21-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kuoa Wanawake Wa Ahlul Kitaab Kuko Nje Ya Duara La Uharamisho

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

 

21-Kuoa Wanawake Wa Ahlul Kitaab Kuko Nje Ya Duara La Uharamisho:

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

 

"الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ ۖ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ ۖ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ مُحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ وَلَا مُتَّخِذِي أَخْدَانٍ"

 

“Leo mmehalalishiwa vilivyo vizuri.  Na nyama iliyochinjwa na waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na nyama mliyochinja nyinyi ni halali kwao.  Na (mmehalalishiwa pia) wanawake waungwana wema katika Waumini na wanawake waungwana wema katika wale waliopewa Kitabu kabla yenu; mtakapowapa mahari yao bila kuwa maasherati wala kuchukua hawara”.  [Al-Maaidah: 05]

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wamesema kwamba makusudio ya "الْمُحْصَنَاتُ" hapa ni wanawake wema wachaji, ni sawa wakiwa waungwana au vijakazi.  Hivyo basi, kwa muktadha huu, wanawake wa Kiyahudi na Kinaswara hawaingii ndani ya haramisho la Kauli Yake Ta’aalaa:

 

وَلَا تَنكِحُوا الْمُشْرِكَاتِ

 

“Na wala msiwaoe wanawake washirikina”.  Na huu pia ni msimamo wa Jumhuwr ya Maswahaba.

 

1-  Ash-Sha’abiy amesema:

 

"تَزَوَّجَ أَحَدُ السِّتَّةِ مِنْ أَصْحَابِ الشُّورَى يَهُودِيَّةً"

 

“Mmoja wa watu sita aliowateua ‘Umar kushauriana ili kuchagua Khalifah baada yake alimwoa mwanamke wa Kiyahudi”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Sa’iyd bin Manswuwr katika “Sunanih” (717)] 

 

2-  Jaabir aliulizwa kuhusu mwanaume wa Kiislamu kumwoa mwanamke wa Kiyahudi au Kinaswara akasema:

 

"تَزَوَّجْنَاهُنَّ زَمَانَ الفَتْحِ بِالكُوْفَةَ معَ سَعْدِ بن أَبِيْ وَقَّاص، وَنَحْنُ لا نَكَادُ نَجِدُ المُسْلِمَاتِ كثِيْرًا، فلَمَّا رَجَعْنَا طَلَّقْنَاهُنَّ"

 

“Wakati wa ukombozi wa Makkah, tuliwaoa pamoja na Sa’ad bin Abiy Waqqaasw huko Kufah.  Ilikuwa ni vigumu sana kwetu kuwapata wanawake wa Kiislamu.  Tuliporudi, tuliwataliki”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Ash-Shaafi’iy katika “Al-Ummu” (5/8) na Al-Bayhaqiy (7/172)]

 

3-  Abu Waail kasema: 

 

"تَزَوَّجَ حُذَيْفَةُ يَهُوْدِيَّةً فَكَتَبَ إِلَيْهِ عُمَرٌ: طَلِّقْهَا، فَكَتَبَ إِلَيْهِ: لِمَ؟ أَحَرَامٌ هِيَ؟ فَكَتَبَ إِلَيْهِ: لا، وَلكِنِّيْ ×ِفْتُ أَنْ تَعَاطَوا المُوْمِسَاتِ مِنْهُنَّ"

 

“Hudhayfah alioa mwanamke wa Kiyahudi na ‘Umar akamwandikia barua ya kumwamuru amtaliki.  Naye akaandika kuuliza sababu kwa nini mwanamke huyo awe haramu.  Akamjibu akisema:  Hapana, si haramu, lakini nimehofia msije mkaoa makahaba kati yao”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Sa’iyd bin Manswuwr (716) na Al-Bayhaqiy (7/172)]

 

Baadhi ya ‘Ulamaa pamoja na Ash-Shaafi’iy wanaona kwamba Baniy Israaiyl ambao wanafuata dini ya Uyahudi au Unaswara, hao wanawake wao wanaolewa na wanyama waliochinja wanaliwa.  Ama yule ambaye amefuata dini yao naye si katika wao, ni sawa akiwa Mwarabu au taifa jingine lolote, basi hao wanawake wao hawaolewi wala walivyochinja haviliwi.  Hii pia ni kauli ya ‘Aliy bin Abi Twaaalib (Radhwiya Allaah ‘anhu) na baadhi ya Masalaf.

 

Toka kwa ‘Ubaydah toka kwa ‘Aliy, amesema:

 

"لا تُؤْكَلُ ذَبَائِحُ نَصَارى العَرَبِ، فَإِنَّهُمْ لا يَتَمَسَّكُونَ مِنَ النَّصْرَانِيَّةِ إِلا بِشُرْبِ الخَمْرِ"

 

“Vilivyochinjwa na Manaswara wa Kiarabu haviliwi, kwa kuwa wao hawashikamani na unaswara ila kwa kunywa tembo tu”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na ‘Abdulrazzaaq (6/72) na Al-Bayhaqiy (9/217)] 

 

Lakini maneno haya hayana dalili toka kwenye Qur-aan au Sunnah Marfuw’ah.  Ama kauli ya ‘Aliy, hiyo inapingana na kauli ya Maswahaba wengineo, bali hata Ibn ‘Abbaas amesema:  “Kuleni nyama iliyochinjwa na Bani Taghlab na oeni wanawake wao, kwani Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْيَهُودَ وَالنَّصَارَىٰ أَوْلِيَاءَ ۘ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ"

 

”Enyi walioamini! Msifanye Mayahudi na Manaswara marafiki wandani. Wao kwa wao ni marafiki wandani”.  [Al-Maaidah: 51]

 

Na lau kama wasingelikuwa miongoni mwao isipokuwa kwa urafiki, basi pia wangelikuwa ni miongoni mwao”.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah katika Al-Muswannaf (3/477) na Al-Bayhaqiy (9/217)]

 

Mtumishi wa ‘Umar alimwandikia barua akimweleza kwamba kuna watu kule aliko wanaojulikana kama “As-Saamirah” ambao wanasoma Taurati na wanapumzika siku ya jumamosi, lakini hawaamini kufufuliwa.  Akamuuliza kama inafaa kula nyama zao walizochinja.  ‘Umar akamjibu na kumweleza kwamba hao ni sehemu ya Ahlul Kitaab.  [Isnaad yake ni swahiyh.  Imekharijiwa na Abdulrazzaaq (7/187) na Al-Bayhaqiy (7/173)]

 

Ninasema:  “Nyuma kidogo tumeeleza kwamba ‘Umar alimwamuru Hudhayfah amtaliki mwanamke wa Kiyahudi aliyekuwa amemwoa.  Agizo hilo kama ilivyobainika halikuwa kwa ajili ya kuharamisha ndoa kama hiyo, bali ‘Umar alikuwa anachelea Wanaume wa Kiislamu kuja kuoa wanawake makahaba katika hao.  Hili ni jambo la kuzingatiwa na kutanabahiwa pamoja na kujuzu kwake.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”. 

 

 

Share