05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Tano Na La Sita

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

Kivazi Cha Mwanamke 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

005-Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Tano Na La Sita:

 

Sharti la tano:

 

Nguo isiwe imefukizwa au imepuliziwa manukato.  Abu Muwsaa Al-Ash-‘ariyy amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"أَيُّمَا امْرَأَةٍ اسْتَعْطَرَتْ فَمَرَّتْ عَلَى قَوْمٍ لِيَجِدُوا مِنْ رِيحِهَا فَهِيَ زَانِيَةٌ"

 

“Mwanamke yeyote aliyejifukiza manukato, halafu akapita karibu na wanaume ili waipate harufu yake, basi ni mzinifu”.  [An-Nasaaiy (2/283), Abu Daawuwd (4173), At-Tirmidhiy (2786) na wengineo kwa Sanad Hasan].

 

Sababu ya kukataza hilo iko wazi, nayo ni kuwa tabia hiyo inachochea na kuchemsha matamanio ya kimwili ya wanaume.  Na ‘Ulamaa wameingiza mambo mengine ndani ya hili na kuyafanya kuwa sawa nalo kama vile kuvaa vipambo vinavyoonekana, mavazi ya kuvutia, mapambo ya kifahari na kuchanganyika na wanaume.  [Fat-hul Baariy (2/279)].

 

Al-Haythamiy ameeleza kwenye “Az-Zawaajir” (2/37) kwamba mwanamke akitoka nyumbani kwake akiwa amejitia manukato na kujipamba, basi hilo ni katika madhambi makubwa, hata kama ametoka kwa ruksa ya mumewe.

 

Sharti la sita:

 

Nguo yake isifanane na nguo za kiume.  Ibn ‘Abbaas amesema:

 

"لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمُتَشَبِّهِينَ مِنَ الرِّجَالِ بالنِّسَاءِ، وَالْمُتَشَبِّهَاتِ من النِّسَاءِ  بِالرِّجَالِ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake, na wanawake wanaojifananisha na wanaume”.  [Al-Bukhaariy (5885), At-Tirmidhiy (2784), Abu Daawuwd (4097) na Ibn Maajah (1904)].

 

Maana ni kwamba haijuzu wanaume kujifananisha na wanawake katika mavazi na mapambo ambayo yanawahusu wanawake na kinyume chake.

 

Na Abu Hurayrah amesimulia: 

 

"لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الرَّجُلَ يَلْبَسُ لِبْسَةَ الْمَرْأَةِ وَالْمَرْأَةَ تَلْبَسُ لِبْسَةَ الرَّجُلِ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwanaume anayevaa mavazi ya kike, na mwanamke anayevaa mavazi ya kiume”.  [Abu Daawuwd (4098) na Hamad (2/325) kwa Sanad Swahiyh].

 

Faida:

 

Kidhibiti katika kukataza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kila jinsia kujifananisha na nyingine, hakirejei tu katika kile wanachojichagulia wanaume na wanawake, au wanavyovitamani na wanavyovizoea, bali kinarejea kwa kila kinachowafaa wanaume na kinachowafaa wanawake.  Kinachowafaa wanawake ni lazima kinasibiane na kile walichoamrishwa katika kujisitiri na kujifunika bila kuonekana yasiyofaa kuonekana na ajinabi.  Na kwa msingi huu, tutaona kwamba sharia ina makusudio mawili.  La kwanza ni kuweka tofauti kati ya mwanaume na mwanamke, na la pili ni kusitiriwa mwanamke, na yote mawili ni lazima yapatikane.

 

 

 

Share