000-Utangulizi Wa Tarjama Ya Alhidaaya.com

 

Utangulizi Wa Tarjama Ya Maana Ya Al-Qur-aan Al-‘Adhiwym

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

 

Himdi zote Anastahiki Allaah (سبحانه وتعالى) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) na Swahaba zake (رضي الله عنهم) na wote waliowafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Mwisho.

 

Qur-aan ni Maneno Matukufu ya Allaah Aliyoteremshiwa Nabiy wa mwisho Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) yenye kusadikisha yale yaliyokuja kabla yake katika Vitabu vilivyotangulia, na ni Maneno yasiyoweza kufikiwa na upotofu mbele yake wala nyuma yake kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ ﴿٤٢﴾

“Hakitokifikia ubatili mbele yake wala nyuma yake. Ni Uteremsho kutoka kwa Mwenye Hikmah wa yote, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.”[1]

 

 

Pia Qur-aan ni Kitabu cha mwisho chenye Risala (Ujumbe) kwa viumbe wote kutoka kwa Rabb wa walimwengu, kwa lengo la kuwaongoza viumbe kwenye njia iliyonyooka; na ni Mwongozo, Rahmah na Shifaa kwa Waumini.

 

 

Pia Qur-aan ni muujiza wa pekee, na wakati huo huo ni changamoto kwa viumbe wote. Hata kama viumbe vyote vitashirikiana ili vilete mfano wa Qur-aan basi havitoweza kuleta mfano wake; katika ufasaha wake, hukumu zake, ilimu zake, mwongozo wake na yote iliyoyaelezea.[2]

 

 

Qur-aan imekusanya yale yote yenye kuhitajiwa na viumbe; yawe ya dunia au ya Aakhirah yao, zikiwemo khabari za kabla yao na khabari za baada yao, na ni muamuzi na hakimu kwa Waumini wake, na ni Kitabu Alichohitimishia Allaah Sharia Zake.

 

 

Ni katika desturi Zake Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa kila Rasuli akitumwa huwa anapelekwa kwa lugha ya watu wake ili aweze kuwafikishia ujumbe. Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ۖ

“Na Hatukutuma Rasuli yeyote isipokuwa kwa lugha ya kaumu yake ili awabainishie (Risala).”[3]

 

 

Ni jambo lenye kujulikana kuwa lugha ya Quraysh ambayo ni lugha ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), ilikuwa ni Kiarabu sanifu. Na kwa sababu hiyo, ujumbe uliokuja ndani ya Qur-aan ulikuja katika lugha ya Kiarabu, ambayo ndiyo lugha fasaha kuliko lugha zote.[4]  

 

 

Usomaji wa Qur-aan katika lugha yake, kwa walengwa wake wengi wasiokuwa Waarabu ambao hawakuafikishwa kuisoma lugha ya Kiarabu na kuifahamu vizuri, haswa Qur-aan na taaluma zake, haukuweza kuwafikisha kufahamu misingi ya Dini yao, hivyo basi, ndio pakawa na haja na umuhimu mkubwa wa kuweko Tarjama itakayoweza kumsaidia Muislamu kuweza kufahamu anachosemeshwa na Rabb wake, ikiwa maamrisho apate kuyatekeleza, na ikiwa makatazo apate kuyaepuka.

 

 

Kadhaalika, kuna ilimu na fani nyingi ambazo zimefungamana na kushikamana na Qur-aan zenye kuweza kusaidia katika kufikia kufahamu Tafsiyr ya Aayah. Ni kama vile ilimu ya Uswuwl ya Tafsiyr pamoja na kutabahari (kubobea) katika fani zote zile ambazo hakuna njia ya kufahamika Tafsiyr wala kuwa sahihi isipokuwa kwayo, kama vile kufahamu sababu za kuteremka kwa Suwrah au Aayah (Asbaab An-Nuzuwl) pamoja na za mwanzo na za mwisho kuteremka. Pia Naasikh wa Mansuwkh (kinachofuta na kilichofutwa), ukusanyaji wake, mpangilio wa Aayah na Suwrah zake, visa vyake, mifano yake, kujibu tuhuma dhidi yake na kadhalika. Hivyo, Tafsiyr inayokubalika ni ile yenye kufuata Manhaj iliyoelezwa juu inayotegemea zaidi nukuu badala ya mawazo au rai ya Mfasiri.

 

 

Mkusanyiko wa hayo yote na mengineyo ndani ya sayansi hiyo unadhihirisha kuwa kunahitajika uangalifu mkubwa katika kukata shauri na kutoa hukumu kuhusu maana ya Maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى). Ndio ikawa njia pekee sahihi na ya salama ya kufanikisha hilo, ni kwa kushikamana na kutegemea yale yaliyopokelewa na kuthibiti kutoka kwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) na Swahaba (رضي الله عنهم)  na wala si kutokana na rai.

 

 

La msingi na lililo muhimu katika kazi ya Tarjama ambalo ni sharti katika masharti ya anayefanya hiyo Tarjama ni kuwa awe mtu mwenye kushikamana na msingi madhubuti wa kufuata Manhaj ya Salaf[5] na wala si msingi wa kuzusha au ubunifu. Atakapokuwa ameshikamana na Manhaj sahihi ya Salaf, basi hivyo ndivyo kutampeleka na kumlazimisha kama ni sehemu ya ‘Aqiydah yake, kushikamana na zile Tarjama zenye kwenda sambamba na mafundisho ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), zenye kunukuu kauli za Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), au kauli za Swahaba (رضي الله عنهم)  au kauli za Taabi’iyn[6] na Atbaa’ Taabi’iyn.[7]  

 

 

Kutokana na hali hii basi, Mufassiruna wa Qur-aan wameweka Manhaj maalumu ya Tafsiyr ya kufuatwa na kushikiliwa na ambayo kwayo kwa kuipitia vizuri, ndipo tutaweza kupata Tarjama iliyo sahihi.

 

1.     Tafsiyr Ya Qur-aan Kwa Qur-aan

 

 

Kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan ndio njia ya kwanza inayopasa kufuatwa, kwani Qur-aan inajifasiri yenyewe kwa yenyewe. Utakuta pahala inaeleza jambo kwa kifupi na pahala pengine inalieleza jambo hilo hilo kwa ufafanuzi na kwa uchambuzi. Jambo inalolieleza kwa ujumla katika sehemu moja hulieleza kwa kuliwekea ima mipaka au kulihusisha kwa watu makhsusi katika sehemu nyingine. Hivyo, njia iliyo sahihi kabisa katika kufasiri Qur-aan, ni kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan.[8]

 

 

Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema: “Kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan ni njia bora kabisa inayofikisha Risala (Ujumbe) na kuifafanua. Na si ajabu kwani Allaah (سبحانه وتعالى) ni Mjuzi wa malengo na makusudio Yake. Anafafanua Aayah Zake kwa Aayah nyinginezo. Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

وَكَذَٰلِكَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ وَلِيَقُولُوا دَرَسْتَ وَلِنُبَيِّنَهُ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿١٠٥﴾

“Na hivyo ndivyo Tunavyosarifu namna kwa namna Aayaat ili (makafiri) waseme: Umedurusu (kutoka kwa Watu wa Kitabu), na ili pia Tuibainishe kwa watu wenye kujua.”[9]

 

 

Ni jambo lisilopingika kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akifahamu kikamilifu kila kilichoelezwa ndani ya Qur-aan na ndio akawa wa kwanza kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan kama ilivyopokewa kuwa alifasiri baadhi ya Aayah kwa Aayah nyinginezo.[10]

 

 

Swahaba (رضي الله عنهم)  walishuhudia na kumsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akifasiri Qur-aan kwa Qur-aan, hivyo nao kama ilivyo desturi yao, walimuiga katika hilo pia kama walivyokuwa wakimuiga katika mengineyo, na kwa kufahamu kuwa ni jukumu lao kufikisha kila walichochukua kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuwafikishia wataokuja baada yao. Hivyo basi Swahaba (رضي الله عنهم) waliwafunza Taabi’iyn [Waislamu ambao hawakumuwahi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika uhai wake], kila walichopokea kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) tena kwa muradi wake Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Taabi’iyn nao waliwafunza Atbaa’ Taabi’iyn (Waislamu ambao hawakuwawahi Swahaba katika uhai wao) kila walichopokea na kuchukua kutoka kwa waalimu wao ambao ni Swahaba (رضي الله عنهم). Kisha nao kwa upande wao walinukuu na kufikisha kwa waliokuja baada yao, tena kwa muradi ule ule walioupokea na kuuchukua kutoka kwa Swahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na katika waliyoyapokea ni aina hii ya kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan.  

 

 

Hivyo, haijuzu wala si sahihi kuiacha aina hii ya Tafsiyr na kuiendea nyingine ikiwa Aayah husika ina Aayah nyingine iliyoifasiri kama ilivyo katika mifano ifuatayo: Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّة فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٥٩﴾

“Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghaibu, hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Anajua yale yote yaliyomo barani na baharini. Na halianguki jani lolote ila Hulijua, wala punje katika viza vya ardhi, wala kinyevu na kikavu isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha wazi.”[11]

 

Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwabainishia na kuwawekea wazi kuwa funguo za ghaibu ni tano; kwa kuwasomea kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى) ifuatayo:

 

 إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾

“Hakika Allaah Ana ujuzi wa Saa (Qiyaamah), na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika matumbo ya uzazi. Na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani.  Hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye Khabari za dhahiri na siri.”[12]

 

 

Mfano mwengine ni pale Allaah (سبحانه وتعالى) Anaposema:

 

 

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٨٢﴾

“Wale walioamini na hawakuchanganya imaan zao na dhulma, hao ndio watakaopata amani nao ndio waliohidika.”[13]

 

 

Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwabainishia Swahaba na kuwawekea wazi kuwa dhulma ni shirki kwa kuwasomea Aayah ifuatayo:

 

وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

“Na Luqmaan alipomwambia mwanawe huku akimuwaidhi: Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno!”[14]

 

 

2.     Kufasiri Qur-aan Kwa Sunnah[15] Za Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

Sunnah inafasiri, inasherehesha na inabainisha Qur-aan kwa kudhihirisha yasiyokuwa dhahiri. Sunnah inaisherehesha Qur-aan kwa kuyachambua, kuyapambanua na kwa kuyaainisha yale ambayo Qur-aan imeyaelezea kwa ujumla. Sunnah inaweka mipaka kwa yale yasiyokuwa yamewekewa mipaka na Qur-aan. Sunnah inayachambua yaliyotolewa hukumu kwa pamoja, ikifafanua yaliyoachwa wazi hukumu zake. Yote hayo kwa kuwa katika Qur-aan, kuna yasiyoweza kufahamika isipokuwa kwa kupata ufafanuzi na kuwekwa wazi na Sunnah za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kama vile uchambuzi wake (صلى الله عليه وآله وسلم) katika namna za amri na makatazo, idadi za Rakaa za Swalaah, utekelezaji wa ‘Umrah na Hajj, viwango vya yale Aliyofaradhisha Allaah (سبحانه وتعالى) katika hukumu.[16]

 

 

Basi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alibainisha na kufafanua kwa kufasiri maana za Aayah za Qur-aan kwa Swahaba zake (رضي الله عنهم) kama inavyoashiria Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ﴿٤٤﴾

“Na Tumekuteremshia Ukumbusho (Qur-aan) ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao huenda wakapata kutafakari.”[17]

 

 

Ufafanuzi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ni kitu kisichoweza kuepukika, na ndio akaweka wazi kwa kusema kuwa hakupewa Qur-aan pekee, bali alipewa pamoja na Qur-aan kinachofanana nayo.[18]

 

 

Umahiri katika lugha ya Kiarabu pekee haukuwa wenye kutosheleza wala hautatosheleza katika kufahamu kusudio la Maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kutafuta msaada kutoka kwenye Sunnah. Kama ilivyokuwa hali kwa Swahaba (رضي الله عنهم)  japokuwa walikuwa wenye ufasaha na umiliki kamili wa lugha ya Kiarabu, lakini walikuwa wakitatanishwa au wakati mwengine wakifahamu baadhi za Aayah kinyume na inavyotakiwa ifahamike, jambo lililowapelekea kurejea kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kutafuta ufafanuzi. Basi hufasiri Aayah au neno ambalo Swahaba (رضي الله عنهم)  hawakuweza kuifahamu Tafsiyr yake au walipofahamu kinyume na inavyotakiwa ifahamike.

 

 

Kuna mifano mingi tu ya Aayah za Qur-aan ambapo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amezifasiri na kuzifafanua.

 

 

Mfano neno la الْكَوْثَرَ

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alilifasiri nenoالْكَوْثَرَ  katika Suwrah Al-Kawthar:  

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ﴿١﴾

“Hakika Sisi Tumekupa (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Al-Kawthar[19] (Mto katika Jannah).”

 

kuwa ni Mto katika Jannnah, maana ambayo haikufahamika isipokuwa kwa njia ya kufafanuliwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) : ((إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ)) أَنّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، قَالَ: ((هُوَ نَهْرٌ فِي الْجَنَّةِ))

Amesimulia Anas (رضي الله عنه) : Kuhusu kauli yake Allaah:

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ

“Hakika Sisi Tumekupa Al-Kawthar.”

 

Kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Huo ni Mto katika Jannah.”[20]  

 

 

Mfano mwengine ni neno زِيَادَةٌ

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alifasiri kwa kubainisha kuwa neno زِيَادَةٌ   katika Aayah ya Suwrat Yuwnus,

 

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ

“Kwa wale waliofanya ihsaan watapata (huko Jannah) jazaa nzuri kabisa na ziada (kumuona Allaah).”[21]

 

 

Kuwa maana ya ziada ni kumuona Allaah (سبحانه وتعالى), maana ambayo haikufahamika isipokuwa kwa njia ya ufafanuzi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

عَنْ صُهَيْبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِذَا دَخَلَ أَهْلُ الْجَنَّةِ الْجَنَّةَ نُودُوا: يَا أَهْلَ الْجَنَّةِ، إِنَّ لَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ مَوْعِدًا لَمْ تَرَوْهُ، فَقَالُوا: وَمَا هُوَ؟ أَلَمْ تُبَيِّضْ وُجُوهَنَا وَتُزَحْزِحْنَا عَنِ النَّارِ، وَتُدْخِلْنَا الْجَنَّةَ؟)) قَالَ: ((فَيُكْشَفُ الْحِجَابُ، فَيَنْظُرُونَ إِلَيْهِ، فَوَاللَّهِ مَا أَعْطَاهُمْ اللَّهُ شَيْئًا أَحَبَّ إِلَيْهِمْ مِنْهُ)) ثُمَّ تَلاَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَى وَزِيَادَةٌ))

Amesimulia Swuhayb (رضي الله عنه) : Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watakapoingia Watu wa Jannah katika Jannah (Pepo), wataitwa: Enyi Watu wa Jannah! Hakika nyinyi mna ahadi kwa Rabb wenu bado hamjaiona. Watauliza: Ni (ahadi) ipi hiyo? Kwani Hukuzing’arisha nyuso zetu, na Hukutuokoa na moto, na Hukutuingiza Jannah?” Akasema: “Litaondoshwa pazia, na watamtazama Allaah. Basi Wa-Allaahi, Hakuwahi Allaah kuwapa jambo walolipenda zaidi kuliko hilo (kumuona Allaah).” Kisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasoma Aayah hii:

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ

“Kwa wale waliofanya ihsaan watapata (huko Jannah) jazaa nzuri kabisa na ziada (kumuona Allaah).”[22]

 

 

Hii inathibitisha kuwa ufafanuzi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ni wenye umuhimu mkubwa katika kufasiri Qur-aan, kwani ni ufafanuzi wa aina yake pekee na wenye thamani isiyoweza kununulika wala kukadirika. Ndio ikawa Qur-aan inaihitaji Sunnah (Hadiyth), na ndio ikawa hakuna kitabu katika vitabu vya Hadiyth isipokuwa kutakuwepo mlango wa Tafsiyr Maathuwr.[23]

 

 

3.     Kufasiri Qur-aan Kwa Kauli Za Swahaba (رضي الله عنهم) 

 

Kauli (Tafsiyr) za Swahaba  (رضي الله عنهم) ni chanzo cha tatu cha kutafuta ufafanuzi pale inapokuwa haujapatikana kutoka vyanzo viwili vilivyotangulia, kama alivyosema Al-Haafidhw Ibn Kathiyr katika utangulizi wa Tafsiyr yake kuwa: “Tutakapokuwa hatukufanikiwa kupata Tafsiyr katika Qur-aan au Sunnah, tutarejea katika kauli za Swahaba (رضي الله عنهم)  kwani wao waliifahamu Qur-aan vilivyo kwa ufasaha na sarufi zake, na kwa kuwa walishuhudia matukio yaliyosababisha kuteremshwa kwa Aayah au Suwrah husika. Hakuna aliyeyashuhudia isipokuwa wao, na pia kutokana na wao kuwa na ilimu sahihi na amali njema haswa haswa Wanachuoni miongoni mwao.”[24]

 

 

Swahaba (رضي الله عنهم)  walijifunza Qur-aan na ilimu yake kwa kina kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).[25]

 

 

Hata hivyo, ufahamu wa Swahaba (رضي الله عنهم)  wa Qur-aan haukuwa wa daraja moja kwani miongoni mwao (رضي الله عنهم)   wako waliojulikana kuwa ni wafasiri wa Qur-aan, kama vile Makhalifa wanne (رضي الله عنهم), Ibn Mas’uwd[26] ambaye alikuwa akijulikana miongoni mwa Swahaba kuwa ni mjuzi wao wa Qur-aan (kuisoma na kuifasiri). Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما),[27] pia Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)  na wengineo ambao walikuwa na ufahamu uliokamilika kwa vile ulijengeka juu ya ilimu iliyo sahihi iliyopambika kwa amali njema. Hivyo, Tafsiyr zao zina thamani, uzito na umuhimu mkubwa mpaka ikawa Tafsiyr ya Swahaba inachukua hukumu ya Al-Marfuw[28] haswa inapojulikana kuwa Swahaba huyo hakuwahi kupokea Israaiyliyyaat[29] katika hilo.

 

 

Kilichojitokeza ni kuwa hakuna Tafsiyr iliyoandikwa katika wakati wao, kwani ilikuwa ni sehemu katika Hadiyth.

 

 

Mfano wa Tafsiyr ya neno لَامَسْتُمُ  (mmewagusa) kuwa ni kujimai katika kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ

“au mmewagusa wanawake.”[30]

 

Ibn ‘Abbaas alilitafsiri kwa kusema kuwa: “Ni kujimai.”[31]

 

 

Mfano mwengine ni Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِى لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٦﴾

“Na miongoni mwa watu, yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) Njia ya Allaah bila ilimu, na huzichukulia (Aayaat) mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha.”[32]

 

 

Ibn Mas'uwd (رضي الله عنه) amesema kuhusu Aayah hii: “Naapa kwa Jina la Allaah! Hii inamaanisha ni muziki.”[33]

 

Mfano mwengine ni kuhusu Sa’yi baina ya majabali mawili ya Swafaa na Marwah kulikotajwa kwenye kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ اللَّـهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ ﴿١٥٨﴾

“Hakika Swafaa na Marwah ni katika Alama za Allaah. Kwa hiyo yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah, hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo. Na atakayejitolea kufanya kheri, basi hakika Allaah Ni Mwenye Kupokea Shukurani, Mjuzi wa yote.”[34] 

 

 

Baadhi ya Swahaba (رضي الله عنهم)  walifahamu kinyume na vile inavyotakiwa ifahamike Aayah hiyo. Mmojawao ni baba wa Hishaam bin ‘Urwah. Alimuuliza Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) ambaye alimfahamisha kwa kutumia Sababun-Nuzuwl (Sababu ya kuteremshwa) ili aweze kufahamu usahihi wa maana ya Aayah kama ilivyothibiti katika kauli ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)  katika usimulizi ufuatao:

 

عَنْ هِشَامِ بْنِ عُرْوَةَ، عَنْ أَبِيهِ، أَنَّهُ قَالَ: قُلْتُ لِعَائِشَةَ زَوْجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، وَأَنَا يَوْمَئِذٍ حَدِيثُ السِّنِّ: "أَرَأَيْتِ قَوْلَ اللَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: ((إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِنْ شَعَائِرِ اللَّهِ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ يَطَّوَّفَ بِهِمَا))  فَمَا أُرَى عَلَى أَحَدٍ شَيْئًا أَنْ لَا يَطَّوَّفَ بِهِمَا، فَقَالَتْ عَائِشَةُ: "كَلَّا، لَوْ كَانَتْ كَمَا تَقُولُ، كَانَتْ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ لَا يَطَّوَّفَ بِهِمَا، إِنَّمَا أُنْزِلَتْ هَذِهِ الْآيَةُ فِي الْأَنْصَارِ كَانُوا يُهِلُّونَ لِمَنَاةَ، وَكَانَتْ مَنَاةُ حَذْوَ قُدَيْدٍ، وَكَانُوا يَتَحَرَّجُونَ أَنْ يَطُوفُوا بَيْنَ الصَّفَا وَالْمَرْوَةِ، فَلَمَّا جَاءَ الْإِسْلَامُ سَأَلُوا رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ ذَلِكَ، فَأَنْزَلَ اللَّهُ: ((إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِنْ شَعَائِرِ اللَّهِ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ يَطَّوَّفَ بِهِمَا))

 

Amesimulia Hishaam bin ‘Urwah kutoka kwa baba yake alisema: Nilimwambia ‘Aaishah (رضي الله عنها)  mke wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na mimi wakati huo ni kijana mdogo: Unaionaje Kauli ya Allaah (تبارك وتعالى),  

 

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ  

“Hakika Swafaa na Marwah ni katika Alama za Allaah. Kwa hiyo yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah, hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo. Na atakayejitolea kufanya kheri, basi hakika Allaah Ni Mwenye Kupokea Shukurani, Mjuzi wa yote.”

 

Sioni kama kutakuwa na kitu juu ya yeyote ikiwa hatotufu baina yake. Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)  akasema: Si hivyo! Ingelikuwa kama unavyosema basi ingekuwa (hivi): Hakutokuwa na dhambi juu yake kama hatotufu baina ya (vilima) viwili hivyo. Kwa hakika Aayah hii imeteremshwa kuhusiana na Answaar ambao walikuwa wakilitukuza Manaat (wakiliabudu sanamu hilo na wakilifanyia Hijjah na wakilitufu), lakini walikuwa hawatufu (Sa’yi baina ya Swafaa na Marwah) na lilikuwa hilo sanamu la Manaat likielekea (kijiji cha) Qadiyd, hivyo walikuwa wakiona tabu kulitufu. Ulipokuja Uislamu walimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu hivyo (Sa’yi baina ya Swafaa na Marwah), ndio Allaah Akateremsha:

 

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ اللَّـهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ ﴿١٥٨﴾

“Hakika Swafaa na Marwah ni katika Alama za Allaah. Kwa hiyo yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah, hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo. Na atakayejitolea kufanya kheri, basi hakika Allaah Ni Mwenye Kupokea Shukurani, Mjuzi wa yote.[35] 

 

 

4.     Kufasiri Qur-aan Kwa Kauli Za Taabi’iyn

 

 

Kutakaposhindwa kupatikana Tafsiyr ya Aayah husika kwenye Qur-aan, au kwenye Sunnah, au kwenye kauli za Swahaba (رضي الله عنهم), ‘Ulamaa[36]  hurejea kwenye kauli za Taabi’iyn, kwani kama walivyotajika baadhi ya Swahaba (رضي الله عنهم)   kwa Tafsiyr, wametajika pia baadhi ya Taabi’iyn[37] kwa Tafsiyr.

 

 

Taabi’iyn walitegemea katika Tafsiyr zao, ufahamu wao wa Qur-aan kutokana na yaliyokuja ndani ya Qur-aan yenyewe, na yale waliyoyapokea kutokana na Swahaba (رضي الله عنهم), kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na yale Aliyowafungulia Allaah kupitia njia ya ijtihaad na utafiti wao katika Qur-aan na wala hawakuwa tayari kutumia rai zao.[38]

 

 

Kinachofahamika ni kuwa Tafsiyr zilizopokelewa kutokana na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na pia kutokana na Swahaba (رضي الله عنهم)  hazikuwa za Qur-aan yote, bali zilikuwa ni zenye kuhusiana na baadhi ya Aayah za Qur-aan au baadhi ya maneno ya Aayah ambayo yalionekana kuwa ni miongoni mwa yale yenye kuhitaji ufafanuzi kwa wale waliokuwa katika zama hizo. Kutofahamika huku, huwa kunazidi kila pale wanapobaidika watu na zama za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na Swahaba (رضي الله عنهم). Hivyo wale wenye kujishughulisha na fani ya Tafsiyr miongoni mwa Taabi’iyn, wakaongeza katika Tafsiyr kadiri ya kule kuongezeka kutofahamika, kisha baada yao wakaja wale waliokamilisha Tafsiyr ya Qur-aan huku wakitegemea juu ya yale waliyoyafahamu katika lugha na lahaja za Waarabu, na juu ya yale yaliyothibiti kuwa ni sahihi kwao katika matukio yaliyotokea wakati wa kuteremka Qur-aan.

 

 

Taabi’iyn wametunukiwa daraja ya kuwa miongoni mwa watu bora kabisa[39] kwa kuwa walichukua na kuchota ilimu zao kutoka vyanzo sahihi na vilivyoasisiwa kwa misingi sahihi.

 

 

Mfano wa Tafsiyr ya neno قَانِتُونَ  katika Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَقَالُوا اتَّخَذَ اللَّـهُ وَلَدًا ۗ سُبْحَانَهُ ۖ بَل لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ كُلٌّ لَّهُ قَانِتُونَ ﴿١١٦﴾

“Na wakasema: Allaah Amejichukulia mwana. Utakasifu Ni Wake! Bali ni Vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, vyote vinamtii.”[40]

  

 

Kuhusiana na neno قَانِتُونَ Mujaahid alilifasiri kwa kusema kuwa: “Ni kutii. Na kwamba utiifu wa kafiri hupatikana pale kivuli chake kinaposujudu wakati ambapo yeye mwenyewe (kafiri) ni mwenye kuchukia hilo.”[41]

 

 

Mfano mwengine ni kuhusiana na Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قَالَ أَنَا أُحْيِي وَأُمِيتُ ﴿٢٥٨﴾

“Akasema: Mimi (pia) nahuisha na kufisha.”[42]

 

 

Kuhusiana na ibara hii: Mimi (pia) nahuisha na kufisha.” Qataadah amesema kuwa yule mfalme aliyemuhoji Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) alimaanisha kuwa: Watu wawili waliostahiki kuuawa, wangeletwa mbele yake, na angeliamrisha mmoja wao auawe basi angeliuawa. Na angeliamrisha kuwa mtu wa pili asamehewe, basi angesamehewa. Hivi ndivyo ninavyoleta uhai na kifo.[43]

 

 

Hivyo Tafsiyr ya Taabi’iyn ni chanzo chengine cha kutafuta ufafanuzi pale inapokuwa haujapatikana ufafanuzi kutoka kwenye vyanzo vilivyotangulia. Hata hivyo baadhi ya Wanachuoni wanaonelea kuwa Tafsiyr za Taabi’iyn na wanafunzi wao hazitoki moja kwa moja kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na wala si kama Tafsiyr za Swahaba (رضي الله عنهم), yote kwa kuwa Taabi’iyn na wanafunzi wao hawajamuona Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na wala hawakushuhudia Wahy pale zinapoteremshwa Aayah. Na vilevile si wote wanakubalika uaminifu wao, kwa kuwa wao si kama Swahaba (رضي الله عنهم)    ambao uaminifu na uadilifu wao umeshuhudiwa na kuthibitishwa na Qur-aan. Ama wao Taabi’iyn na wanafunzi wao wamesifiwa kama ni ‘karne’ na si mmoja mmoja.

 

 

Hata hivyo, maelezo mazuri na ya salama ni yale ya Shu‘bah bin Al-Hajjaaj na wengineo ambayo ameyanukuu Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: “Kauli za Taabi’iyn katika furuw’ (matawi ya Sharia) si hoja, basi vipi zitakuwa hoja katika Tafsiyr. Kwa maana kuwa haziwi hoja juu ya wengineo wasiokuwa wao miongoni mwa wale waliowakhalifu, na hii ndio sahihi. Ama pale watakapokubaliana juu ya kitu, basi bila shaka yoyote ile ni hoja. Na endapo watakhitalifiana basi haitokuwa kauli ya baadhi yao hoja juu ya wengine. Na wala juu ya watakaokuja baada yao, bali kutafuatwa na kutazamwa lugha ya Qur-aan, au Sunnah, au kauli za Swahaba (رضي الله عنهم).“[44]

 

 

Hakuna shaka yoyote ile kwamba ujuzi wa lugha ya Kiarabu na matawi yake una mchango mkubwa na ni ufunguo katika kuifahamu Qur-aan na kuweza kupata Tafsiyr yenye kukubalika. Hivyo basi, ufahamu sahihi wa Tafsiyr ya Qur-aan, makusudio yake na yote yenye kufungamana nayo, unafungamana pia na ufahamu sahihi wa lugha ya Kiarabu na matawi yake.

 

 

Ilimu ya Tarjama ilibuniwa na kupelekea kuweko Tarjama nyingi sana katika kila zama na kila pahala na kwa lugha maarufu za walimwengu, jambo lililopelekea kumwezesha mlengwa kuweza kufahamu aliyolengewa kuyafahamu. Lakini, huenda Tarjama nyingi zikawa zimefanikiwa kumwezesha mlengwa kufahamu Maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kiasi fulani na kufahamu baadhi ya makusudio ya Aayaat katika upande wa Sharia. Ama kwenye upande wa ‘Aqiydah (Itikadi), baadhi ya Tarjama, hazikufanikiwa kumwezesha Muislamu kupata ufahamu wa wazi wa mas-ala muhimu ya ‘Aqiydah Sahihi kwa kuyatanabahisha na kuyafafanua kiwaziwazi baadhi ya mas-ala hayo ya ‘Aqiydah, mas-ala ambayo yana ufahamu usio sahihi katika itikadi za madhehebu mengineyo.

 

 

Hivyo basi, katika Tarjama hii[45], tumejitahidi kubainisha na kuyafafanua kwa dalili baadhi ya mas-ala yanayohusiana na ‘Aqiydah sahihi ili yamwezeshe mwenye kuzungumza Kiswahili afahamu pale alipotakiwa kufika kiitikadi; ‘Aqiydah iliyobalighishwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na inayorandana na ‘Aqiydah ya Salaf Asw-Swaalih (Wema waliotangulia) miongoni mwa Swahaba, Taabi’iyn na Atbaa' Taabi’iyn na waliowafuata kwa wema.

 

 

Mifano ya baadhi ya mas-ala hayo ya ‘Aqiydah:

 

(i) Kuthibitisha Sifa za Allaah (سبحانه وتعالى) kama Aliyojithibitishia Mwenyewe (سبحانه وتعالى). Mifano: Wajihi Wake. Rejea Al-Qaswasw (28:88), Al-Baqarah (2:115) na Ar-Rahmaan (55:27). Mkono au Mikono Yake. Rejea Al-Fat-h (48:10). Macho Yake. Rejea Huwd (11:37). Nafsi Yake. Rejea Aal-‘Imraan (3:28). Na Sifa nyenginezo bila ya Ta'twiyl (kuzipinga, kukanusha uwezekano), wala Tamthiyl (kumithilisha, kufafanisha, kulinganisha), wala Takyiyf (kuainisha maana na kuziulizia namna yake au kuuliza ni vipi Sifa hiyo ipo, kuchunguza ni kwa “namna gani” zimefungamana au kuambatana na Allaah), wala Tahriyf (kubadilisha maana, kupotosha Sifa ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kutoa maana isiyo sahihi).

 

 

Na hakuna khofu wala shaka kuwa Sifa za Allaah (سبحانه وتعالى) zikithibitishwa kama zilivyotajwa katika Qur-aan, kwamba atashabihishwa Muumba na Viumbe Vyake! Hiyo si hoja muwafaka, kwani imaan thabiti ya Muislamu kuhusiana na Allaah (سبحانه وتعالى) ni kuwa: Hapana anayefanana Naye (Muumba) hata mmoja wala hakuna kitu chochote mfano Wake kama inavyothibitishwa na Allaah (سبحانه وتعالى) Mwenyewe.[46]

 

 

(ii) Kuthibitisha Sifa ya Allaah (سبحانه وتعالى)  ya Al-‘Uluww. Na  kwamba Allaah Yuko juu ya Mbingu Zake saba, juu ya ‘Arsh Yake, na Ametenganishwa na viumbe Vyake, na viumbe Vyake vimetenganishwa Naye. Rejea Al-Mulk (67:16). Ama Anaposema Yuko na Waja Wake basi ‘Aqiydah sahihi ni kuamini kwamba Yuko na Waja Wake kwa Ujuzi Wake tu na si kwa Dhati Yake. Rejea Al-Mujaadalah (58:7). 

 

 

(iii) Istawaa: Kuamini Kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Yuko juu Ya ‘Arsh Yake kama Alivyojijulisha Mwenyewe. Na kuweko huko juu ya ‘Arsh Yake, ni kulingana na Utukufu, Uadhama, Uajalali Wake na Ukamilifu Wake. Rejea Al-A’raaf (7:54) na Twaahaa (20:5).

 

 

(iv) Kuamini kwamba Qur-aan ni Kalaamu-Allaah (Maneno ya Allaah) na kwamba hayakuumbwa. Rejea At-Tawbah (9:6).

 

 

(v) Kuamini kwamba Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام)  Yuhai na Atateremka duniani kutoka mbinguni iwe ni alama mojawapo kubwa za Qiyaamah. Rejea  An-Nisaa (4:159), Aal-‘Imraan (3:55) na rejea nyenginezo zilizotajwa humo.

 

 

(vi) Kuamini kwamba Waumini watamuona Allaah (سبحانه وتعالى) watakapokuwa Jannah (Peponi). Rejea Yuwnus (10:26) na Al-Qiyaamah (75:23).

 

 

(vii) Kuamini Kalaam (Kuongea): Kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anaongea kama Alivyoongea na Nabiy Muwsaa (عليه السّلام). Rejea An-Nisaa (4:164), Al-A’raaf (7:143).

 

 

Kwa minajili hiyo, tukaona kuna umuhimu wa kuweko kwa Tarjama itakayokwenda sambamba na Manhaj ya Salaf haswa katika kuibalighisha na kuidhihirisha ile ‘Aqiydah iliyobalighishwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ambayo iko wazi kwenye Qur-aan kwa atakaye kushikamana nayo.

 

 

Pia, tumeona ni vyema na ndio sahihi ndani ya kazi hii pia, kulithibitisha Jina la ‘Allaah’ badala ya kulifasiri kwa kuligeuza na kutumia neno ‘Mwenyezi Mungu’, kama linavyotumika katika karibu Tarjama zote za lugha ya Kiswahili, kwani Allaah ni Pekee na mungu inatumika kwa miungu wengi hata kama itaunganishwa na ‘mwenyezi.’ Ni imaan yetu kuwa kulithibitisha jina Lake ‘Allaah’ kama lilivyothibiti, ni kumuadhimisha Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) na kulipa haki Jina Lake Tukufu kwani hakuna mwenye Majina kama Yake Allaah (سبحانه وتعالى). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا فَاعْبُدْهُ وَاصْطَبِرْ لِعِبَادَتِهِ ۚ هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا ﴿٦٥﴾

“Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake. Basi mwabudu Yeye tu na dumisha subira katika Ibaada Yake. Je, unamjua yeyote anayefanana Naye (Allaah)?” [Maryam (19:65)][47]

 

 

Na kubwa na la muhimu zaidi ni kuwa kuna thawabu kwa kuwa ndivyo lilivyothibiti. Hivyo, tutalitumia na kulithibitisha Jina la ‘Allaah’ pote katika Tarjama hii kama lilivyothibitishwa na Qur-aan na Sunnah za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa lengo la kuwarejesha Waumini katika kutumia Majina ya Allaah kama yalivyothibiti.

 

 

Hali kadhaalika, tumethibitisha Sifa ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya ‘Rabb’ kwa kuibakisha kama ilivyo katika asli yake bila kuipa maana, kwa sababu neno ‘Rabb’ linatumika Kiswahili kama ‘Rabi’ na linafahamika. Ama kulipa maana ya ‘Mola’ tumeona ni maana finyu isiyokidhi taarifu kamili ya ‘Rabb’ kwa sababu ‘Ar-Rabb’ ina maana nyingi na pana. Inaweza kumaanisha: Mfalme, Bwana, Mlezi, Mwendeshaji, Mpangaji, Mola, Msimamiaji, Mwenye Kuneemesha, Mwenye Kuruzuku n.k. Hivyo, tumeonelea litumike kwenye Tarjama hii hivyo hivyo lilivyo.

 

 

Pia, tumejaribu sana kutumia misamiati ya lugha ya Kiswahili, ambayo inalingana sawasawa katika maana na misamiati ya lugha ya Kiarabu, ili iwafikiane na makusudio ya neno la asili la Kiarabu. Na misamiati mingineyo ambayo hayafahamiki kiwepesi katika jamii, tumeyawekea ufafanuzi katika Faharasa. Na baadhi ya misamiati hiyo, inapatikana katika Kamusi za Kiswahili zifuatazo: (i) Kamusi Ya Kiswahili Sanifu (ii) Kamusi Ya Maana Na Matumizi (iii) Kamusi Ya Visawe. 

 

 

Vilevile, tumeweka baadhi ya faida au tanbihi ili nazo zimpanulie ufahamu msomaji na kumuongezea ilimu ya ufahamu wa Qur-aan.

 

 

Pia katika kila Suwrah, tumetanguliza Tangulizi za Suwrah; humo tumetaja Maqaaswid As-Suwrah[48] (Makusudio ya Suwrah), maudhui za Suwrah kwa mukhtasari, fadhila za Suwrah na faida nyenginezo.

 

 

Pia tumeambatanisha katika faharasa, kurasa zenye maana ya Majina Mazuri Kabisa ya Allaah na Sifa Zake Kamilifu, ili zimfaidishe msomaji na kumuongezea ilimu.

 

 

Msomaji akipendelea kupata faida ya ziyada zifuatazo: (i) Sababu Za Kuteremshwa (Asbaabun-Nuzuwl) Suwrah au Aayah za Qur-aan (ii)  Kinachofuta Na Kinachofutwa (An-Naasikh Wal-Mansuwkh) ambayo ni ujuzi wa kujua Aayah zilizofutwa hukmu zake na ambazo zikateremshwa Aayah nyenginezo badala yake (iii) Aayah Na Mafunzo (iv) Tafsiyr Al-Muyassar iliyofasiriwa kwa Kiswahili, basi atembelee Tovuti ya Alhidaaya.com  ambako masomo hayo yameorodheshwa kwa bayana. Njia ya kuzifikia ni ifuatavyo:

 

Maudhui Za Qur-aan > Tangulizi Za Suwrah

 

Maudhui Za Qur-aan > Tafsiyr Al-Muyassar (Kiswahili)

 

Maudhui Za Qur-aan > Tafseer As-Sa’di (Kiarabu)

 

Maudhui Za Qur-aan > Tafseer As-Sa’di (Kiingereza)

 

Maudhui Za Qur-aan > Asbaabun-Nuzuwl (Sababu Za Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah.

 

Maudhui Za Qur-aan > An-Naasikh Wal-Mansuwkh (Kinachofuta Na Kinachofutwa)

 

Maudhui Za Qur-aan > Aayah Na Mafunzo.

 

 

Basi hizo hazitamzidishia faida pekee, bali atazidisha ilimu yake ya ufahamu wa Qur-aan kwa kina, na atapata ladha, raghba (utashi), ilhamu na mapenzi ya Qur-aan.

 

 

Tumetegemea zaidi katika kuikamilisha kazi hii Tafsiyr zifuatazo:

 

 

تفسير القرآن العظيم للإمام الحافظ ابن كثير

Tafsiyr Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym ya Al-Haafidhw ‘Imaad Ad-Diyn Abi Al-Fidaa Ismaa’iyl bin Kathiyr. Au umaarufu wake تفسير ابن كثير Tafsiyr Ibn Kathiyr.

 

 

تيسير الكريم الرحمن في تفسير كلام المنان

Taysiyr Al-Kariym Ar-Rahmaan Fiy Tafsiyr Kalaam Al-Manaan ya Al-‘Allaamah Ash-Shaykh ‘Abdur-Rahmaan bin Naaswir As-Sa’diy. Au umaarufu wake kama تفسير السعدي Tafsiyr As-Sa’diy.

 

 

التفسير الميسر - نخبة من العلماء

At-Tafsiyr Al-Muyassar – Nukhbat Minal ‘Ulamaa

 

 

Na Tarjama ya Kiingereza:

 

Interpretation of The Meanings of The Noble Quran in The English Language (A Summarized Version of At-Tabari, Al-Qurtubi and Ibn Kathir with Comments from Sahih Al-Bukhari) Dr. Muhammad Taqi-ud-Diyn Al-Hilaaliy, Dr Muhammad Muhsin Khan.

 

 

Mwisho tunamshukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kutuwafikisha kuweza kuikamilisha kazi hii tukufu, kazi ambayo ni jukumu kubwa mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) wala hatusemi kuwa Tarjama hii itakuwa haina kasoro, kwani hakuna mkamilifu isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

Tunawaomba ndugu zetu watuarifu kwa kosa lolote lile watakaloligundua au kasoro yoyote ile watakayoiona kwa kuwasiliana nasi kupitiwa webmaster@alhidaaya.com.

 

 

Tunamuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Atughufurie kwa makosa yetu na Aijaalie kazi hii iwe ni kwa ajili ya kuzipata Radhi Zake Pekee na Atutakabalie.

 

 

Na Allaah Ni Mjuzi Zaidi  

 

الحمد لله رب العالمين وصلى الله على محمد وعلى آله واصحابه وسلم

 

 

Imeandaliwa Na:  Alhidaaya.com

 

 

 

[1] Fusw-Swilat (41:42).

 

[2] Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

قُل لَّئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَن يَأْتُوا بِمِثْلِ هَـٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا ﴿٨٨

“Sema: Ikiwa watajumuika wanaadamu na majini ili walete mfano wa hii Qur-aan, hawatoweza kuleta mfano wake na japokuwa watasaidiana wao kwa wao.” [Al-Israa (17:88)]

 

[3] Ibraahiym (14:4).

 

[4] Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّهُمْ يَقُولُونَ إِنَّمَا يُعَلِّمُهُ بَشَرٌ ۗ لِّسَانُ الَّذِي يُلْحِدُونَ إِلَيْهِ أَعْجَمِيٌّ وَهَـٰذَا لِسَانٌ عَرَبِيٌّ مُّبِينٌ ﴿١٠٣﴾

“Na kwa yakini Tunajua kwamba wao wanasema: Hakika hapana isipokuwa mtu anamfundisha (Muhammadصلى الله عليه وآله وسلم  Qur-aan). Lugha wanayomnasibishia nayo ni ya kigeni, na hii ni lugha ya Kiarabu bayana.” [An-Nahl (16:103)]

 

[5] Salaf:

 

Maana yake kilugha ni kilichopita, kilichotangulia.

Na wanaokusudiwa kuwa ni Salafus-Swaalih ni Wema Waliotangulia. Nao ni  Waumini wa  karne ya kwanza ambao ni  Swahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)    katika Muhaajirina na Answaar kama Anavyosema Allaah (عزّ وجلّ):

 

 وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِى تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٠٠﴾

“Na wale waliotangulia awali (katika Uislamu) miongoni mwa Muhajirina na Answaar na wale waliowafuata kwa ihsaan, Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia Jannaat zipitazo chini yake mito, wadumu humo abadi. Huko ndiko kufuzu kukubwa kabisa.” [At-Tawbah (9:100)] Rejea pia Al-Hashr (59:8-10).  

 

Kisha wale waliokuja baada yao na wakajifunza kwao miongoni mwa Taabi’iyn na Atbaa’ At-Taabi’iyn, halafu pia waliokuja baada yao katika karne iliyo bora kabisa aliyosema Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمَ): “Wabora wenu zaidi ni wa karne yangu, kisha wale wanaowafuatia (Taabi’iyna), kisha wale wanaowafuatia hao (Atbaa’ Taabi’iyn).” [Al-Bukhaari - Yamenukuliwa kutoka Manhaj As-Salaf Asw-Swaalih Wa Haajatul-Ummati Ilayhi, Tovuti Rasmi ya Ma’aaliy Shaykh Ad-Duktuwr Swaalih Bin Fawzaan Bin ‘Abdillaah Al-Fawzaan]

 

Kisha wengineo ambao wamewafuata hao wote katika Manhaj ya Salaf kwa kufuata mafundisho ya Kitabu na Sunnah, kuyalingania kwa watu, na kuyafanyia kazi mpaka Siku ya Qiyaamah. Na kwa mwenendo huu, wanakuwa ni Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah.”

 

[6] Taabi’iyn: Ni Waislamu waliokuja baada ya zama za Unabii na hawakuwahi kukutana na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمَ), bali walikutana na Swahaba wake wakasuhubiana nao. Miongoni mwa hao ni: Hasan Al-Baswriy, Qtaadah, ‘Urwah bin Az-Zubayr, Sa’iyd bin Al-Musayyib, Mujaahid bin Jabar, Sa’iyd bin Jubayr, Naafi’ (Mtumwa aliyeachwa huru na Ibn ‘Umar رَضِيَ اللهُ عَنهُمَا),  na ‘Ikrimah (Mtumwa aliyeachwa huru na Ibn ‘Abbaas رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا). 

 

[7] Atbaa' Taabi’iyn: Ni Waislamu ambao hawakuwahi kukutana na Swahaba wa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمَ), bali walikutana na Taabi’iyn na wakasuhubiana nao. Miongoni mwa hao ni: Maalik, Abu Haniyfah (ingawa baadhi ya Wanachuoni wanasema ni Taabiy' kwa sababu alikutana na Swahaba wa mwisho mwisho), Ash-Shaafi’iy, Ahmad bin Hanbal,  Sufyaan Ath-Thawriy, Sufyaan bin ‘Uyaynah, Ibn ‘Abiy Laylaa, Rabiy’ah, Abu ‘Abdirrahmaan Al-Awzaa’iy, Ibn Hurmuz, Al-Hasan Ibn Swaalih, ‘Abdullaah Ibn al-Hasan, na Ibn Shubrumah.

 

Kisha baada ya hao wakaja Taabiy' Atbaa' Taabi'iyn, na katika hao ni Imaam wa Hadiyth ambao ni: Al-Bukhaariy,  Muslim Abu Daawuwd At-Tirmidhiy An-Nasaay, Ibn Maajah.

 

[8] Tazama Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr - Ibn Taymiyyah.

 

[9] Al-An’aam (6:105).

 

[10] Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

إِنَّ عَلَيْنَا جَمْعَهُ وَقُرْآنَهُ ﴿١٧﴾ فَإِذَا قَرَأْنَاهُ فَاتَّبِعْ قُرْآنَهُ ﴿١٨﴾ ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا بَيَانَهُ ﴿١٩﴾

“Hakika ni juu Yetu Kuikusanya na Kukuwezesha kuisoma kwake. Basi Tunapoisoma (kupitia Jibriyl), fuata kusomwa kwake. Kisha ni juu Yetu Kuibainisha (kwako).” [Al-Qiyaamah (75:17-19)]

 

[11] Al-An’aam (6:59).

 

[12] Luqmaan (31:34).

 

[13] Al-An‘aam (6:82).

 

[14] Luqmaan (31:13).

 

[15] Sunnah:

 

Ni kila kilichonasibishwa kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kauli au kitendo au yale aliyoyakubali au sifa za kimaumbile au tabia au mwenendo.

 

[16]Hakika kila kile alichohukumu kwacho Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ni katika yale aliyoyaelewa (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na Qur-aan kama alivyosema Imaam Ash-Shaafi’y. Taz. Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr. Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

إِنَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِتَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ بِمَا أَرَاكَ اللَّـهُ ۚ وَلَا تَكُن لِّلْخَائِنِينَ خَصِيمًا ﴿١٠٥﴾

“Hakika Sisi Tumekuteremshia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Kitabu kwa haki ili uhukumu baina ya watu kwa Aliyokuonyesha Allaah. Wala usiwe mtetezi kwa makhaini.” [An Nisaa (4:105)] 

 

Pia Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

وَمَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ إِلَّا لِتُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي اخْتَلَفُوا فِيهِ ۙ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٦٤﴾

“Na Hatukukuteremshia Kitabu (Qur-aan) isipokuwa uwabainishie yale waliyokhitilafiana, na pia ni Mwongozo na Rahmah kwa watu wanaoamini.” [An Nahl (16:64)]

 

[17] An-Nahl (16:44).  Kadhalika Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا بَيَانَهُ ﴿١٩

“Kisha ni juu Yetu kuibainisha (kwako).” [Al-Qiyaamah (75:19)] inawarudi kwa uwazi kabisa wale wenye kudai kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakubainisha maana ya Majina na Sifa za Allaah, na kwa kauli yao hii, ima wanakusudia kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa hajui maana ya Majina na Sifa za Allaah, au Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alificha kile alichokifahamu. Taz. Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr.

 

[18] Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: 

 

 أَلَا إِنِّي أُوتِيتُ الْقُرْآنَ وَمِثْلَهُ، أَلَا يُوشِكُ رَجُلٌ يَنْثَنِي شَبْعَانًا عَلَى أَرِيكَتِهِ يَقُولُ: "عَلَيْكُمْ بِالْقُرْآنِ فَمَا وَجَدْتُمْ فِيهِ مِنْ حَلَال فَأَحِلُّوهُ وَمَا وَجَدْتُمْ فِيهِ مِنْ حَرَامٍ فَحَرِّمُوهُ...  رواه أبو داود والترمذي والحاكم وصححه وأحمد بسند صحيح

“Tanabahi! Hakika nimepewa Qur-aan na inayofanana nayo (Sunnah) Tanabahi! Utafika wakati mtu aliyeshiba mno ataegemea kwenye kochi na kusema: “Shikamaneni na Qur-aan, mtakayokuta humo ya halali halalisheni, na mtakayokuta ya haramu haramisheni.” [Imepokewa na Abu Daawuwd, na At-Tirmidhiy, na Al-Haakim na ameisahihisha Ahmad kwa isnaad Swahiyh]

 

[19] Al-Kawthar (108:1).

 

[20] Al-Bukhaariy katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, At-Tirmidhiy katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan.

 

[21] Yuwnus (10:26).

 

[22] Ahmad katika Musnad, Kumi waliobashiriwa Jannah, Ukamilisho wa Musnad ya Kuufiyyiyn; na At-Tirmidhiy, katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, na Riwaaya nyenginezo.  

 

[23]Ni Tafsiyr yenye kutegemea yaliyo sahihi katika yaliyopokelewa kulingana na mpangilio huu: Tafsiyr ya Qur-aan kwa Qur-aan, Tafsiyr ya Qur-aan kwa Sunnah, Tafsiyr ya Qur-aan kwa kauli za Swahaba (رضي الله عنهم), Tafsiyr ya Qur-aan kwa kauli za Taabi’iyn kwa kuwa wao walichukua Tafsiyr zao kutokana na Swahaba (رضي الله عنهم). Vitabu vinavyotajika katika fani hii ya Tafsiyr ni kama:

 

i. Jaami’ul Bayaan Fiy Tafsiyril Qur-aan ya Ibn Jariyr Atw-Twabariy.

ii. Tafsiyrul Qur-aanil ‘Adhwiym ya Ibn Kathiyr.

iii. Fat-hul Qadiyr ya Ash-Shawkaaniy.

 

[24] Utangulizi wa Tafsiyr Ibn Kathiyr; vyanzo vya Tafsiyr.

 

[25]Amesema Abuu ‘Abdir-Rahmaan As-Sulamy: “Wametuhadithia wale waliokuwa wakitusomesha Qur-aan kama ‘Uthmaan bin ‘Affaan (رضي الله عنه)   na ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه)  na wengineo kuwa wao walikuwa pale wanapojifunza kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) Aayah kumi huwa hawaongezi nyingine mpaka pale watakapojifunza (na kutekeleza) yale yaliyomo ya ilimu na amali katika hizo Aayah kumi walizojifunza, basi wakasema: Tulijifunza Qur-aan na ilimu na amali kwa pamoja, na kwa sababu hiyo ndio walikuwa wakichukua muda kati kuhifadhi Suwrah.” Taz. Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr.  

 

[26]Aliyepokelewa akisema: “Naapa kwa Yule Ambaye hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakuna katika Kitabu cha Allaah Suwrah isipokuwa mimi najua ilivyoteremka, na hakuna Aayah isipokuwa najua imeteremshwa kwa ajili gani (sababu) na lau ningelimjua yeyote kuwa yeye ni mjuzi zaidi yangu kwa Kitabu cha Allaah, na ngamia anaweza kufika kwake, basi ningepanda kwenda kwake.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Fadhila za Swahaba, mlango wa fadhila za ‘Abdullaah bin Mas’uwd na mama yake (رضي الله عنهما)]

 

[27]Ibn ‘Abbaas aliyetambulikana kama ni ‘Tur-jumanil Qur-aan’ na aliyeombewa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):

((اللَّهُمَّ عَلِّمْهُ الْحِكْمَةَ وَتَأْوِيلَ الْكِتَابِ))

“Ee Allaah, Mfunze Hikmah na Ta-awiyl (ufasiri, utambuzi) wa Kitabu (Qur-aan).” [Imepokelewa na At-Tirmidhiyy, katika Kitabu cha Ad-Da’waat, milango ya Manaaqiyb; na Sunan Ibn Maajah, katika Kitabu cha Ibn Maajah, milango ya fadhila za Swahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)]

 

[28]Ni kila kilichotegemezwa kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kauli au kitendo au kuthibitisha jambo au sifa katika tabia zake au umbo lake.

 

[29] Israaiyliyyaat: Ni khabari, visa, simulizi zitokazo kwa Mayahudi katika Vitabu vya Tafsiyr, Taariykh n.k.

 

[30]An-Nisaa (4:43).

 

[31]Tafsiyr Ibn Kathiyr.

 

[32] Luqmaan (31:6). Tanbih: Kinachoruhusiwa ni dufu na sio ala nyenginezo za muziki.

 

[33] Atw-Twabariy (20:127).

 

[34] Al-Baqarah (2:158).

 

[35] Al-Baqarah (2:158).

 

[36] Tazama Ibn Taymiyyah, Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl at-Tafsiyr.

 

[37] Kama vile Mujaahid, Sa’iyd bin Jubayr, ‘Ikrimah, Twaawuws, ‘Atwaa, Zayd bin Aslam, Abul ‘Aaliyah na Muhammad bin Ka’b, ‘Alqamah bin Qays, Masruwq, ‘Aamir Ash-Sha’biy na Hasan Al-Baswriy na Qataadah.

 

[38] Imaam At-Tirmidhiy amesema: “Ama yale yaliyopokelewa kutokana na Mujaahid na Qataadah na wengineo miongoni mwa Ahlul-‘Ilmi kwamba walifasiri Qur-aan,  basi hakuna haja ya kuwadhania kuwa walifasiri Qur-aan bila ya ilimu –kwa rai zao- au kutokana na nafsi zao, na kumekwishapokewa kutokana na wao yale tuliyoyasema yenye kuthibitisha kwamba wao hawakuifasiri Qur-aan kutokana na nafsi zao bila ya ilimu kama ilivyothibiti kutokana na Al-Hassan bin Al-Mahdiy Al-Baswriyy amesema: Ametupa khabari ‘Abdur-Razzaaq kutokana na Ma’mar kutoka kwa Qataadah amesema: “Katika Qur-aan hakuna Aayah yoyote ile isipokuwa nimesikia kitu kuhusiana nayo.” [At-Tirmidhiyy katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, mlango wa katika yale yaliyokuja kwa yule anayefasiri Qur-aan kwa rai yake]

 

[39] Kutoka kwa Ibn Mas’uwd(رضي الله عنه) : Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

((خَيْرُ النَّاسِ قَرْنِي، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ)) صحيح البخاري ومسلم

“Watu bora kabisa ni karne yangu, kisha wanaowafuatia, kisha wanaowafuatia.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu Al-Manaaqib, mlango wa Fadhila za Swahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), Muslim Kitabu cha Fadhila za Swahaba, mlango wa Fadhila za Swahaba (رضي الله عنهم)]

 

[40] Al-Baqarah (2:116).

 

[41] Tafsiyr Ibn Kathiyr.

 

[42] Al-Baqarah (2:258).

 

[43] Tafsiyr Ibn Kathiyr.

 

[44] Tazama Ibn Taymiyyah, Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr.

 

[45] Tarjama Hii Ziko Mbili: Ya Mtandaoni Na Iliyochapishwa:

 

(i) Tarjama Iliyoko Mtandaoni Alhidaaya.com:

 

Tarjama hii imetoa maelezo na fafanuzi kwa baadhi ya Aayah kwa faida ya msomaji. Maelezo hayo yanahusiana na mas-ala ya ‘Aqiydah kama Al-Istiwaa (Uwepo wa Allaah (سبحانه وتعالى) juu ya ‘Arsh). Pia kuthibitisha Sifa Zake kama Alivyojithibitishia Mwenyewe na kadhalika. Vile vile, imefafanua baadhi ya maneno ya Kiarabu au ya Kiswahili ambayo hayafahamiki kiwepesi katika jamii. Isitoshe, pametajwa ndani yake rejea za Aayah zilizo katika Suwrah tofauti ambazo zinagusia maudhui moja, ili msomaji aweze kuzipata kirahisi pale zilipo, na kulifahamu suala kwa ujumla wake. Na hatimaye, zimetajwa rejea za mtandaoni Alhidaaya.com za maudhui kwenye makala na vitabu vya maudhui husika, zikiwemo rejea za Asbaabun-Nuzuwl (Sababu Za Kuteremshwa) Aayah au Suwrah., ambazo zitampa msomaji uelewa kamili na mzuri wa Aayah au Suwrah husika ili msomaji ajinufaishe zaidi na aweze kuongeza ilimu yake.

 

(ii) Tarjama Iliyochapishwa:   

 

Tarjama hii iliyochapishwa kwenye karatasi haikuwekewa maelezo au fafanuzi kuhusu baadhi ya Aayaat.  Sababu, ni kuzipa nafasi hati ziwe kubwa za wazi zinazosomeka kirahisi, na pia upatikane mjeledi mmoja tu wa Tarjama ili msomaji aweze kuutumia kiwepesi. 

 

[46] Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١١﴾

“Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote.” [Ash-Shuwraa (42:11)]

 

[47] Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: Hakuna yeyote anayeitwa Ar-Rahmaan isipokuwa Allaah (تبارك وتعالى) na Jina Lake linatukuzwa [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[48] Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym Nukhbah Min Al-‘Ulamaa – Markaz Tafsiyr Lid-Diraasaat Al-Qur-aaniyyah. Na Maqaaswid nyenginezo.

 

مركز تفسير للدراسات القرآنية

 

 

Share