13-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Masharti Ya Uharamu (Umahram) Kwa Sababu Ya Kunyonya: Idadi Ya Manyonyesho Ya Kuleta Uharamu (Umahram): Kauli Ya Nne

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

13-Masharti Ya Uharamu (Umahram) Kwa Sababu Ya Kunyonya: Idadi Ya Manyonyesho Ya Kuleta Uharamu (Umahram):  Kauli Ya Nne:

 

"لاَ يُحَرِّمُ إِلا عَشْرِ رَضَعَاتٍ مَعْلُومَاتٍ فَأَكْثَرَ"

 

Hayaharamishi isipokuwa manyonyesho kumi na zaidi yaliyothibiti”.  Hili limepokewa toka kwa ‘Aaishah na Hafswa (Radhwiya Allaah ‘anhumaa).

 

1-  Toka kwa Saalim: 

 

"أَنَّ عَائِشَةَ أُمَّ الْمُؤْمِنِينَ أَرْسَلَتْ بِهِ وَهُوَ يَرْضَعُ إِلَى أُخْتِهَا أُمِّ كُلْثُومٍ بِنْتِ أَبِي بَكْرٍ الصِّدِّيقِ فَقَالَتْ: أَرْضِعِيهِ عَشْرَ رَضَعَاتٍ حَتَّى يَدْخُلَ عَلَىَّ.‏ قَالَ سَالِمٌ: فَأَرْضَعَتْنِي أُمُّ كُلْثُومٍ ثَلاَثَ رَضَعَاتٍ ثُمَّ مَرِضَتْ فَلَمْ تُرْضِعْنِي غَيْرَ ثَلاَثِ رَضَعَاتٍ فَلَمْ أَكُنْ أَدْخُلُ عَلَى عَائِشَةَ مِنْ أَجْلِ أَنَّ أُمَّ كُلْثُومٍ لَمْ تُتِمَّ لِي عَشْرَ رَضَعَاتٍ"

 

“Kwamba Mama wa Waumini ‘Aaishah alimpeleka -akiwa ananyonya- kwa dada yake Ummu Kulthum bint Abi Bakr As-Swiddiyyq na kumwambia:  Mnyonyeshe manyonyesho kumi ili aweze kuingia kwangu.  Saalim anasema:  Ummu Kulthum akaninyonyesha mara tatu halafu akaugua, na hakuninyonyesha tena isipokuwa mara hizo tatu.  Sikuwa nikiingia kwa ‘Aaishah kutokana na kwamba Ummu Kulthum hakunikamilishia manyonyesho kumi”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Maalik katika Al-Muwattwa (1278), Abdulrazzaaq (7/469) na Al-Bayhaqiy (7/457)]

 

2-  Swafiyyah bint Abiy ‘Ubayd (mke wa ‘Abdullaah bin ‘Umar) amesema:  

 

"أَنَّ حَفْصَةَ أُمَّ الْمُؤْمِنِينَ أَرْسَلَتْ بِعَاصِمِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ سَعْدٍ إِلَى أُخْتِهَا فَاطِمَةَ بِنْتِ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ تُرْضِعُهُ عَشْرَ رَضَعَاتٍ لِيَدْخُلَ عَلَيْهَا وَهُوَ صَغِيرٌ يَرْضَعُ فَفَعَلَتْ فَكَانَ يَدْخُلُ عَلَيْهَا"

 

Kwamba Mama wa Waumini Hafswah alimpeleka ‘Aaswim bin ‘Abdillaah bin Sa’ad akiwa mdogo ananyonya kwa dada yake Faatwimah bint ‘Umar bin Al-Khattwaab amnyonyeshe manyonyesho kumi ili awe mahram yake na aweze kuingia kwake bila tatizo.  Akamnyonyesha, naye (‘Aaswim) akawa anaingia kwake bila ukakasi wowote”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Maalik katika Al-Muwattwa (1279), Abdulrazzaaq (7/470) na Al-Bayhaqiy (7/457)].

 

Ninasema:  “Kauli yenye nguvu ni ya wale waliosema kuwa manyonyesho matano yaliyothibiti, ndiyo yanamfanya mtoto kuwa mahram.  Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah ya kunasikhiwa manyonyesho kumi na kubaki matano.  Pia Hadiyth hii inazatitiwa na Hadiyth ambazo hazikuainisha idadi, hivyo hayo matano yanaingizwa ndani yake.  Ama Hadiyth zilizotaja manyonyesho mawili, Hadiyth hizo haziko wazi katika kuharamisha manyonyesho matatu au manne.  Lakini pia riwaayah ya manyonyesho matano iko wazi, hivyo inakuwa ni mhimili wa kuegemewa.  Na kwa maneno haya, dalili zinapangika na wala hazikinzani”.

 

Faida:

 

Imeandikwa katika Al-Mughniy (7/547):  “Ikiwa mwanamke atapata maziwa kutokana na mimba aliyoipata toka kwa mumewe, kisha akamnyonyesha mtoto manyonyesho matatu halafu maziwa yake yakakatika, kisha akaja kuolewa na mume mwingine na akapata maziwa kutokana naye, kisha akamnyonyesha mtoto manyonyesho mawili, hapo anakuwa ni mama yake bila mvutano wowote kwa wenye kusema kwamba manyonyesho matano yanaharamisha, lakini yeyote katika waume wawili hawi ni baba wa mtoto, kwa kuwa hakukamilisha idadi ya manyonyesho yanayotokana na maziwa yake. Kwa maana wa kwanza, mtoto alipata matatu tu, nayo hayatoshi, na wa pili akaambulia mawili, nayo pia hayafikishi kiwango cha kuleta umahram na mtoto huyo, lakini mwanamke huyo alipata yote matano”.

 

 

Share