07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Udhwhiyah: Wakati Wa Kudhwahi

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

الأُضْحِيَةُ

 

 Udhwhiyah  

 

 

Alhidaaya.com

 

 

08-Udhwhiyah: Wakati Wa Kudhwahi:

 

‘Ulamaa wamekubaliana kwa sauti moja kwamba haijuzu kuchinja mnyama wa udhwhiyah kabla ya kuchomoza alfajiri ya Yawm An Nahr (tarehe 10 Dhul Hijja), lakini wamekhitalifiana kuhusiana na yanayofuatia baada ya hapo.  [Al-Ijmaa cha Ibn Al-Mundhir (64), At-Tamhiyd (23/162), Sharhu Muslim (13/110) na Al-Muhallaa (7/374)].

 

 

1-   Ash-Shaafi’iy, Daawuwd, Ibn Al-Mundir na wengineo wamesema kwamba wakati wake unaingia jua linapochomoza na ukapita muda wa kiasi cha kuswali Swalaatul ‘Iyd na khutba mbili.  Kama atachinja baada ya wakati huu, basi itamtosheleza, ni sawa ikiwa imamu ameswali au bado, au mchinjaji ameswali au hakuswali, ni sawa akiwa ni mtu wa mjini, au kijijini, au majangwani.

 

 

2-  ‘Atwaa na Abu Haniyfah wamesema kwamba wakati wake kwa upande wa watu wa vijijini na majangwani, unaingia inapochomoza alfajiri ya pili.  Ama kwa upande wa watu wa mjini, wakati hauingii mpaka imamu aswali na watu na akhutubu.  Ikiwa atachinja kabla ya hapo, basi haitofaa.

 

 

3-  Maalik amesema kwamba haijuzu kuchinja ila baada ya imamu kuswali, kukhutubu na kuchinja.

 

 

4-  Ahmad amesema kwamba haijuzu kabla ya Swalaah, na inajuzu baada yake, kabla imamu hajachinja.

 

Ninasema:  “Toka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  

 

"مَنْ ذَبَحَ قَبْلَ الصَّلَاةِ فَإِنَّمَا يَذْبَحُ لِنَفْسِهِ وَمَنْ ذَبَحَ بَعْدَ الصَّلَاةِ فَقَدْ تَمَّ نُسُكُهُ وَأَصَابَ سُنَّةَ الْمُسْلِمِيْن"

 

“Mwenye kuchinja kabla ya Swalaah, hakika huyo anachinja kwa ajili ya nafsi yake, na mwenye kuchinja baada ya Swalaah, basi amali yake ya kuchinja imetimia na ameipata sunnah ya Waislamu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5546) na Muslim (1962)].

 

Al-Baraa bin ‘Aazib:  Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikhutubu na kusema: 

 

 "إِنَّ أَوَّلَ مَا نَبْدَأُ بِهِ فِي يَوْمِنَا هَذَا نُصَلِّي ثُمَّ نَرْجِعُ فَنَنْحَرُ فَمَنْ فَعَلَ ذَلِكَ فَقَدْ أَصَابَ سُنَّتَنَا وَمَنْ ذَبَحَ فَإِنَّمَا هُوَ لَحْمٌ قَدَّمَهُ لأَهْلِهِ لَيْسَ مِنَ النُّسُكِ فِي شَىْءٍ ‏، فَقَالَ أَبُوْ بُرْدَةٌ : يَا رَسُوْلَ اللهِ، ذَبَحْتُ قَبْلَ أَنْ أُصَلِّيَ ، وَعِنْدِيْ جَذَعَةٌ خَيْرٌ مِنْ مُسِنَّةٍ ، فَقَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : اجْعَلْهَا مَكَانَهَا ، وَلَنْ تُجْزِئَ عَنْ أَحَدٍ بَعْدَكَ"

 

“Jambo la kwanza tunaloanza nalo katika siku yetu hii (‘Iyd Al-Adhwhaa) ni kuswali, halafu tunarudi (majumbani) tunachinja.  Basi mwenye kufanya hivyo, huyo anakuwa ameipata sunnah yetu.  Na mwenye kuchinja (kabla ya Swalaah), hakika hiyo inakuwa ni nyama anayowapa watu wake, haihusiki na chochote na amali ya kudhwahi”.  Abu Burdah akasema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Mimi  nimechinja kabla sijaswali.  Nami nina jadh-‘a ambaye kwangu ni mbora zaidi kuliko musinnah.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Mfidie huyo huyo mahala pa uliyemchinja, na hatofaa kwa yeyote baada yako”.    [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5560).  Imetajwa nyuma]. 

 

Hadiyth hizi mbili zinafahamisha kwa uwazi kabisa kwamba wakati wa kudhwahi unaingia baada ya watu kuswali -kwa wale ambao kwao Swalaah ya ‘Iyd huswaliwa- na hakuna ulazima au sharti ya kusubiri mpaka Imamu achinje kwanza, kwa kuwa kama Imamu hakuchinja, basi hilo haliondoshi kwa watu sunnah ya kudhwahi.  Na hata kama Imamu huyo atachinja kabla ya Swalaah, basi kudhwahi kwake hakutoshelezi.  Hivyo basi, yeye na watu wote wako sawa katika wakati wa kuchinja (yaani baada ya Swalaah).  [Al Fat-h (10/24), na Al-Ummu (2/332)].  

 

Ama Hadiyth ya Jaabir: 

 

"صَلَّى بِنَا النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ النَّحْرِ بِالْمَدِينَةِ فَتَقَدَّمَ رِجَالٌ فَنَحَرُوا ، وَظَنُّوا أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَدْ نَحَرَ ، فَأَمَرَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَنْ كَانَ نَحَرَ قَبْلَهُ أَنْ يُعِيدَ بِنَحْرٍ آخَرَ ، وَلاَ يَنْحَرُوا حَتَّى يَنْحَرَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ"

 

“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituswalisha Yawm An-Nahr (‘Iyd Al-Adhwhaa) mjini Madiynah, na baadhi ya watu wakatangulia kuchinja.  Walidhani kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameshachinja.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru kila aliyechinja kabla yake achinje tena mnyama mwingine, na wasije kuchinja tena mpaka Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) achinje kwanza.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1963), Ahmad (3/204) na Al-Muhallaa (7/374)].

 

Hadiyth hii Jumhuwr wameiawilisha wakisema kuwa muradi wake ni kuwa Rasuli aliwakataza kuharakia kunakoweza kupelekea mtu kudhwahi kabla ya wakati wake.  Na kwa ajili hiyo, Hadiyth nyingine zote zimekuja zikifungamanisha Swalaah, na kwamba mwenye kuchinja baada yake, basi huyo amesibu sunnah, na atakayechinja kabla, basi hajasibu chochote katika amali ya kudhwahi.

 

Mwisho Wa Wakati Wa Kudhwahi

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na wakati wa mwisho wa kudhwahi kama ilivyotangulia katika Kitabu cha Hajji katika Masiku ya Kuchinja.  Na kwa mujibu wa makhitilafiano hayo, lililokubalika ni kuwa wakati wa kudhwahi unaendelea hadi mwisho wa Masiku ya Tashriyq (tarehe 13 ya Dhul Hijjah).  Lakini kiakiba zaidi ni kudhwahi Yawm An Nahr (tarehe 10) kutokana na Ijmaa kuwa inatosheleza katika Siku hiyo.  Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

                                               

                                                           

 

 

 

Share