14-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu: Vipodozi Na Poda Za Kujipambia Mwili

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ 

Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo

 

 

الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ

Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu

 

Alhidaaya.com

 

 

14-Vipodozi Na Poda Za Kujipambia Mwili:

 

Mwanamke anaruhusiwa kutumia aina yoyote ya vipodozi aipendayo kwa ajili ya kujipamba kwa mumewe.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"....وَخَيْرَ طِيبِ النِّسَاءِ مَا ظَهَرَ لَوْنُهُ وَخَفِيَ رِيحُهُ"

 

“… na mafuta mazuri zaidi kwa mwanamke ni yale yenye rangi inayoonekana, yasiyo na harufu”.  [At-Tirmidhiy (2788) na Abu Daawuwd (2174).  Ni Hadiyth Hasan Lighayrih]

 

Kati ya linalotilia nguvu hili, ni Hadiyth ya Anas:

 

 "أَنَّ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ عَوْفٍ جَاءَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  وَبِهِ أَثَرُ صُفْرَةٍ ، فَسَأَلَهُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  فَأَخْبَرَهُ أَنَّهُ تَزَوَّجَ امْرَأَةً مِنَ الأَنْصَارِ"

 

“Kwamba ‘Abdurrahmaan bin ‘Awf alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na athari ya rangi njano.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza imekuwaje?  Akamweleza kwamba ameowa mwanamke wa Kianswaar”.  [Swahiyhul Bukhaariy (5153)]

 

Unjano huo ulimganda toka kwa mkewe kwa mujibu wa kauli ya An-Nawawiy.

 

Haya yote ni dalili ya kujuzu mwanamke kujipaka vipodozi na poda za kujipamba mwili wake.

 

Kiufupi, ni ruksa kwa mwanamke kutumia vipodozi madhali tu havionyeshi ila kwa wale tu alioruhusiwa kufanya hivyo, wala isiwe kwa ajili ya kudanganya au kuficha kitu, na wala visisababishe madhara kwa ngozi yake.  Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.  [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (4/418).  Na hivi ndivyo walivyofutu Bin Baaz na Bin ‘Uthaymiyn (Rahimahumal Laah]

 

Angalizo:

 

Baadhi ya madaktari wanasema kwamba vipodozi vina madhara kwa ngozi.  Ikiwa hili litathibiti, basi haitoruhusiwa kuvitumia.  Dk. Mustwafa Husayn ‘Abdul Maqsoud mbobezi wa magonjwa ya ngozi na uzazi katika Chuo Kikuu cha Tanta nchini Misri amesema:

 

“Vipodozi vinavyotengenezwa hivi sasa vina madhara makubwa sana kwa ngozi kama ifuatavyo:

 

Kwanza:  Madhara ya vipodozi

 

1-  Husababisha ngozi kudumaa na kusinyaa, na hii hupelekea kuzeeka ngozi mapema.

 

2-  Husababisha ngozi kukauka na kupasuka.

 

3-  Husababisha ngozi kuvimba, kuwashwa na kupata ukurutu (eczema).

 

4-  Husababisha kubadilika rangi ya ngozi, ima kwa kuongezeka rangi yake na kutokeza mabaka meusi, au kwa kupungua rangi na kutokeza madoa meupe.

 

5-  Baadhi ya rangi za vipodozi hufyonza miale na kusababisha mwasho wa kimiale kwenye ngozi au kuota nywele nyingi usoni.

 

6-  Viambata vya vipodozi vinaweza kupelekea kubadilika muundo wa seli za ngozi, na hii inaweza kusababisha kansa.

 

7-  Krimu huziba vitundu vya kutolea jasho kwenye ngozi na husababisha kumea vipele na chunusi.

 

8-  Vipodozi husababisha chunusi kupwita vikali kwa walionazo na kuchelewesha kuondoka.

 

Pili:  Rangi ya mdomo (Lipstick)

 

1-  Husababisha midomo kukauka na kunyauka, na hatimaye huwasha vikali.

 

2-  Kutumia mara kwa mara husababisha ukurutu (eczima) na kuwashwa, na kunaweza kusababisha kansa kwenye midomo.

 

3-  Mada yenye kutoa rangi hunyonya miale ambayo hujikita kwenye midomo, na hii huongeza rangi na kusawidika midomo kuzungukia kinywa.  Haya ni malalamiko ya akina mama wengi wanaotumia rangi za mdomo.

 

4-  Ikichanganyika na chakula au kinywaji, inaweza kufyonza baadhi ya mada ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa kwa mwili.  [Jarida la Al-Wa-’ayul Islaamiyy la Kuwait toleo nambari 140, ukurasa 93]

 

Dk. Wajiyh Zaynul ‘Aabidiyna aliandika makala kwenye jarida la Al-Wa-‘ayu Al-Islaamiy akisema:

 

“Pambo la nywele kwa sasa kwa msichana ni kuzitia mada telezi ijulikanayo “spray” ili zisimame.  Mada hii inaweza kusababisha nywele kukatika na kunyonyoka, au inaweza kusababisha madhara kwa konea ya jicho ikiwa italigusa moja kwa moja au kwa namna nyingine.  Na huenda matibabu yake yakaendelea kwa miezi kadhaa.

 

Ama poda na vipodozi vya uso, hivi huleta lengelenge za uso na maambukizi kwenye ngozi.  Hali hii huifanya ngozi kuwa na mikunjano kunjano na kuzeeka haraka, na mikunjano hii huacha mstari mkubwa chini ya jicho.  Na msichana anapobaleghe baada ya miaka 20, anakuja kusumbuliwa mara kwa mara na mwasho kwenye vigubiko vya jicho (eyelid) kutokana na kope bandia, au mwasho kwenye vigubiko vya jicho kutokana na rangi zinazopakwa juu yake. 

 

Rangi nyekundu ya mdomo inaweza kusababisha uvimbe au kunyauka ngozi yake laini, kwa sababu rangi hii huondosha tabaka lenye kulinda mdomo.  Kadhalika, rangi za kucha husababisha wakati mwingine kucha kukatika, au kuvunjika, au kuharibika, au hata maradhi sugu.

 

Bila shaka mwanadamu kwa maumbile yake ni lazima apate himaya kutokana na viathiri vya nje anavyokabiliana navyo katika maisha yake ya hapa ardhini.  Na ngozi ndiyo mstari wa kwanza wa kinga, na kwa kiasi cha tunavyoichunga ndivyo ambavyo tunafaidika zaidi na nguvu yake ya ulinzi.  Lakini kwa masikitiko makubwa, ustaarabu wa kisasa unaiharibu nguvu hii ya ulinzi kwa utumiaji wa kupitiliza wa madawa ya kujiremba na viambata vyake”.

 

Naye Dk. Naadiyah ‘Abdul Hamiyd Swaaleh ambaye ni bingwa wa magonjwa ya macho anasema:

 

“Vipodozi vya jicho vina viambata vya kemikali kali zinazosababisha madhara kwa macho, kutoka kope, mwasho, majipu kwenye ngozi ya kufunika jicho pamoja na kutokeza vifuko vya duhuni kwenye ngozi hiyo na kukunjana pia.  Hatimaye macho huja kuonekana yamechoka, yamekauka, sambamba na kutokeza weusi pembezoni mwa ngozi ya kufunika jicho”.

 

Dk. Naadiyah anatahadharisha pia kupasiana vipodozi hivi kati ya mtu na mwingine.  Tabia hii inapelekea kuambukizana magonjwa ya macho kupitia kalamu na brashi. 

 

Na kwa upande mwingine, madaktari wanasema kwamba mada ambazo wanawake wanapaka kwenye kope zao za asili zina viambata vya chumvi za nickel, au mpira bandia.  Mada hizi husababisha mwasho kwenye ngozi ya jicho na kung’ooka kope.

 

Ama rangi wanazotumia akina mama kupaka pembezoni mwa jicho, madaktari wamefichua ukweli wake wa kitaaluma, nao ni:

 

1- Rangi nyeusi ni kaboni nyeusi na oksidi nyeusi ya chuma.

 

2- Rangi bluu ni “bruce” na kemikali buluu.

 

3-  Rangi kijani inatokana na "chromium oxide". 

 

4-  Rangi ya kahawia ni "iron oxide" iliyounguzwa.

 

5-  Rangi ya njano ni "iron oxide". 

 

Mada zote hizi ni kemikali, nazo husababisha madhara hatari kwa jicho na sehemu za pembezoni mwake.

 

Kadhalika, madaktari wameeleza kwamba kati ya michanganyiko yake ni mada zinazosababisha athari sugu ya sumu kama “chlorophyll hexate” na “pheniylenediamine”.  Athari hii hupelekea vidonda kwenye konea na maambukizi kwenye jicho na hatimaye kope hudondoka.

 

Ninasema:  “Ikiwa mambo ni hivi, basi utumiaji wa vipodozi hivi ni haramu.  Lakini ikithibiti kutokuwa na madhara yoyote, basi ni halali.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Angalizo:

 

Rangi za kucha hazina ubaya kuzitumia kama hazina madhara ya mada za kemikali.  Lakini tatizo lake ni kuwa zinazuia maji ya wudhuu kufika kwenye kucha.  Kama zitaondoshwa wakati wa kutawadha, basi hakuna ubaya.

 

Na hapa tunapenda kuwakumbusha akina mama kwamba ni muhimu kukata kucha zao, wasiziachie kurefuka kama wanavyofanya wasichana wengi.  Hili ni kinyume na Sunnah ya maumbile asili (fitwrah).

 

Vile vile, hairuhusiwi kuunganisha kucha na kucha nyingine bandia zilizo ndefu kuliko za asili.  Kufanya hivyo ni kubadili umbile la Allaah, kujifananisha na makafiri, na kwenda kinyume na umbile salama.

 

 

Share