15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu: Pambo La Madini

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ 

Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo

 

 

الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ

Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu

 

Alhidaaya.com

 

 

15-Pambo La Madini:

 

Mwanamke anaruhusiwa kujipamba kwa aina zote za dhahabu na fedha.  ‘Aliyy bin Abiy Twaalib amesema:

 

"أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَخَذَ حَرِيرًا فَجَعَلَهُ فِي يَمِينِهِ، وَأَخَذَ ذَهَبًا فَجَعَلَهُ فِي شِمَالِهِ، ثُمَّ قَالَ: إِنَّ هَذَيْنِ حَرَامٌ عَلَى ذُكُورِ أُمَّتِي"

 

“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichukua hariri akaiweka kuliani mwake, na akachukua dhahabu akaiweka kushotoni mwake, kisha akasema:  Hakika viwili hivi ni haramu kwa wanaume wa umati wangu”.  [Abu Daawuwd (4057), An-Nasaaiy (8/160) na Ibn Maajah (3595).  Ni Hadiyth Swahiyh]

 

Mwanamke anaruhusiwa kujipamba kwa bangili, hereni, pete, mkufu wa shingoni, kidani na kadhalika.

 

Toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr:

 

" أَنَّ امْرَأَةً أَتَتْ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَبِنْتٌ لَهَا، فِي يَدِ ابْنَتِهَا مَسَكَتَانِ غَلِيِظَتَانِ مِنْ ذَهَبٍ فَقَالَ لَهَا: ‏أَتُؤَدِّينَ زَكَاةَ هَذِه؟‏‏ قَالَتْ: لاَ.‏ قَالَ: ‏"‏أَيَسُرُّكِ أَنْ يُسَوِّرَكِ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ بِهِمَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ سِوَارَيْنِ مِنْ نَارٍ"

 

“Kwamba mwanamke mmoja alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na binti yake.  Binti huyu alikuwa amevaa bangili mbili nzito za dhahabu mkononi.  Akamuuliza:  Je, unazitolea hizi zaka?  Akasema hapana.  Akamwambia:  Je, uko tayari Allaah Akuvishe badala yake bangili mbili za moto Siku ya Qiyaamah?!”  [Abu Daawuwd (1563), At-Tirmidhiy (623) na An-Nasaaiy (5/38) kwa Sanad Hasan]

 

Katika tukio la Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwatolea wanawake mawaidha Siku ya ‘Iyd,  Ibn ‘Abbaas anahadithia kwamba Rasuli alikuwa na Bilaal na akawaamuru akina mama watoe swadaqah.  Kila mwanamke akaanza kutoa hereni na pete yake na kuitupia (kwenye kapu la swadaqah).  [Imetajwa nyuma mara kadhaa]

 

Na katika Hadiyth ya Twawbaan:

 

"فَانْتَزَعَتْ فَاطِمَةُ سِلْسِلَةً فِي عُنُقِهَا مِنْ ذَهَبٍ وَقَالَتْ: هَذِهِ أَهْدَاهَا إِلَىَّ أَبُو حَسَنٍ"

 

“Faatwimah akautoa mkufu wa dhahabu shingoni mwake na kusema:  Abul Hasan amenipa huu zawadi”.  [An-Nasaaiy (5140) na Ahmad (21892) kwa Sanad Swahiyh]

 

Mwanamke anaruhusiwa vilevile kuvaa vikuku nyumbani kwake kwa mumewe.  Haruhusiwi kuvionyesha kwa wasio maharimu wala kupiga chini miguu ili wanaume wajue kuwa amevivaa.  Na hii ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ"

 

“Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao”.  [An-Nuwr: 31]

 

Faida:

 

Mwanamke anaweza kuvaa pete kidole chochote apendacho, kinyume na mwanaume ambaye anakatazwa kuvaa kwenye kidole cha kati na cha shahada.

 

Katika Swahiyh Muslim (2078), ‘Aliyy amesema:

 

" نَهَانِي رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ أَتَخَتَّمَ فِي إِصْبَعِي هَذِهِ أَوْ هَذِهِ، فَأَوْمَأَ إِلَى الْوُسْطَى وَالَّتِي تَلِيهَا"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinikataza kuvaa pete katika kidole changu hiki au hiki.  Akaashiria cha kati na kinachofuatia  (cha shahada)”.  [Ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2078), At-Tirmidhiy (1786), An-Nasaaiy (5210) na Abu Daawuwd (4225)]

                                  

An-Nawawiy amenukuu ‘Ijmaa ya kwamba katazo hili linawahusu wanaume tu pasina wanawake ambao wanaruhusiwa kidole chochote kama ilivyotangulia.

 

Hakuna Neno Kuvaa Pete Ya Chuma:

 

Kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Swahaba aliyetaka kuoa na hakuwa na chochote cha kulipia mahari:

 

"الْتَمِسْ وَلَوْ خَاتَمًا مِنْ حَدِيدِ"

 

“Tafuta japokuwa pete ya chuma”.  [Bukhaariy na Muslim]

 

 

                                                               

Share