19-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Kivazi Cha Mwanamke Na Mapambo Yake Kwa Mumewe

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

Kivazi Cha Mwanamke 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

019-Kivazi Cha Mwanamke Na Mapambo Yake Kwa Mumewe:

 

 

Kauli ya Jumhuwr inasema:  “Mke na mume wana haki ya kuangaliana wenyewe kwa wenyewe mwili mzima bila ukakasi wowote, ni sawa iwe kwa matamanio au bila matamanio, iwe kwenye sehemu nyeti au penginepo popote”.  Baadhi ya yanayoashiria hili ni:

 

1-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ • إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِين"َ

 

“Na ambao wanahifadhi tupu zao • Isipokuwa kwa wake zao, au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao si wenye kulaumiwa”.  [Al-Ma’aarij: 29, 30].

 

Aayah hii inaonyesha kwamba yaliyo juu ya kuangalia ambayo ni kugusa na kuvaana kimwili, ni halali kwao.  Na kwa vile mume ameruhusiwa kustarehe na utupu wa mkewe, basi kwa ustahikivu zaidi, anaruhusiwa kuuangalia na kuugusa kama sehemu nyinginezo zote za mwili.  [Al-Mabsutw (10/148) na Al-Muhallaa (10/33)].

 

2-  ‘Aaishah amesema:

 

"كُنْتُ أَغْتَسِلُ أَنَا وَالنَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مِنْ إِنَاءٍ وَاحِدٍ مِنْ قَدَحٍ يُقَالُ لَهُ الْفَرَقُ‏"

 

“Nilikuwa mimi naoga pamoja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye chombo kimoja kiitwacho “Al-Faraq”.  [Al-Bukhaariy (250) na Muslim (319)].   

 

Na hii ni dalili ya kujuzu mwanaume kuangalia uchi wa mkewe na mkewe kuangalia wake.  [Fat-hul Baariy (1/364)].

 

3-  Toka kwa Bahz bin Hakiym, toka kwa baba yake toka kwa babu yake, amesema:

 

"يَا رَسُولَ اللَّهِ ، عَوْرَاتُنَا مَا نَأْتِي مِنْهَا وَمَا نَذَرُ؟ قَالَ: ‏"‏احْفَظْ عَوْرَتَكَ إِلاَّ مِنْ زَوْجَتِكَ أَوْ مِمَّا مَلَكَتْ يَمِينُكَ‏" 

 

“Ee Rasuli wa Allaah!  Kuhusu nyuchi zetu, ni zipi ambazo tunaweza kuzifunika, na ni zipi ambazo tunaweza kuziachia?  Akasema:  Uhifadhi uchi wako isipokuwa kwa mkewe au watumwa wako”.  [Hadiyth Hasan.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (7/40), At-Tirmidhiy (2769) na Ibn Maajah (1920)].

 

Kiufupi, hakuna mpaka wa uchi kati ya mke na mume.  Mwanamke anaruhusiwa kuvaa chochote atakacho kwa mumewe, kuvua chochote atakacho, na kujipamba kwa mumewe kwa aina zote za mapambo yanayoruhusiwa kisharia ambayo yatakuja kuzungumziwa milango ya mbeleni In Shaa Allaah. 

 

 

 

 

 

Share