07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Wanawake Walioharamika Kuwaoa Milele: Walio Haramu Kwa Sababu Ya Nasaba (Hawa Ni Saba)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

07-Wanawake Walioharamika Kuwaoa Milele: Walio Haramu Kwa Sababu Ya Nasaba (Hawa Ni Saba):

 

1-   Mama (wamama):  Hawa ni wale ambao kuna fungamano la uzao kati yao na mwanaume kwa upande wa mama au baba.  Ni kama mama zake, mama za baba zake na mababu zake kwa upande wa kuumeni na kikeni na kwenda juu.

 

2-  Mabinti:  Hawa ni wale walionasibishwa kwa mtu kwa kuwazaa.  Ni kama mabinti zake aliowazaa yeye, au mabinti wa binti zake (wajukuu) na kwenda chini. 

 

3-  Madada:  Hawa ni wa pande zote.

 

4-  Mashangazi:  Hawa ni dada wa baba na kwenda juu.  Hapa anaingia pia shangazi ya baba yake na shangazi ya mama yake.

 

5-  Makhalati:  Hawa ni dada za mama yake au mama wa baba zake (mabibi).

 

6,7-  Mabanati wa kaka na mabanati wa dada.  Hawa ni kutoka pande zote hata kama daraja yao itashuka.

 

Ibn ‘Abbaas amesema:

 

"حُرِّمَ مِنَ النَّسَبِ سَبْعٌ وَمِنَ الصِّهْرِ سَبْعٌ، ثُمَّ قَرَأَ: حُرِّمَتْ عَلَيْكُم أُمَّهَاتكُم [الْآيَة]"

 

“Walioharamishwa kwa sababu ya nasaba ni saba, na kutokana na uhusiano wa ndoa ni saba”.  Kisha akasoma aayaah ya 23 ya Suwrat An-Nisaa.  [Al-Bukhaariy (5105) na At-Twabariy katika “At-Tafsiyr” (8/141), na Al-Haakim (2/304)] 

 

Na ili kulijua suala hili kwa wepesi, kidhibiti chake ni:  “Kwamba akaribu wote wa mwanaume kwa upande wa nasaba ni haramu kwake ila wanne:  Mabanati wa ami yake, mabanati wa mjomba wake, mabanati wa shangazi yake na mabanati wa khalati yake”. 

 

Wanne hawa, Allaah Ta’aalaa Alimhalalishia Rasuli Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Alipomwambia:

 

"يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَحْلَلْنَا لَكَ أَزْوَاجَكَ اللَّاتِي آتَيْتَ أُجُورَهُنَّ وَمَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ مِمَّا أَفَاءَ اللَّـهُ عَلَيْكَ وَبَنَاتِ عَمِّكَ وَبَنَاتِ عَمَّاتِكَ وَبَنَاتِ خَالِكَ وَبَنَاتِ خَالَاتِكَ اللَّاتِي هَاجَرْنَ مَعَكَ"

 

“Ee Nabiy!  Hakika Sisi Tumekuhalalishia wake zako ambao uliwapa mahari yao, na  wale iliyomiliki mkono wako wa kuume katika wale (mateka) Aliokuruzuku Allaah, na mabinti wa ‘ammi zako, na mabinti wa mashangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa makhalati zako ambao wamehajiri pamoja nawe”.  [Al-Ahzaab: 50]

 

Swali:  Je, Inafaa Mtu Kumwoa Binti Yake Wa Zinaa?

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanaona kwamba haijuzu mtu kumwoa binti yake wa zinaa.  Wanasema kuwa binti huyu anaingia ndani ya Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"حُرِّمَتْ عَلَيْكُمْ أُمَّهَاتُكُمْ وَبَنَاتُكُمْ"

 

“Mmeharamishiwa (kuwaoa) mama zenu, na mabinti zenu”.  [An-Nisaa: 23]

 

Bali hata Jumhuwr wamevutana vikali kuhusiana na mtu aliyemwoa binti yake wa zinaa, je huyu atauawa au la?  Ahmad amesema atauawa!!

 

Katika kesi hii, ni haramu pia mtu kumwoa dada yake wa zinaa, au binti ya mtoto wake wa kiume wa zinaa, au binti ya binti yake wa zinaa, au binti ya kaka yake au dada yake wa zinaa.  Hii ni kauli ya ‘Ulamaa wote.

 

 

Share