

 

Ash-Shawkaan akioanisha kati ya dalili amesema:  “Ngamia anawatosha watu kumi kama ni wa udhwhiyah, na watu saba kama ni wa amali za Hijja”.

  

Ya pili:  Imamu Maalik (Rahimahul Laah) -kinyume na Jumhuwr-  ameshurutisha  kwa wenye kushirikiana ng’ombe mmoja au ngamia mmoja wawe ni watu wa nyumba moja!!

 

Kauli hii inabidi iangaliwe, kwa kuwa Hadiyth ya Jaabir iliyotangulia ambayo inasema:  “Tulichinja pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwaka wa Al-Hudaybiyah ngamia mmoja kwa watu saba, na ng’ombe mmoja kwa watu saba”, inaonyesha kuwa Maswahaba walikuwa ni watu tofauti tofauti toka makabila mbalimbali.  Na hata makabila yao yangelikuwa ni mamoja, basi wangetofautiana nyumba, na lau zingekuwa nyumba zao ni moja, basi ingelikuwa vile vile ni vigumu kila nyumba kukamilisha idadi ya watu saba, ima wangezidi, au wangepungua.  [Al-Haawiy cha Al-Mawruwdiy (19/145-146) na Fiqhul Udhwhiyah (uk. 89-90)].

 

Ya tatu:  Jumhuwr -kinyume na Abu Haniyfah- wamejuzisha kutofautiana nia kwa watu saba wenye kushirikiana kwenye mnyama mmoja.  Wamesema kuwa inajuzu baadhi yao washiriki kwa niya ya udhwhiyah, na wengine kwa niya ya kupata nyama tu.  Kwa sababu fungu la kila mmoja wao linazingatiwa kwa mujibu wa niya yake na si kwa mujibu wa niya ya mwenzake.  Kwa kuwa, lau kama dhabihu zao zitatofautiana, baadhi yao wakafanya fungu lao kwa ajili ya qiraan, na wengine kwa tamattu, na wengine kwa kunyoa, na waliobaki kwa kivazi, basi itajuzu.  Kadhalika, hata kama mwingine fungu lake likawa kwa ajili ya nyama tu, kwa kuwa niya ya asiyejikurubisha haiathiri niya ya mwenye kujikurubisha.  

 

Ya nne:  Umri ufaao kwa ngamia na ng’ombe

 

Jaabir amesema:  “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam amesema: 

 

"لاَ تَذْبَحُوا إِلاَّ مُسِنَّةً إِلاَّ أَنْ يَعْسُرَ عَلَيْكُمْ فَتَذْبَحُوا جَذَعَةً مِنَ الضَّأْنِ‏"‏ 

 

“Msichinje isipokuwa “musinnah”, ila kama itakuwa vigumu kwenu kumpata, basi chinjeni “jadha’ah” wa mbuzi au kondoo”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1963), Abu Daawuwd (2797), An-Nasaaiy (7/218) na Ibn Maajah (3141)]. 

 

“Musinnah” ni mnyama aliyekomaa vizuri.  Kwa ngamia ni yule aliyetimiza miaka mitano na kuingia wa sita, na kwa ng’ombe ni yule aliyetimiza miaka miwili na kuingia wa tatu.  Haitojuzu kuchinja walio chini ya miaka hiyo kwa wote wawili.  Ama “jadha’ah” kwa mbuzi na kondoo, ni yule aliyefikisha miezi sita kwenda juu.  Haijuzu wa chini ya miezi sita.

 

(c)  Kondoo

 

Toka kwa Anas, kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"ضَحَّى بِكَبْشَيْنِ أَمْلَحَيْنِ .... "

 

“Alichinja kondoo wawili dume wenye rangi mseto ya weupe na weusi….”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma kidogo].

 

Kondoo mmoja anamtosheleza mtu; yeye pamoja na watu wa nyumba yake.  ‘Aaishah amesema:  

 

"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمَرَ بِكَبْشٍ أَقْرَنَ يَطَأُ فِي سَوَادٍ وَيَبْرَكُ فِي سَوَادٍ وَيَنْظُرُ فِي سَوَادٍ فَأُتِيَ بِهِ لِيُضَحِّيَ بِهِ فَقَالَ لَهَا : يَا عَائِشَةُ هَلُمِّي الْمُدْيَةَ ، ثُمَّ قَالَ : اشْحَذِيهَا بِحَجَرٍ ، فَفَعَلَتْ ثُمَّ أَخَذَهَا وَأَخَذَ الْكَبْشَ فَأَضْجَعَهُ ، ثُمَّ ذَبَحَهُ ، ثُمَّ قَالَ : بِسْمِ اللَّهِ ، اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنْ مُحَمَّدٍ وَآلِ مُحَمَّدٍ وَمِنْ أُمَّةِ مُحَمَّدٍ ،  ثُمَّ ضَحَّى بِهِ."

 

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliagiza beberu la kondoo mwenye pembe, mwenye miguu myeusi, mwenye tumbo jeusi, na mwenye macho meusi.  Akaletewa ili amchinje (kwa udhwhiya). Akamwambia:  Ee ‘Aaishah!  Niletee kisu.  Kisha akamwambia:  Kinoe kwa jiwe. ‘Aaishah akakinoa, Rasuli akakichukua, akamkamata beberu, akamlaza ubavu, kisha akamchinja huku akisema:  Bismil Laah.  Ee Allaah!  Mtakabalie Muhammad, na familia ya Muhammad, na ummah wa Muhammad”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1967)].

 

Na Abu ‘Atwaa bin Yasaar amesema:

 

"سَأَلْتُ أَبَا أَيُّوبَ الأَنْصَارِيَّ كَيْفَ كَانَتِ الضَّحَايَا فِيكُمْ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ـ قَالَ كَانَ الرَّجُلُ فِي عَهْدِ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يُضَحِّي بِالشَّاةِ عَنْهُ وَعَنْ أَهْلِ بَيْتِهِ فَيَأْكُلُونَ وَيُطْعِمُونَ ، ثُمَّ تَبَاهَى النَّاسُ فَصَارَ كَمَا تَرَى"

 

“Nilimuuliza Abu Ayyuuwb Al-Answaariy:  Ni mazingira yapi mliyokuwa nayo kwa upande wa kudhwahi wanyama wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?  Akasema:  Mtu katika enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikuwa anachinja kondoo kwa niaba yake na kwa niaba ya watu wa nyumba yake, kisha wanakula na kugawa kwa wengine, mpaka watu wakaanza kushindana, na hali ikawa kama unavyoiona”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1505), Ibn Maajah (3147), na Al-Bayhaqiy (9/268)].

 

"وَ عَنْ عَبْدِ اللهِ بِنْ هِشَامِ كَانَ قَدْ أَدْرَكَ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَذَهَبَتْ بِهِ أُمُّهُ زَيْنَبُ ابْنَةُ حُمَيْدٍ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَتْ : يَا رَسُولَ اللَّهِ بَايِعْهُ‏.‏ فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم : ‏"‏ هُوَ صَغِيرٌ ‏"‏، فَمَسَحَ رَأْسَهُ وَدَعَا لَهُ، وَكَانَ يُضَحِّي بِالشَّاةِ الْوَاحِدَةِ عَنْ جَمِيعِ أَهْلِهِ"

 

‘Abdullaah bin Hishaam ambaye alimwahi Rasuli akiwa hai amesema kuwa mama yake Zaynab bint Humayd alimchukua kwenda naye kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Alipofika alisema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Peaneni naye fungamano la kuwajibika na Uislamu na kukutii wewe (Bay-‘a).  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Yeye bado hajabaleghe.  Akakipangusa kichwa chake na akamwombea.  Naye (‘Abdullaah bin Hishaam) alikuwa anachinja kondoo mmoja kwa niaba ya watu wake wote”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (7210), Abu Daawuwd (2942) kwa ufupisho, na Ahmad (4/233)].

 

Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad wanaona kwamba kondoo mmoja anamtosheleza mtu pamoja na familia yake yote hata kama ni wengi.  Lakini Abu Haniyfah na Ath-Thawriy wamelikirihisha hilo!!

 

Umri Ufaao Kwa Kondoo:

 

Nyuma kidogo tumeitaja kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:

 

"لاَ تَذْبَحُوا إِلاَّ مُسِنَّةً إِلاَّ أَنْ يَعْسُرَ عَلَيْكُمْ فَتَذْبَحُوا جَذَعَةً مِنَ الضَّأْنِ‏"‏ 

 

“Msichinje isipokuwa “musinnah”, ila kama itakuwa vigumu kwenu kumpata, basi chinjeni “jadha’ah” wa mbuzi au kondoo”. 

 

Kauli hii inaonyesha kwamba haijuzu katika udhwhiyah aliye chini ya “musinnah”, na “musinnah” kwa kondoo ni yule aliyefikisha mwaka na anaingia mwaka wa pili.  Lakini kama itakuwa vigumu kumpata, basi atatosha “jadha’ah, na huyu ni mwenye kuanzia miezi sita kwenda juu.  Na huu ndio msimamo wa ‘Ulamaa.  Lakini pamoja na msimamo wao huu, wamejuzisha kuchinja kondoo “jadha’ah kwa hali yoyote hata kama “musinnah” atapatikana, kwa kuwa wameichukulia Hadiyth hii kuwa inastahabisha jambo hilo huku wakitolea dalili kwa jumla ya Hadiyth zinazoashiria kujuzu kuchinja kondoo wa kuanzia miezi sita katika hali yoyote ile, lakini Asaaniyd za Hadiyth hizo zote ni Dhwa’iyf.

 

Lenye nguvu na kutegemewa zaidi ni kuwa kondoo “jadha’ah” hatoshelezi isipokuwa tu kama “musinnah” hatopatikana kutokana na udhahiri wa Hadiyth hii, na udhaifu wa wenye kuikhalifu.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.  [Al-Mabsuwtw (12/9), Al-Mudawwanah (2/2), Al-Haawiy (19/89) na Al-Mughniy (9/348)].

 

(d)  Mbuzi

 

Mbuzi anayetosheleza ni yule mwenye mwaka mmoja kwenda juu kutokana na Hadiyth iliyotangulia.  Ama “jadha’ah” wa mbuzi (mwenye umri wa chini ya mwaka mmoja), huyo hatoshelezi katika udhwhiyah kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote.  [Limenukuliwa hili na At-Tirmidhiy katika As-Sunan (4/194), na Ibn ‘Abdul Barri katika At-Tamhiyd (23/185).  Lakini ‘Atwaa na Al-Awzaa’iy wamelikhalifu hilo].

 

Al-Baraa bin ‘Aazib amesema: 

 

"ضَحَّى خَالٌ لِي يُقَالُ لَهُ أَبُو بُرْدَةَ قَبْلَ الصَّلاَةِ فَقَالَ لَهُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ‏"‏شَاتُكَ شَاةُ لَحْمٍ ‏"‏ ‏.‏ فَقَالَ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّ عِنْدِي دَاجِنًا جَذَعَةً مِنَ الْمَعْزِ ، فَقَالَ ‏: "‏اذْبَحْهَا وَلاَ تَصْلُحُ لِغَيْرِكَ"

 

“Mjomba wangu aitwaye Abu Burdah alichinja kabla ya Swalaah.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Kondoo wako ni wa nyama tu.  Akasema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Nina mbuzi wa nyumbani wa chini ya mwaka mmoja .  Akamwambia:  Mchinje, lakini hafai kwa mwingine zaidi yako”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5556) na Muslim (1961)].

 

Naye ‘Uqbah bin ‘Aamir amesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa kondoo wa kudhwahi ili awagawe kwa niaba yake kwa Maswahaba zake.  Akabakia mbuzi mdogo wa chini ya mwaka mmoja, naye akamweleza hilo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Rasuli akamwambia: 

 

"ضَحِّ بِهِ أَنْتَ"

 

“Huyo jichinjie mwenyewe”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5555) na Muslim (1965)].

 

Kauli ya Rasuli:  “Huyo jichinjie mwenyewe”, imechukuliwa na ‘Ulamaa kuwa ni jambo mahsusi kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir tu.  Na kauli yao hii inatiliwa nguvu na   ziada kwenye Hadiyth iliyoko kwa Al-Bayhaqiy isemayo:

 

"وَلاَ رُخْصَةَ فِيْهَا لأَحَدٍ بَعْدَكَ"

 

 “Na hakuna ruksa kwayo kwa mwingine yeyote baada yako”.  [Angalia Fat-hul Baariy (10/17), na Sunan Al-Bayhaqiy (9/70)].

                                                             

 

 

 

 

 

 

 

Share