02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume: Haki Zinazompasa Mke Kumtendea Mumewe: 1- Amtii Kwa Mambo Yote Halali Anayomwamuru

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

الحُقُوْقُ بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

 

Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume

 

Alhidaaya.com

 

 

01:  Haki Zinazompasa Mke Kumtendea Mumewe:  1- Amtii Kwa Mambo Yote Halali Anayomwamuru:

 

"عَنِ الْحُصَيْنِ بْنِ مِحْصَنٍ، أَنَّ عَمَّةً لَهُ أَتَتِ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي حَاجَةٍ، فَفَرَغَتْ مِنْ حَاجَتِهَا، فَقَالَ لَهَا النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أَذَاتُ زَوْجٍ أَنْتِ؟  قَالَتْ: نَعَمْ، قَالَ: كَيْفَ أَنْتِ لَهُ؟ قَالَتْ: مَا آلُوهُ إِلَّا مَا عَجَزْتُ عَنْهُ، قَالَ: فَانْظُرِي أَيْنَ أَنْتِ مِنْهُ، فَإِنَّمَا هُوَ جَنَّتُكِ وَنَارُكِ" 

 

“Toka kwa Al-Huswayn bin Mihswan amesema kwamba:  Shangazi  yake alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya haja fulani.  Alipomaliza kueleza haja yake, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza:  Una mume wewe?  Akajibu:  Na’am.  Akamuuliza:  Uko naye vipi?  Akasema:  Sizembei kwa lolote (analoniamuru) isipokuwa lile nisiloliweza.  Akamwambia:  Basi chunga nafasi yako kwake,  kwani yeye ndiye (sababu ya) Pepo yako na moto wako”.  [Hadiyth Hasan.  An-Nasaaiy katika Al-‘Ishrah (uk. 106), Al-Haakim (2/189), Al-Bayhaqiy (7/291) na Ahmad (4/341)]

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu mwanamke aliye bora zaidi kuliko wengine akajibu:

 

"الَّتي تُطِيْعُ زَوْجَهَا إِذَا أَمَرَ، وَتَسُرُّهُ إِذَا نَظَرَ، وَتَحْفَظُهُ فِي نَفْسِهَا وَمَالِهِ"

“Ni yule anayemsikiliza mumewe anapomwamrisha, anamfurahisha anapomtazama, na anamlinda kwa kujichunga yeye mwenyewe na mali yake”.  [Hadiyth Swahiyh.  An-Nasaaiy (6/68)]

 

Angalizo:

 

Utiifu wa mke kwa mumewe una mipaka yake.  Mwanamke anaruhusiwa kumtii mumewe kwa yote yanayokubalika kisharia.  Ama kwa ya kumwasi Allaah Ta’aalaa, hayo hayaruhusiwi kumtii.  Ni kama kumwamuru atoke nje bila hijabu, au asiswali, au amuingilie kinyume na maumbile au wakati akiwa katika hedhi na kadhalika.  Kwa mambo kama haya haruhusiwi kumtii.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا طَاعَةَ فِي مَعْصِيَةٍ إِنَّمَا الطَّاعَةُ فِي الْمَعْرُوف"

 

“Hakuna ruksa hata kidogo kutii jambo la uasi, bali utiifu ni katika jambo jema la halali”.  [Al-Bukhaariy (7258) na Muslim (1840)]

 

 

Share