04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Hukumu Ya Kuoa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

04-Hukumu Ya Kuoa:

 

Waislamu wote kwa itifaki wamekubaliana kwamba kuoa ni jambo la halali, kisha ‘Ulamaa wakakhitilafiana kuhusu hukmu yake katika kauli tatu:

 

Ya kwanza:  Ni wajibu kwa kila mwenye uwezo mara moja tu katika maisha yote.  Ni madhehebu ya Daawuwd Adh-Dhwaahiriy na Ibn Hazm, na pia ni kauli ya baadhi ya Salaf.  Dalili yao ni amri zilizoelezwa kwenye baadhi ya Aayaat na Hadiyth zilizotangulia ambazo zinaraghibisha kuoa.  Wamesema asili ya amri hizo ni uwajibu, kwa kuwa hakuna matini nyingine zilizozitoa nje ya duara hilo.

 

Ya pili:  Ni jambo linalopendeza.  Ni madhehebu ya ‘Ulamaa walio wengi, Jumhuwr ya Maimamu wanne na wengineo.

 

Wamezichukulia amri za kuoa kama ni za himizo la jambo linalopendeza.  Wakasema katika Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ"

 

“Basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine”, kwamba Allaah Ta’aalaa Amelifungamanisha jambo la kuoa na mtu kupendezewa nalo.  Hivyo basi, ambaye nafsi yake haikupendezwa na kuoa, basi hakuna ubaya kwake.  Na hapo hapo, Allaah Akasema:

 

"مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ"

 

“Wawili au watatu au wanne”, na hili si wajibu kwa itifaki ya ‘Ulamaa, hivyo basi inaonyesha kwamba jambo lenyewe si faradhi, bali linapendeza. 

 

Hoja yao imejibiwa kwamba lililofungamanishwa na kupendezewa ni amri ya kuoa zaidi ya mke mmoja, yaani inapendeza mtu kuongeza wa pili, wa tatu n.k,  na si kwa asili ya ndoa yenyewe ya mke mmoja.

 

Jumhuwr wamesema:  Vile vile Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ"

 

basi mmoja tu au ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki.  [An-Nisaa: 03]

 

Ya tatu:  Hukmu yake inatofautiana kwa mujibu wa hali ya mtu.  Hili ni mashuhuri kwa Wamaalik, Mashaafi’i na Mahanbali.  Wamesema:

 

(a)  Ndoa inakuwa ni waajib kwa mtu ambaye ana hamu na kiu ya tendo la kujimai na anajihofia kufanya zinaa kama hatooa.  Mtu huyu ni lazima aizuie nafsi yake na haramu, na njia ya kuzuia ni kuoa, kwani jambo ambalo wajibu hautimii ila kwalo, basi linakuwa ni lazima.   

 

(b)  Ndoa inakuwa ni jambo lenye kupendeza kwa mtu mwenye hamu ya jimai lakini ana uwezo wa kujidhibiti asiweze kufanya zinaa.  Mtu huyu kuoa kwake inakuwa ni bora zaidi kuliko kujikita kwenye ibada za sunnah.  Hii ni kauli ya Jumhuwr, kinyume na Ash-Shaafi’iy, yeye anasema kujikita kwenye ibada za sunnah ni bora zaidi kuliko kuoa katika hali hii.

 

(c)  Ndoa inakuwa ni haramu kwa mtu ambaye hajiwezi kwa tendo la ndoa na mkewe, lakini pia uwezo wake ni duni mno katika matumizi ya maisha.

 

Ninasema:  “Kuoa ni moja kati ya sunnah zilizokokotezwa mno.  Ndoa ni mwenendo wa Mitume wote kama tulivyoona katika Aayaat na Hadiyth zilizotangulia ambazo zinaraghibisha jambo hili.  Na hapana shaka kuwa kama mtu atahofia kuzini na uwezo wa kuoa anao, basi itakuwa ni waajib kuoa.  Ama kufanya baadhi ya vigawanyo vyake kuwa ni jambo mubaah, hii inakuwa ni kuzikinga dalili na kuyarejesha maraghibisho mengi yaliyotajwa kwenye Qur-aan na Sunnah.  Kadhalika, haifai kuifanya ndoa kuwa haramu kwa asiyejiweza katika tendo la ndoa, kwani ndoa ina malengo mengineyo ambayo yanaweza kupatikana ikiwa mke ataridhia udhaifu huo wa mume wake.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

 

Share