06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Udhwhiyah: Kukata Kucha Na Kunyoa Nywele Kwa Aliyeazimia Kudhwahi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

الأُضْحِيَةُ

 

 Udhwhiyah  

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

06-Udhwhiyah: Kukata Kucha Na Kunyoa Nywele Kwa Aliyeazimia Kudhwahi

 

Toka kwa Ummu Salamah, kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِذَا دَخَلَتِ الْعَشْرُ وَأَرَادَ أَحَدُكُمْ أَنْ يُضَحِّيَ فَلاَ يَمَسَّ مِنْ شَعَرِهِ وَبَشَرِهِ شَيْئًا ‏"

 

“Linapoingia kumi (la mwanzo la mwezi wa Dhul-Hijja) na mmoja wenu akaazimia kudhwahi, basi asikate chochote katika nywele zake na kucha zake”.  [Imekharijiwa na Muslim (1977) na wengineo.  Imepita nyuma kidogo].

 

‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na yule ambaye kumi la mwanzo la Dhul-Hijja limeshaingia naye anataka kudhwahi.  [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/138), Al-Mughniy (9/346), Ma’aalimu As-Sunan (2/196) na Fiqhul Udhwhiya (uk. 99)].

 

 

Ibn Al-Musayyib, Rabiy’ah, Ahmad, Is-haaq, Daawuwd, na baadhi ya wafuasi wa Ash-Shaafi’iy, hawa wanasema kwamba ni haramu kwa mtu huyo kukata chochote katika nywele zake au kucha zake mpaka pale atakapodhwahi.  Ni kutokana na uwazi wa Hadiyth hii.

 

 

Maalik, Ash-Shaafi’iy na maswahibu zake wanaona kwamba hilo ni makruhu -ukaraha khafifu (tanziyh), na si haramu.  Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa):

 

"كُنْتُ أَفْتِلُ قَلاَئِدَ بُدْنَ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَمَ ، ثُمَّ يُقَلِّدُهُ وَيَبْعَثُ بِهِ ، وَلا يَحْرُمُ عَلَيْهِ شَيْئٌ أَحَلَّهُ اللَّهُ حَتَّى يَنْحَرَ الْهَدْىَ "

 

“Nilikuwa ninasuka vigwe vya ngamia wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha yeye huwavika vigwe hivyo na kumtuma mtu ampelekee (Al-Haram ngamia hao). Na wala hakiharamiki kwake chochote ambacho Allaah Amekihalalisha mpaka mnyama wake anachinjwa”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1698) na Muslim (1321)].

 

Wamesema:  “Wamekubaliana kwa sauti moja kwamba hakatazwi kuvaa nguo za kushonwa na kujitia manukato kama inavyoharamishwa kwa aliyehirimia.  Hivyo, hilo limedulisha kuwa ni jambo linalopendeza na lililonadibiwa, na si jambo la wajibu lililolazimishwa”.

 

Lakini Abu Haniyfah amesema kuwa kufanya hivyo si jambo la karaha.

 

Ninasema: “Jambo hili linazungukia baina ya uharamu na umakuruhu.  Ni kwamba, kunyoa au kupunguza nywele, au jambo lolote ambalo linafanyika kwa nadra sana, jambo hili halikusudiwi katika Hadiyth ya ‘Aaishah, bali yeye amekusudia yale yote anayoyafanya nyakati zote kama kuvaa, kujitia manukato na mfano wake (yaani haya ndiyo ambayo Rasuli hajajiharamishia)”.

 

Faida Mbili:  [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/138]

 

Ya kwanza:  Makusudio ya katazo la kukata kucha kunajumuisha kuziondosha kwa kuzikata, kuzivunja na mfano wake.  Ama nywele, inajumuisha kuzinyoa kipara, kuzipunguza, kuzinyofoa na mfano wake, ni sawa ikiwa za kwapa, za sharubu, za kinena, za kichwa au sehemu nyingine yoyote ya mwili.

 

Ya pili:  Hikma ya katazo hilo, ni kubaki aliyeazimia kuchinja na viungo vyake kamili ili aachwe huru navyo na moto.  Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kuwa hikma ya hilo ni kujifananisha na aliyehirimia.  Lakini kauli hii ina angalizo, kwa kuwa waazimiaji hao hawaepuki wanawake, wameruhusiwa kujitia manukato na kuvaa nguo, na mengineyo ambayo ni marufuku kwa aliyehirimia.

 

 

 

Share