17-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Kivazi Cha Mwanamke Kwa Wanaume Wasio Na Matamanio Ya Wanawake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

Kivazi Cha Mwanamke 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

017-Kivazi Cha Mwanamke Kwa Wanaume Wasio Na Matamanio Ya Wanawake:

 

Allaah Amesema:

 

"أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ"

 

“Au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume”.  [An-Nuwr: 31].

 

Hawa ni wale wasio na matamanio ya kingono kwa wanawake kutokana na utu uzima uliopevuka, au ukhanithi, au kufa kabisa nguvu za kiume.  Watu kama hawa wanaruhusika kumwangalia mwanamke kwa haja ya dharura tu ili kuepusha usumbufu, lakini ikiwa itagundulika kwamba khanithi kwa mfano anadadisi mambo ya akina mama na kuyaeleza kwa watu nje, basi huyo atazuiliwa kuingia kwa wanawake na kuwaangalia.

 

Ummu Salamah amesema:

 

"أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كَانَ عِنْدَهَا وَفِي الْبَيْتِ مُخَنَّثٌ ، فَقَالَ المُخَنَّثٌ لِعَبْدِ اللَّهِ بْنِ أَبِي أُمَيَّةَ أَخِي أُمِّ سَلَمَةَ: يَا عَبْدَ اللَّهِ إِنْ فَتَحَ اللَّهُ لَكُمْ غَدًا الطَّائِفَ فَإِنِّي أَدُلُّكَ عَلَى ابْنَةِ غَيْلَانَ فَإِنَّهَا تُقْبِلُ بِأَرْبَعٍ وَتُدْبِرُ بِثَمَانٍ ، فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: لَا يَدْخُلَنَّ هَذا عَلَيْكُم"

 

“Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa nyumbani  kwake na ndani ya nyumba yuko khanithi.  Khanithi yule akamwambia kaka wa Ummu Salamah ‘Abdullaah bin Abiy Umayyah:  Ee ‘Abdullaah!  Allaah Akiwafungulieni Twaif kesho mkaiteka, basi nitakupeleka umuone binti wa Ghaylaan. Akikuelekea, utaona mikunjano minne ya tumbo lake (kutokana na unene), na akikupa mgongo, utaona minane.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema hapo hapo:  Msimruhusu huyu kuingia tena hapa”.  [Al-Bukhaariy (5235) na Muslim (2180)].

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomsikia anamsifia binti wa Ghaylaan, alijua kwamba huyo anafahamu na kufuatilia mambo ya wanawake, na moja kwa moja akaamuru asiruhusiwe kuingia kwake.

 

Angalizo:

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wamekubaliana kwamba mwanaume aliyehasiwa au aliyekatwa uume, ni haramu kwao kuwaangalia wanawake, kwa kuwa kiungo ingawa hakifanyi kazi au hakipo, lakini matamanio ya wanaume yanabakia kwenye nyoyo zao.  [Angalia Al-Mabsuwtw (10/158) na Al-Majmuw’u (16/140)].

 

 

 

 

Share