04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume: (ii) Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: Matumizi: Masharti Ya Matumizi Kuwa Wajibu

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

الحُقُوْقُ بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ

 

Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume

 

Alhidaaya.com

 

 

03:  Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: Matumizi: (b) Masharti Ya Matumizi Kuwa Wajibu:

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wameweka masharti kwenye suala hili.  Masharti haya ni ya kabla ya kumuingilia na baada ya kumuingilia mke.

 

Masharti Ya Kabla Ya Kumuingilia:

 

1-  Mke amwezeshe mume kumuingilia kwa kumrahisishia kila kitu baada ya ndoa kufungwa.  Na kama hakufanya hivyo, au akakataa bila ya udhuru wa kukubalika, basi matumizi yatakuwa si wajibu juu ya mume.

 

2- Mke awe na uwezo wa kuingiliwa, kwa maana, asiwe bint mdogo sana au kuwepo kizuizi kinachozuia tendo kufanyika.

 

3-  ‘Aqdi iwe sahihi.  Ikiwa ni batili, basi hakuna matumizi juu ya mume, na mke hazingatiwi kwamba yuko chini ya mamlaka ya mume, kwa kuwa ndoa yenyewe ni batili.

 

Masharti Baada Ya Kumuingilia:

 

1-  Mume awe anajiweza kimali.  Kama hali yake ni ngumu hana cha kutoa, basi si juu yake kutoa katika muda wote wa kugandwa na hali hiyo.  Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

"لِيُنفِقْ ذُو سَعَةٍ مِّن سَعَتِهِ ۖ وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ فَلْيُنفِقْ مِمَّا آتَاهُ اللَّـهُ ۚ لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا مَا آتَاهَا ۚ سَيَجْعَلُ اللَّـهُ بَعْدَ عُسْرٍ يُسْرًا"

 

Ili mwenye wasaa agharimu kwa wasaa wake, na aliyebaniwa riziki yake, basi agharimie katika kile Alichompa Allaah.  Allaah Haikalifishi nafsi yeyote ile isipokuwa kwa kile Alichoipa.  Allaah Atajaalia baada ya ugumu kuwa wepesi”.  [At-Twalaaq: 07]

 

2-  Awe chini ya mamlaka yake (asiwe ametoka nje ya mamlaka ya utiifu), akitoka, basi mume hana matumizi juu yake.

 

Faida:  Mwanamke Anayefanya Kazi, Je, Mume Anawajibikiwa Kumpa Matumizi?

 

Ikiwa atafanya kazi mbali na nyumba yake -kazi ya halali- na kwa ridhaa ya mume, basi ni lazima mume ampatie matumizi, kwa sababu yeye mwenyewe ameiachia haki ya mkewe kubaki nyumbani.  Na kama hakuridhia, akamkataza kutoka naye akatoka kwenda kufanya kazi, basi haki yake ya kupewa matumizi itadondoka, kwa kuwa haki kwa mumewe ya kubakia nyumbani katika hali hii inakuwa na pengo.  (Ibn ‘Aabidiyna (2/891)]

 

 

Share