02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: (Vinywaji) Pombe Kwa Aina Zake Zote Ni Haramu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الأَشْرِبَةُ

 

Vinywaji 

 

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

002- Vinywaji: Pombe Kwa Aina Zake Zote Ni Haramu

 

 

 

Hili limethibiti katika Qur-aan, Sunnah na Ijmaa.  Katika Qur-aan, Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾  إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ ﴿٩١﴾

 

“Enyi walioamini!  Hakika pombe, kamari,  masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli, ni najisi na chukizo kutokana na kazi ya shaytwaan, basi jiepusheni navyo mpate kufaulu •  Hakika shaytwaan anataka kukutilieni baina yenu uadui na bughudha katika pombe na kamari na akuzuieni kumdhukuru Allaah na Swalaah, basi je mtakoma?”.  [Al-Maaidah: 90-91].

 

Uharamisho wa pombe katika Aayaah hizi mbili, umepewa uzito kwa picha kadhaa za usisitizo.  Miongoni mwazo ni:   

 

(a)  Kutanguliwa Aayah na herufi ya "إِنَّمَا" .  Na hii ni herufi ya usisitizo na kulipa jambo uzito.

 

(b)  Allaah Ta’aalaa Ameiweka kundi moja na ibada ya masanamu.

 

(c)  Ameifanya kuwa ni najisi.

 

(d)  Ameifanya kuwa ni kazi ya shaytwaan, na shaytwaan haji isipokuwa na shari tupu.

 

(e)  Ameamuru iepukwe.

 

(f)  Amekufanya kuiepuka ndio mafanikio, hivyo basi, kuinywa hatima yake ni mbaya, lakini pia kunaondosha kheri na baraka zote.

 

(g)  Ametaja matokeo yake mabaya, nayo ni kuzalikana uadui na mizozano kwa wanywaji na wadau wake, mbali na kumzuia mtu asiweze kumdhukuru Allaah na kuchunga nyakati za Swalaah.

 

(h)  Kauli Yake Ta’aalaa:  "فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ" basi je mtakoma?.. ni maneno ya nguvu kabisa yaliyofikia ukomo wa mwisho wa kukemea.  Ni kama wanaambiwa:  Hakika mmesomewa ndani yake madhara yake mbalimbali na namna inavyowazuieni kumdhukuru Allaah, basi je mtaiacha pombe kwa sababu ya madhara haya, au mtaendelea na tabia yenu mliyokuwa nayo, iwe kama hamkuonywa wala kukemewa?!

 

Ama katika Sunnah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَعَنَ اللَّهُ الْخَمْرَ، وَشَارِبَهَا، وَسَاقِيَهَا، وَبَائِعَهَا، وَمُبْتَاعَهَا، وَعَاصِرَهَا، وَمُعْتَصِرَهَا، وَحَامِلَهَا، وَالْمَحْمُولَةَ إِلَيْهِ"

 

“Allaah Ameilaani pombe, mnywaji wake, mhudumu wake, muuzaji wake, mnunuzi wake, mkamuaji wake, mwenye kukamuliwa, mchukuzi wake na mwenye kupelekewa”. [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3674), At-Tirmidhiy (1295) na Ibn Maajah (3380)].

 

 

 

Share