086-Atw-Twaariq: Utangulizi Wa Suwrah

 

086-Atw-Twaariq: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 17

 

Jina La Suwrah: Atw-Twaariq

 

Suwrah imeitwa Atw-Twaariq (Kinachokuja Na Kugonga Usiku), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na kwamba Anawafahamu wanaadam wote, na Yeye Ndiye Atakayewarejesha (Kwake Siku ya Qiyaamah). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kusimamisha dalili ya Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na kuthibitisha kwamba Qur-aan inatoka Kwake na Desturi ya Allaah Kulipiza vitimbi vya makafiri na kuwaangamiza.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia mbingu na nyota inayogonga inapotoka usiku. Ikafuatia jambo linalohakikishwa kiapo, kwamba kila mtu amewakilishwa Malaika mwenye kuchunguza na kusajili amali zake njema na ovu ili ahesabiwe Siku ya Qiyaamah.

 

2-Wamekumbushwa wanaokanusha kufufuliwa wajitazame na wazingatie wameumbwa na nini, ili wajue kwamba Aliyewaumba kwa manii, ni Mweza wa kuwarudisha katika umbo lao mara ya pili, Siku ya Qiyaamah, Siku ambayo siri zote zitafichuliwa wazi.

 

3-Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaapia kwa mbingu yenye mvua ya kurudiarudia kunyesha. Na kwa ardhi yenye mpasuko za kufanya mimea ichipuke. Kisha Allaah Akahakikisha jambo Analoapia ambalo ni kuthitibisha kuwa Qur-aan ni kauli zinazopambanua haki na baatwil, na kwamba wala si upuuzi.  

 

4-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwatishia washirikina wanaofanya vitimbi vya kupinga haqq (haki) na kutilia nguvu baatwil, kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Analipiza vitimbi vyao, basi Anamliwaza Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) awape muhula washirikina, kwani atakuja kuona adhabu na maangamizi watakayoyapata. 

 

Faida:

 

عَنْ جَابِرِ بْنِ سَمُرَةَ، أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ يَقْرَأُ فِي الظُّهْرِ وَالْعَصْرِ بِالسَّمَاءِ ذَاتِ الْبُرُوجِ وَالسَّمَاءِ وَالطَّارِقِ وَنَحْوِهِمَا ‏.‏

Amesimulia Jaabir Bin Samrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma katika Swalaah ya Adhuhuri na Alasiri:

وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الْبُرُوجِ ﴿١﴾

Naapa kwa mbingu yenye buruji.” [Al-Buruwj (85)]

 

Na

وَالسَّمَاءِ وَالطَّارِقِ ﴿١﴾

“Naapa kwa mbingu na kinachogonga kinapotoka usiku.” [Atw-Twaariq (86)]

 

Na Suwrah zinazofanana kama hizo. [Hadiyth Hasan Swahiyh - At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Swahiyh Abiy Daawuwd (805)]   

 

 

 

Share