06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Saba Na La Nane

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

 

Kivazi Cha Mwanamke 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

006- Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Saba Na La Nane:

 

Sharti la saba:

 

Isifanane na nguo za wanawake wa kikafiri.  Hii ni kwa mujibu wa yaliyopitishwa na sharia ya Kiislamu kwamba haifai kwa Waislamu -wanaume kwa wanawake- kujifananisha na makafiri, ni sawa katika ibada zao, au sikukuu zao, au mavazi yao yanayowahusu wao.  

 

Kuna matini nyingi zinazoelezea nukta hii.  Kwa yanayohusiana na nguo, ni Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amri aliyesema:

 

 

"رَأَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَىَّ ثَوْبَيْنِ مُعَصْفَرَيْنِ فَقَالَ‏: "‏إِنَّ هَذِهِ مِنْ ثِيَابِ الْكُفَّارِ فَلاَ تَلْبَسْهَا"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniona nimevaa nguo mbili za rangi ya zafarani.  Akaniambia:  Hakika hizi ni katika nguo za makafiri, usizivae”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2077)].

 

Mbali ya Hadiyth hii, ziko nyingine nyingi tele.  Na makusudio hapa ni kutaka ijulikane kuwa haifai kwa mwanamke wa Kiislamu avae nguo ifananayo na nguo za wanawake wa kikafiri, kwa kuwa kushirikiana katika jambo la dhahiri, kunazalisha mvaano na muundano kati ya wafananao, na hatima yake ni kukubaliana tabia na matendo, na hili kiuhalisia liko.  [Kwa maudhui hii, pitia kitabu cha “Iqtidhwaau As-Swiraat Al-Mustaqiym” cha Ibn Taymiyyah.  Kitabu hiki hakina mfano wake].

 

Sharti la nane:

 

Lisiwe ni vazi la umashuhuri (la kipekee tofauti na mengineyo).  Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar:

 

"مَنْ لَبِسَ ثَوْبَ شُهْرَةٍ فيٍ الدُّنْيَا أَلْبَسَهُ اللَّهُ ثَوْبَ مَذَلَّةٍ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، ثُمَّ أَلْهَبَ فِيْهِ نَارًا"

 

“Mwenye kuvaa nguo ya umashuhuri duniani, Allaah Atamvisha nguo ya udhalili Siku ya Qiyaamah, kisha Atamwashia ndani yake moto”.  [Abu Daawuwd (4029) na Ibn Maajah (3607) kwa Sanad Hasan Lighayrih].

 

Nguo ya umashuhuri ni nguo yoyote ambayo mtu anataka apate umashuhuri kwayo kwa watu, ni sawa ikiwa nguo yenyewe ni ya thamani kubwa anaivaa ili kujifaharisha nayo, au iwe ni ya thamani duni ili kuonyesha zuhd (kutoijali dunia) na riyaa.

 

 

 

Share