14-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Kivazi Cha Mwanamke Mbele Ya Wanawake Wenzake

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

Kivazi Cha Mwanamke 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

014- Kivazi Cha Mwanamke Mbele Ya Wanawake Wenzake

 

 

Allaah Mtukufu Anasema:

 

"وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ"

 

“Na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika.  Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wenzao (wa Kiislamu)”.  [An-Nuwr: 31]

 

Ibn  Kathiyr amesema (3/284):  Neno Lake “Au wanawake wenzao”, ina maana adhihirishe pambo lake pia kwa wanawake wenzake wa Kiislamu.

 

Na uchi wa mwanamke ambao ni lazima ausitiri kwa mwanamke mwenzake, ni uchi ule ule wa mwanaume kwa mwanaume mwenzake ambao ni kutoka kitovu hadi magoti.  [Al-Mughniy (6/562)].

 

Haijuzu mwanamke kuangalia sehemu ya kati ya kitovu na magoti ya mwanamke mwenzake kama wanavyofanya hivyo wanawake wengi wa Kiislamu.  Ibn Al-Jawziy amesema:  “Wanawake wengi wasiofahamu, hawajali kuachia wazi uchi wao au sehemu ya uchi mbele ya mama, au dada, au bint huku wakisema kwamba hawa ni watu wa karibu.  Basi na ajue kila mwanamke kwamba akifikisha miaka saba, haruhusiwi mama yake, wala dada yake wala binti yake kuangalia uchi wake”.  [Ahkaamun Nisaa cha Ibn Al-Jawziy (uk. 76)].

 

Ninasema:  “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا يَنْظُرُ الرَّجُلُ إِلَى عَوْرَةِ الرَّجُلِ وَلَا الْمَرْأَةُ إِلَى عَوْرَةِ الْمَرْأَةِ ، وَلَا يُفْضِي الرَّجُلُ إِلَى الرَّجُلِ فِي ثَوْبٍ وَاحِدٍ وَلَا تُفْضِي الْمَرْأَةُ إِلَى الْمَرْأَةِ فِي ثَوْبٍ وَاحِدٍ "

 

“Mwanaume haruhusiwi kuangalia uchi wa mwanaume mwenzake, wala  mwanamke kuangalia uchi wa mwanamke mwenzake.  Na mwanaume asigusane ngozi kwa ngozi na mwanaume mwenzake ndani ya nguo moja, na mwanamke pia asigusane ngozi kwa ngozi na mwanamke mwenzake ndani ya nguo moja”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (338), At-Tirmidhiy (2793) na Abu Daawuwd (4018)].

 

 

Share