01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume: Kwanza: Haki Zinazompasa Mke Kumtendea Mumewe
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الحُقُوْقُ بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume
Kwanza: Haki Zinazompasa Mke Kumtendea Mumewe: Baadhi Ya Dalili Kutoka Kwenye Qur-aan Na Hadiyth:
Asili ya haki hizi iko ndani ya Kauli Yake Ta’aalaa:
"الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا "
“Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine, na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao. Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. Na wale ambao mnakhofu uasi wao wa ndoa, basi wanasihini na wahameni katika malazi na wapigeni (kipigo kisichodhuru). Wakikutiini, basi msitafute njia dhidi yao (ya kuwaudhi). Hakika Allaah daima Ni Mwenye Uluwa, Mkubwa wa Dhati, Vitendo na Sifa”. [An-Nisaa: 34]
Haki anazopaswa mke kumtendea mumewe ni kubwa mno kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"لا يَصْلُحُ لبَشَرٍ أنْ يَسْجُدَ لِبَشَرٍ، وَلَوْ صَلَحَ أَنْ يَسْجُدَ بَشَرٌ لِبَشَرٍ ، لَأَمَرْتُ المرْأَةَ أَنْ تَسْجُدَ لِزَوْجِهَا مِنْ عِظَمِ حَقِّهِ عَلَيْهَا ، وَالَّذِيْ نَفْسِيْ بِيَدِه ، لَوْ أَنَّ مِنْ قَدَمِهِ إلى مَفْرِقِ رَأْسِهِ قُرْحَةً تَنْبَجِسُ بالقَيْحِ والصَّدِيدِ ، ثم أَقْبَلَتْ تَلْحَسُه ، ما أَدَّتْ حَقَّه"
“Si haki kwa mwanadamu kumsujudia mwanadamu mwenzake. Na lau ingelikuwa ni haki kwa mwanadamu kumsujudia mwanadamu mwingine, basi ningelimwamuru mwanamke amsujudie mumewe kutokana na ukubwa wa haki anazopasa kumtendea. Basi naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake, lau kama mume ana madonda yenye kutumbuka maji maji na usaha kuanzia miguuni hadi kichwani, kisha mke akawa anampangusa kwa ulimi wake, basi pia asingeliweza kuikamilisha haki yake”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyhul Jaami’i (7725)]
Kadhalika, mwanamke kumtii mumewe ni moja kati ya mambo yatakayomfanya aingie Peponi. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا صَلَّتْ الْمَرْأَةُ خَمْسَهَا، وَصَامَتْ شَهْرَهَا، وَأَحْصَنَتْ فَرْجَهَا، وَأَطَاعَتْ زَوْجَهَا، قِيْلَ لَهَا: ادْخُلِي الجَنَّةَ مِنْ أَيِّ اَبْوَابِهَا شِئْتِ"
“Mwanamke akiswali swalaah zake (tano), akafunga mwezi wake (wa Ramadhaan), akalinda utupu wake (na zinaa), na akamtii mumewe, ataambiwa (Siku ya Qiyaamah): Ingia Jannah kupitia mlango wake wowote uutakao”. [Hadiyth Swahiyh. Ibn Hibaan (4163)]
Ikiwa mambo ni hivi, basi ni vyema sana kwa mwanamke wa Kiislamu kuzijua vyema haki anazopaswa kumfanyia mumewe. Haki hizo ni hizi zitakazotajwa moja baada ya nyingi.
