14-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mpaka Wa Muda Wa Kunyonya Ili Umahramu Upatikane

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

 

14-Mpaka Wa Muda Wa Kunyonya Ili Umahramu Upatikane:

 

‘Ulamaa wana kauli nyingi kuhusiana na umri unaozingatiwa wa kumfanya mnyonyaji awe maharimu kwa anayemnyonyesha.  Kati ya kauli hizo, ziko tatu mashuhuri zaidi:

 

Kauli Ya Kwanza:  Unyonyeshaji unaoharamisha ni ule wa miaka miwili ya mwanzo tu. 

 

Hii ni kauli ya Jumhuwr ya ‘Ulamaa wakiwemo Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq, Abu Thawr na Al-Awzaa’iy.  Pia ni kauli ya ‘Umar na mwanawe ‘Abdullaah, Ibn Mas-‘uwd, Ibn ‘Abbaas, Abu Muwsaa na wake wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa ‘Aaishah.  Dalili zilizotolewa kuhusu kauli hii ni:

 

1-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ"

 

“Na wazazi wa kike wanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili.”  [Al-Baqarah: 233]

 

Wanasema kwamba haya ni maelekezo toka kwa Allaah Ta’aalaa kwa wamama kuwa wawanyonyeshe watoto wao unyonyeshaji ulio kamili nao ni miaka miwili.  Hivyo basi, unyonyeshaji wenye kuharamisha na ambao unapita njia ya unasaba ni ule uliokamilisha miaka miwili, na baada ya hapo, umahram haupatikani. [Angalia Tafsiyr Al-Qurtwubiy (Al-Baqarah: 233) na Ibn Kathiyr]

 

2-  Hadiyth ya ‘Aaishah:

 

"أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ دَخَلَ عَلَيْهَا وَعِنْدَهَا رَجُلٌ فَكَأَنَّهُ تَغَيَّرَ وجْهُهُ، كأَنَّهُ كَرِهَ ذَلِكَ فَقَالَت: إِنَّه أخي، فَقَالَ: "اُنْظُرْنَ مَنْ إِخْوَانُكُنَّ، فَإِنَّمَا اَلرَّضَاعَةُ مِنْ اَلْمَجَاعَةِ"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia ‘Aaishah na kumkuta mwanaume, akawa kama uso wake umebadilika, kana kwamba hilo limemchukiza.  Nikamwambia:  Huyu ni ndugu yangu.  Akasema:  “Hakikisheni vizuri kuwajua nani kaka zenu, kwani hakika kunyonya ni pale maziwa tu yanapokuwa ndio lishe pekee ya kumshibisha mtoto kutokana na njaa”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5102) na Muslim (1455)]

 

Yaani, uharamu (umahram) unaotokana na kunyonya ni ule wa mtoto anapokuwa bado mdogo hajala kitu kingine zaidi ya maziwa ambayo ndiyo yanayomshibisha na kumwondoshea njaa.

 

3-  Ummu Salamah amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا يُحَرِّمُ مِنَ الرِّضَاعِ إِلَّا مَا فَتَقَ الْأَمْعَاءَ فِي الثَّدْيِ وَكَانَ قبل الْفِطَام"

 

“Umahramu wa kunyonya haupatikani mpaka mtoto anyonye ziwa, na maziwa yapenye na kuingia kwenye machango yake, isitoshe, kunyonya kuwe kabla ya muda wa kuachishwa mtoto ziwa”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1162) na Ibn Maajah (6/214)]

 

4-  ‘Abdullaah bin Diynaar amesema:

 

"جَاءَ رَجُلٌ إِلَى عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ وَأَنَا مَعَهُ عِنْدَ دَارِ الْقَضَاءِ يَسْأَلُهُ عَنْ رَضَاعَةِ الْكَبِيرِ، فَقَالَ عَبْدُ اللَّهِ بْنُ عُمَرَ: جَاءَ رَجُلٌ إِلَى عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ فَقَالَ: إِنِّي كَانَتْ لِي وَلِيدَةٌ وَكُنْتُ أَطَؤُهَا فَعَمَدَتِ امْرَأَتِي إِلَيْهَا فَأَرْضَعَتْهَا فَدَخَلْتُ عَلَيْهَا فَقَالَتْ: دُونَكَ فَقَدْ وَاللَّهِ أَرْضَعْتُهَا.‏ فَقَالَ عُمَرُ: أَوْجِعْهَا وَأْتِ جَارِيتَكَ فَإِنَّمَا الرَّضَاعَةُ رَضَاعَةُ الصَّغِيرِ"‏

 

“Mtu mmoja alikuja kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar nami nikiwa naye kwenye ofisi ya mashtaka na hukumu na akamuuliza kuhusu hukmu ya kumnyonyesha mtu mzima.  ‘Abdullaah bin ‘Umar akamwambia:  Mtu mmoja alikuja kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab akamwambia:  Mimi nilikuwa na kijakazi, na nilikuwa ninamuingilia, na mke wangu akamwendea na kumnyonyesha. Nami nilipoenda kwa kijakazi, mke wangu akaniwahi na kuniambia:  Usimkaribie tena, naapa kwa Allaah, hakika nimemnyonyesha.  Umar akasema:  Kamtie adabu, na muingilie kijakazi wako, kwani hakika kunyonya kunakoleta umahram, ni kunyonya mtoto akiwa mdogo”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Maalik (1289), Abdulrazzaaq (7/462) na Al-Bayhaqiy (7/461)]

 

5-  Ibn ‘Umar amesema:

 

 "لاَ رَضَاعَةَ إِلاَّ لِمَنْ أُرْضِعَ فِي الصِّغَرِ وَلاَ رَضَاعَةَ لِكَبِيرٍ"

 

“Umahram wa kunyonya haupatikani ila kwa aliyenyonyeshwa udogoni, hakuna umahram wa kunyonya kwa mkubwa”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Maalik (1282), Abdulrazzaaq (7/465) na Ibn Jariyr katika At-Tafsiyr (4956)]

 

6-  Mtu mmoja alikuja kwa Ibn Mas-‘uwd akamwambia:  Nilikuwa na mke wangu, kisha ziwa lake likajaa na maziwa yakawa hayatoki.  Nikaanza kulinyonya titi lake na kutema maziwa yake .  Kisha nikamwendea Abu Muwsaa ili nimuulize kuhusu hili, naye akanijibu kwamba mke wangu amekuwa si halali tena kwangu.  Akasema:  Akasimama (Ibn Mas-‘uwd), nasi tukasimama pamoja naye, akatuongoza hadi kwa Abu Muwsaa.  Tulipofika alimuuliza Abu Muwsaa:  Umemjibu nini huyu?  Akamweleza fatwaa aliyomjibu.  Ibn Mas-‘uwd akaukamata mkono wa yule mtu na kumuuliza Abu Muwsaa:  Je, huyu ni mtoto mchanga?  Kunyonya kunakoleta umahram ni kule kunakojenga nyama na damu.  Abu Muwsaa akasema:  Msiniulize tena chochote madhali mwanachuoni huyu mkubwa yuko nanyi”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Abdulrazzaaq (7/463), Al-Bayhaqiy (7/461) na At-Twabariy (4958)]

 

7-  Ibn ‘Abbaas amesema:

"لا رضَاعَ إِلاَّ ما كَانَ في حَوْلَيْنِ"

 

“Unyonyaji mtoto hauzingatiwi (ukaleta umahram) ila ule uliofanyika katika miaka miwili”. [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Sa’iyd bin Mansouwr katika Sunanih (980) na Al-Bayhaqiy (7/462)]

   

8-  Wake wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliikataa kauli ya ‘Aaishah ya kupatikana umahram kwa kumnyonyesha mkubwa.   Hili litazungumziwa mbeleni.

 

Kauli Ya Pili:  Unyonyeshaji unaoharamisha ni ule ulio katika muda wa miezi thelathini (miaka miwili na nusu). 

 

Haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah, na hujja yake ni Kauli ya Allaah Ta’aalaa:

 

"وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا"

 

“Kuibeba mimba na kuachishwa kwake kunyonya ni miezi thelathini”.  [Al-Ahqaaf: 15]

 

Kauli ya tatu:  Kumnyonyesha mkubwa kunaharamisha kama kunavyoharamisha kumnyonyesha mdogo. 

 

Ni madhehebu ya Adh-Dhwaahiriyyah, ‘Atwaa na Al-Layth.  Hii pia ni kauli ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa).  Dalili ya kauli hii ni Hadiyth ya ‘Aaishah kuhusu Sahlah bint Suhayl ambaye alikwenda kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia”: 

 

"إِنِّي أَرَى فِي وَجْهِ أَبِي حُذَيْفَةَ مِنْ دُخُولِ سَالِمٍ - وَهُوَ حَلِيفُهُ-.‏ فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:‏ أَرْضِعِيهِ.‏ قَالَتْ: وَكَيْفَ أُرْضِعُهُ وَهُوَ رَجُلٌ كَبِيرٌ، فَتَبَسَّمَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  وَقَالَ: قَدْ عَلِمْتُ أَنَّهُ رَجُلٌ كَبِيرٌ‏"

 

“Sahlah binti Suhayl alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Ninaona alama ya maudhiko kwenye uso wa Abu Hudhayfah kutokana na kuingia Saalim kwetu (naye ni mwanaye wa kumlea, si wa kumzaa).  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Mnyonyeshe.  Akamuuliza:  Nitamnyonyesha vipi mtu mzima?!  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatabasamu na kumwambia:  Mimi ninajua kwamba yeye (Saalim) ni mtu mzima .  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1453)]

 

Jumhuwr wameijibu Hadiyth hii kwa majibu kadhaa.  Kati yake ni:

 

1-  Hili ni tukio mahsusi linalomhusu Sahlah na Saalim, haliwahusu wengine.  Na ndiyo sababu hata wake wengine wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walimkatalia ‘Aaishah kutolea dalili tukio hili.  Imepokelewa toka kwa ‘Urwah:

 

"أَبَى سَائِرُ أَزْوَاجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يَدْخُلَ عَلَيْهِنَّ بِتِلْكَ الرَّضْعَةِ أَحَدٌ مِنَ النَّاسِ - يُرِيدُ رَضَاعَةَ الْكَبِيرِ - وَقُلْنَ لِعَائِشَةَ وَاللَّهِ مَا نُرَى الَّذِي أَمَرَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  سَهْلَةَ بِنْتَ سُهَيْلٍ إِلاَّ رُخْصَةً فِي رَضَاعَةِ سَالِمٍ وَحْدَهُ مِنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  وَاللَّهِ لاَ يَدْخُلُ عَلَيْنَا أَحَدٌ بِهَذِهِ الرَّضْعَةِ وَلاَ يَرَانَا"

 

“Wake wote wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikataa aingie nyumbani kwao yeyote ambaye amenyonyeshwa nyonyesho hilo (la ukubwani), na wakamwambia ‘Aaishah:  “Tunaapa kwa Allaah kwamba hatuoni lile ambalo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemwamuru Sahlah bint Suhayl isipokuwa ni ruksa maalum toka kwa Rasuli ya kumnyonyesha Saalim tu pasina mwengine.  Tunaapa kwa Allaah kwamba hatutamruhusu yeyote aliyenyonyeshwa nyonyesho hili kuingia nyumbani kwetu, na wala hatotuona”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na An-Nasaaiy (6/106), Maalik (1288), Ahmad (6/269) na Al-Bayhaqiy (7/459).  Iko pia kwa Muslim (1454) na wengineo toka Hadiyth ya Ummu Salamah].

 

2-  Tukio hilo limenasikhiwa (limefutwa hukmu yake) na halizingatiwi, na hususan tarehe yake ikiwa haijulikani wala wakati wake.

 

Ninasema:  “Kauli yenye nguvu ni kwamba nyonyesho linalozingatiwa na lenye kuacha athari ni lile la miaka miwili ya kwanza ya umri wa mtoto kama walivyosema Jumhuwr.  Lakini, endapo patakuwepo dharura isiyoepukika ya mtu kuwa lazima aingie kwa mwanamke ambaye inakuwa ni vigumu kujisitiri asimwone, hapa ili kumfanya awe mahram yake, kutakuwa hakuna kizuizi cha kuitumia Hadiyth hii ya Sahlah na Saalim, na hasa tukizingatia kwamba linalojuzu kwa dharura halijuzu kwa jingine.  Na haya ni madhehebu ya Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahul Laah), na ni chaguo la Ash-Shawkaaniy.  Haya ninayoyasema ni kauli ya nne baada ya tatu zilizotangulia ambapo ndani yake zinajumuika Hadiyth zote katika suala hili bila ya kuzipuuza baadhi yake.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

 

Share