16-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Wanawake Walioharamika Kwa Muda: i-Dada Ya Mke

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

 

16-Wanawake Walioharamika Kwa Muda:  1- Dada Ya Mke:

 

 

Kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa, mwanaume haruhusiwi kuoa madada wawili kwa wakati mmoja.  Allaah Anasema:

 

"وَأَن تَجْمَعُوا بَيْنَ الْأُخْتَيْنِ إِلَّا مَا قَدْ سَلَفَ"

 

“Na (mmeharamishiwa) kuwaoa dada wawili kwa wakati mmoja, isipokuwa yaliyokwisha pita”.  [An-Nisaa: (23)]

 

Lakini ikiwa mkewe atafariki au akamtaliki, basi hapo ataruhusiwa kumwoa dada yake.

 

Ummu Habiybah bint Abiy Sufyaan alimwambia Rasuli:

 

"يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَنْكِحْ أُخْتِي هَمْنَة بنت أبي سُفْيَان، فَقَالَ: أَوَتُحِبِّينَ ذَاكَ؟‏ ‏‏قَالَتْ: نَعَمْ، لَسْتُ بِمُخْلِيَةٍ بِكَ، وَأَحَبُّ مَنْ شَارَكَنِي فِي خَيْرٍ أُخْتِي ‏.‏ قَالَ: ‏فَإِنَّهَا لاَ تَحِلُّ لِي"

 

“Ee Rasuli wa Allaah!  Mwoe dada yangu Hamnah bint Abiy Sufyaan.  Rasuli akamuuliza:  Unaridhia hilo?  Akasema:  Na’am, mimi si mke pekee kwako, nina wakewenza wenzangu, na  mtu ambaye ningependa zaidi ashirikiane nami katika kheri hii ni dada yangu.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Hilo kwangu si halali”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5101) na Muslim (1449)]

 

Wanalingana katika hili madada wa baba mmoja mama mmoja, au baba mmoja mama tofauti, au mama mmoja baba tofauti, au pia wawe kwa nasaba au kwa kunyonya.

 

Faida Mbili:

 

Ya kwanza:  Mtu akioa mwanamke halafu akamwoa dada yake, ndoa hii ya pili itakuwa ni batili, na ya kwanza itabaki sahihi, ni sawa akiwa amemuingilia au hajamuingilia.  Ni lazima amtaliki huyo wa pili.  Na kama ana kijakazi anamuingilia, na kijakazi huyu ana dada yake, basi haruhusiwi kumuingilia dada yake huyu ila kama atamuuza, au atamwozesha au atamwacha huru (huyo anayemuingilia), hapo dada yake huyo atakuwa ni halali kwake.

 

Na kama atawaoa wote wawili kwa aqdi moja, ndoa itafisidika.

 

Ya pili:  Ikiwa kafiri aliyeoa dada wawili kwa pamoja atasilimu, huyu itabidi abaki na mmoja tu na amtaliki mwingine.

 

 

Share