087-Al-A’laa: Utangulizi Wa Suwrah

 

087-Al-A’laa: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 19

 

Jina La Suwrah: Al-A’laa

 

Suwrah imeitwa Al-A’laa (Mwenye ‘Uluwa Aliyetukuka), na yanayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth zilizonukuliwa kwenye Fadhila, na kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuikumbusha nafsi (hali ya) maisha ya Aakhirah na kule kukatika kwake na kila jambo la kidunia. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kudhihirisha wingi wa Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) ambazo haiwezekani kuziorodhesha hesabuni.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kutakasa Jina la Allaah Mwenye ‘Uluwa na ‘Uadhwama, Yuko juu kabisa ya viumbe Vyake na kila kitu, Yu Pekee Hana mshirika na Ametakasika na kila sifa pungufu (سبحانه وتعالى).  

 

2-Imethibitishwa Tawhiyd ya Allaah ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji, Uendeshaji, Uongozaji na kadhaalika) .

 

3-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amebashiriwa bishara kubwa kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), kwamba pindi Atakapoteremshiwa Qur-aan na akafanywa aisome, basi Allaah (سبحانه وتعالى) Ataihifadhisha moyoni mwake ili ithibitike vizuri, basi hatoweza kusahau chochote. Na amebashiriwa pia kusahilishiwa mambo yake yote, yakiwemo majukumu ya Urasuli. Na pia amebashiriwa kusahilishiwa Sharia za Dini hii Tukufu.

 

4-Allaah (سبحانه وتعالى) Anamuamrisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) awakumbushe watu mawaidha. Na kwamba aendelee kuwakumbusha madhali watayasikiliza na kunufaika nayo. Basi hawa ni Waumini wenye kumtii na kumcha Allaah. Na hawa ndio watakaojaaliwa kuhidika, na ndio watakaofaulu kutokana na kuzitakasa nafsi zao. Na kuna watakapoupinga kwa kutokumkhofu Allaah. Basi hawa ni wapotofu, na hatima yao itakuwa ni kuingizwa motoni.

 

5-Wamekemewa watu wanaokhiyari na kupendelea maisha ya dunia kutokana na starehe zake. Lakini starehe za dunia hazidumu milele, bali ni za muda mfupi tu. Ama maisha ya Aakhirah ndiyo yenye starehe na neema tele. Na maisha haya, ndio yenye kudumu milele.   

 

5-Suwrah imekhitimishwa kwa kukumbushwa kwamba waliyokumbushwa katika Suwrah hii tukufu, yametajwa pia katika Suhuf (Maandiko Matukufu) zilizotangulia kabla ya Qur-aan na Suhuf za Ibraahiym na Muwsaa (عليهما السلام)

 

Fadhila Za Suwrah:

 

1-Ni Sunnah Kuisoma Suwrah Hii Katika Swalaah Ya Ijumaa Na ‘Iyd Mbili:

 

عَن النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ، قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الْجُمُعَةِ وَالْعِيدِ بِـ ‏{سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى}‏ وَ ‏{هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْغَاشِيَةِ}‏ وَإِذَا اجْتَمَعَ الْجُمُعَةُ وَالْعِيدُ فِي يَوْمٍ قَرَأَ بِهِمَا ‏.‏

Amesimulia Nu’maan Bin Bashiyr (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma  

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى

[Al-A’laa (87)]

 

Na

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْغَاشِيَةِ

 

[Al-Ghaashiyah (88)]

 

Katika Rakaa ya kwanza ya Swalaah ya Ijuma. Na inapojumuika Ijumaa na ‘Iyd katika siku moja, alizisoma pia (Suwrah hizo). [Muslim, An- Nasaaiy, Abuu Daawuwd]

 

2-Ni Sunnah Kuisoma Katika Swalaah Ya Witr:

 

عَنْ سَعِيدِ بْنِ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ أَبْزَى، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ أُبَىِّ بْنِ كَعْبٍ، قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الرَّكْعَةِ الأُولَى مِنَ الْوَتْرِ بِـ ‏{ سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى }‏ وَفِي الثَّانِيَةِ بِـ ‏{ قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ }‏ وَفِي الثَّالِثَةِ بِـ ‏{ قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ}

Amesimulia Ubayy Bin Ka’ba (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma katika Rakaah ya kwanza ya Swalaah ya Witr:

 

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى

[Al-A’laa (87)]

 

Na katika ya pili:

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ

[Al-Kaafiruwn (109)]

 

Na katika ya tatu:

قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ

[Al-Ikhlaasw (112)]

 

[At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh An-Nasaaiy]

 

 

Share