08-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Walioharamishwa Kwa Sababu Ya Uhusiano Wa Ndoa (Hawa Ni Wanne)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

08-Walioharamishwa  Kwa Sababu Ya Uhusiano Wa Ndoa (Hawa Ni Wanne):

 

1-  Mke wa baba:

 

Ibn ‘Abbaas:

 

"كَانَ أَهْلُ الجَاهِلِيَّةِ يُحَرَمُوْنَ مَا يَحْرُمُ إِلا امْرَأَةَ الأبِ والجَمْعُ بَيْنَ الأُخْتَيْن، قَالَ: فَأَنْزَلَ اللهُ عَزَّ وَجَلَّ: وَلَا تَنكِحُوا مَا نَكَحَ آبَاؤُكُم مِّنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا قَدْ سَلَفَ وَأَن تَجْمَعُوا بَيْنَ الْأُخْتَيْنِ"

 

“Watu wa enzi ya ujahili walikuwa wanaharamisha yaliyo haramu isipokuwa mke wa baba na kuoa dada wawili kwa wakati mmoja, hili lilikuwa halali.  Allaah ‘Azza wa Jalla Akateremsha:  “Na wala msiwaoe wanawake waliowaoa baba zenu isipokuwa yaliyokwisha pita”.  Na Kauli Yake:  “Na kuwaoa dada wawili kwa wakati mmoja”.  [Tafsiyr At-Twabariy (8/132) kwa Sanad Swahiyh]

 

Katika Aayah tajwa ya kwanza, Allaah Ta’aalaa Amekataza mtu kumwoa mwanamke ambaye aliolewa na baba yake.  Lakini Allaah Hakubainisha kusudio la neno “nikaah” kwa baba, je ni kufunga naye  ndoa, au kumuingilia?  ‘Ulamaa kwa upande wao wamesema kwa sauti moja kwamba mwanamke aliyefunga ndoa na baba, ni haramu kuolewa na mtoto wake wa kiume hata kama baba hajamuingilia, na uharamu huu unakuwa ni wa milele.  Na pia ni haramu kwa baba kumwoa mwanamke ambaye mtoto wake wa kiume amefunga naye ndoa hata kama hakumgusa.

 

Al-Baraa amesema:

 

"لَقِيْتُ عَمِّي وَمَعَهُ رَايَةٌ فَقُلْتُ: أَيْنَ تُرِيدُ؟ فَقَالَ: بَعَثَنِي رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِلَى رَجُلٍ نَكَحَ امْرَأَةَ أَبِيهِ فَأَمَرَنِي أَنْ أَضْرِبَ عُنُقَهُ وَآخُذَ مَالَهُ"

 

“Nilikutana na ami yangu akiwa na bendera, nikamuuliza:  Unaelekea wapi?  Akasema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amenituma niende kwa mtu ambaye amemwoa mke wa baba yake.  Ameniamuru nimfyeke shingo na nitwae mali yake”.  [Swahiyh Lishawaahidihi.  Imkekharijiwa na Abu Daawuwd (4457), Ad-Daaramiy (2/153), Al-Haakim (4/357) na Al-Bayhaqiy (8/208).  Sheikh wetu amesema ni Swahiyh]

 

Adhabu ya mwenye kumwoa mke wa baba yake ni kuuawa na kutwaliwa mali yake kwa mujibu wa Hadiyth hii.

 

2-  Mama wa mke (mama mkwe):

 

Mtu akishafunga tu ndoa na binti, basi mama ya binti anakuwa ni haramu kwake kumwoa kwa mujibu wa kauli ya Jumhuwr ya ‘Ulamaa.  Na hii ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَأُمَّهَاتُ نِسَائِكُمْ"

 

“Na mama za wake zenu”.  [An-Nisaa: 23]

 

Mwanaume akimuingilia mke wake, basi mama yake anakuwa ni haramu kwake.  Na hapa anaingia vile vile mama ya mama wa mkewe, na mama ya baba yake.

 

3-  Binti ya mke (binti wa kambo):

 

Sharti ya kuharamika, ni mwanaume kumuingilia mama ya binti.  Ikiwa mama yake atafunga ndoa na mtu, na mtu huyu asiwahi kumuingilia, basi mtu huyu anaweza kumwoa binti yake.  Na hii ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَرَبَائِبُكُمُ اللَّاتِي فِي حُجُورِكُم مِّن نِّسَائِكُمُ اللَّاتِي دَخَلْتُم بِهِنَّ فَإِن لَّمْ تَكُونُوا دَخَلْتُم بِهِنَّ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ"

 

“Na watoto wenu wa kambo (wa kike) walio katika ulinzi wenu waliozaliwa na wake zenu ambao mmewaingilia ●  Lakini ikiwa hamkuwaingilia basi hakuna dhambi (kuwaoa)”.  [An-Nisaa: 23]

 

Ninasema:  “Kauli yenye nguvu ya ‘Ulamaa ni kwamba Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"اللَّاتِي فِي حُجُورِكُم"

(walio chini ya ulinzi wenu)

 

kwa maana ya wanaoishi nanyi katika nyumba zenu, hili halizingatiwi kuwa ni sharti la kuharamisha kumwoa binti ya mke, bali uharamu unabaki pale pale hata kama ataishi mbali na mama yake.  Kuishi mama na bintiye au wanawe kiujumla ndilo jambo lililozoeleka zaidi.  Linalotilia nguvu haya, ni kwamba Allaah Ta’aalaa Ameweka wazi kwa kusema:

 

"فَإِن لَّمْ تَكُونُوا دَخَلْتُم بِهِنَّ"

 

(Lakini ikiwa hamkuwaingilia)

 

na Hakusema:

 "فَإِنْ لَمْ يَكُنَّ في حُجُوْرِكُمْ"

 

(Lakini ikiwa hawako chini ya ulezi wenu),

 

kwa maana kuwa kumuingilia mama yake ni sharti kuu ya kuharamika kumwoa binti na si kuishi kwake ndani ya nyumba ya mume wa mama yake.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Wanajumuishwa kwenye hukumu hii mabinti wa mabinti wa mke na mabinti wa watoto wake wa kiume.

 

4-  Mke wa mtoto wa kiume wa kutoka mgongoni mwako:

 

Haijuzu mwanaume kumwoa mke wa mtoto wake wa kiume wa kutoka mgongoni kwake kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَحَلَائِلُ أَبْنَائِكُمُ الَّذِينَ مِنْ أَصْلَابِكُمْ"

 

“Na (mmeharamishwa) wake wa watoto wenu waliotoka katika migongo yenu”.

 

Anaingia ndani ya Aayaah hii vile vile mke wa mtoto wa kiume wa kunyonya.  Ama Neno Lake Ta’aalaa:

 

"الَّذِينَ مِنْ أَصْلَابِكُمْ"

 

“Waliotoka katika migongo yenu”,  

 

kwa kusema hivi, Allaah Amewatoa kando watoto wa kupanga ambao watu walikuwa wakiwalea na kuwafanya kama watoto wao wa damu wakati wa enzi ya ujahili.  Na hii pia inabainishwa wazi na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

"يَحْرُمُ مِنْ اَلرَّضَاعَةِ‏ مَا يَحْرُمُ مِنْ اَلنَّسَبِ"

 

“Lililo haramu kwa sababu ya kunyonya ni haramu pia kwa sababu ya nasaba”.  [Angalia Tafsiyr Ibn Kathiyr (1/471), At-Twabariy (8/149) na Al-Ummu (5/35)]

 

Faida:

 

Mabinti wa mke wa baba na mke wa mtoto wa kiume, ni ruksa kwa mtu kuwaoa, yaani, inafaa mtu kumwoa binti ya mke wa baba yake, na binti wa mke wa mtoto wake wa kiume.  Na hii ni kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Na ili kuwahifadhi kirahisi wanawake walioharamishwa kwa sababu ya ukwe, tunaweza kusema:  Wanawake wote wanaotokana na uhusiano wa ndoa ni halali kwa mwanaume isipokuwa wanne:  Mke wa baba yake, mama wa mke wake, binti ya mkewe ambaye amemuingilia, na mke wa mwanaye.

 

 

Share