03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Baadhi Ya Faida Za Kuoa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

03-Baadhi Ya Faida Za Kuoa:

 

1-  Ni kutekeleza Amri ya Allaah Ta’aalaa.

 

2-  Ni kufuata Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Mitume waliotangulia.

 

3-  Kunavunja matamanio ya jimai na kuyainamisha chini macho.

 

4-  Kunalinda tupu na zinaa na kuwaheshimisha wanawake.

 

5-  Kunazuia kuenea zinaa na machafu kwa Waislamu.

 

6-  Kunaongeza idadi ya Waislamu ambao Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atajifaharisha kwa wingi wao kwa Manabii na umma zilizotangulia.

 

7-  Kwa jimai ya halali, mke na mume hulipwa thawabu na Allaah.

 

8-  Kunawakilisha jambo alilolipenda Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:

 

"حُبِّبَ إِلَىَّ مِنْ دُنْيَاكُمْ الطِّيبُ والنِّسَاءُ" ‏‏

 

“Nimependezeshwa katika dunia yenu mafuta mazuri na wanawake”.  [Imekharijiwa na An-Nasaaiy (7/61), Ahmad (3/285) na wengineo.  Kuna maneno kuhusiana na Sanad yake]

 

9-  Kunawezesha kupata watoto ambao watawafaa wazazi kwa du’aa baada ya kufariki.

 

10-  Kunapelekea kuingia Peponi kutokana na uombezi wa watoto.  Swahaba mmoja alimsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

"يُقَالُ لِلْوَلَدَانِ يَوْمَ القِيَامَةِ: ادْخُلُوا الجَنَّةَ، قَالَ: فَيَقُوْلُونَ: يا رَبّ حَتَّى يَدْخُلَ آبَاؤُنَا وأُمَّهَاتُنَا، قَالَ: فَيَأْتُوْنَ، قَالَ: فَيَقُولُ اللهُ عزَّ وجَلَّ: مَالِيْ أَرَاهُمْ مُحْبَنْطِئِيْنَ ادْخُلُوا الجَنَّةَ، قَالَ: فَيَقُوْلُونَ: يا رَبّ آبَاؤُنَا وأُمَّهَاتُنَا، قَالَ: فَيَقُولُ: ادْخُلُوا الجَنَّةَ أَنْتُمْ وآباؤُكُم"

 

“Watoto wataambiwa waingie Peponi Siku ya Qiyaamah lakini watasema:  Ee Rabbi wetu, mpaka waingie baba zetu na mama zetu.  Wazazi wao wataletwa, na Allaah Ta’aalaa Atasema:  Mbona nawaona wamevimba kwa hasira, ingieni Peponi.  Watasema:  Ee Rabbi wetu, baba zetu na mama zetu.  Allaah Atawaambia:  Ingieni Peponi nyinyi na wazazi wenu”.  [Hadiyth Hasan.  Imekharijiwa na Ahmad (4/105)]

 

11-  Kunapatikana kizazi cha Waumini watakaolinda nchi za Kiislamu na kuwaombea maghfira Waumini.

 

12-  Yanapatikana mapenzi, huruma na utulivu kati ya mke na mume na manufaa mengineyo ambayo Allaah Ta’aalaa Pekee Anayajua.

 

 

Share