09-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Udhwhiyah: Yanayopatiwa Manufaa Kutokana Na Mnyama

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

الأُضْحِيَةُ

 

 Udhwhiyah  

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

09-Udhwhiyah: Yanayopatiwa Manufaa Kutokana Na Mnyama

 

 

1-  Kula sehemu ya nyama yake  2-  Kutoa swadaqah kwa masikini  3-  Kuiweka akiba.

 

Allaah Ta’aalaa Amesema: 

 

لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ ﴿٢٨﴾

 

28. Ili wahudhurie kupata manufaa yao, na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kupitia yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo.  Basi kuleni sehemu yake, na lisheni mwenye shida fakiri.  [Al-Hajj: 28].

 

Salamah bin Al-Akwaa:  Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  

 

"مَنْ ضَحَّى مِنْكُمْ فَلاَ يُصْبِحَنَّ بَعْدَ ثَالِثَةٍ وَبَقِيَ فِي بَيْتِهِ مِنْهُ شَيْءٌ ‏"‏ ‏.‏ فَلَمَّا كَانَ فِي الْعَامِ الْمُقْبِلِ قَالُوا : يَا رَسُولَ اللَّهِ نَفْعَلُ كَمَا فَعَلْنَا العَامَ الماضِي ؟ قَالَ : ‏"‏كُلُوْا ، وَأَطْعِمُوْا ، وَادَّخِرُوا ،  فَإِنَّ ذلِكَ العَامُ كَانَ بِالنَّاسِ جُهْدٌ ، فَأَرَدْتُ أَنْ تُعِيْنُوا فِيهَا‏"‏  

 

“Aliyedhwahi miongoni mwenu, basi kisibakie kwenye nyumba yake chochote baada ya asubuhi ya siku ya tatu”.  Na mwaka uliofuatia ulipowadia walisema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Je, tufanye kama tulivyofanya mwaka jana?  Akasema:  (Hapana, bali) kuleni, lisheni na wekeni akiba, kwa kuwa mwaka jana watu walikuwa na hali ngumu, hivyo nikataka muwasaidie”. [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5569) na Muslim (1973)].

 

Agizo hili la kula, kulisha na kuweka akiba nyama hapa, ni la sunnah na si la waajib kwa mujibu wa kauli ya Jumhuwr.  Hivyo basi, imestahabiwa kwa aliyedhwahi ale nyama ya mnyama wake, aweke akiba na alishe.  Na ‘Ulamaa wengi wanasema kwamba imestahabiwa atoe swadaqah theluthi moja ya nyama, alishe theluthi, na theluthi ya tatu ale yeye na familia yake. Lakini zimepokelewa aathaar dhwa’iyf  kuhusiana na hili.  Alaa kulli haal, anaweza kuigawa nyama vyovyote apendavyo kwa mujibu wa hali, na hata akitaka kuitoa yote swadaqah basi inajuzu.  ‘Aliy amesema:

 

"أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم أَمَرَهُ أَنْ يَقُومَ عَلَى بُدْنِهِ، وَأَنْ يَقْسِمَ بُدْنَهُ كُلَّهَا، لُحُومَهَا وَجُلُودَهَا وَجِلاَلَهَا، وَلاَ يُعْطِيَ فِي جِزَارَتِهَا شَيْئًا‏"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru asimamie uchinjaji wa ngamia wake, na awagawe wote kuanzia nyama zao, ngozi zao na (hata) matandiko waliyovishwa (au vigwe), na asitoe chochote kama malipo ya kuchinjiwa kutoka kwao”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1717) na Muslim (1317)].   

 

Share