05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume: (ii) Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: Matumizi: Makadirio Ya Matumizi Kwa Mke
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الحُقُوْقُ بَيْنَ الزَّوْجَيْنِ
Haki Za Kutendeana Kati Ya Mke Na Mume
04: Haki Zinazompasa Mume Kumtendea Mkewe: Matumizi: (c) Makadirio Ya Matumizi Kwa Mke:
Asili ya hili ni Kauli Yake Ta’aalaa:
"لِيُنفِقْ ذُوْ سَعَةٍ مِّنْ سَعَتِهِ"
“Ili mwenye wasaa agharimu kwa wasaa wake”. [At-Twalaaq: 7]
Na Kauli Yake:
"وَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ"
“Wapeni kiliwazo kwa mwenye wasaa kadiri ya uwezo wake na mwenye dhiki kadiri ya uwezo wake. Maliwaza kwa mujibu wa ada, ni haki kwa wafanya ihsaan”. [Al-Baqarah: 236]
Na pia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia Hind (mke wa Abu Sufyaan):
"خُذِي مَا يَكْفِيكِ وَوَلَدَكِ بِالْمَعْرُوفِ".
“Chukua kinachokutosha wewe na wanao kwa mujibu wa mahitaji”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5364) na Muslim (1714)]
Linalozingatiwa hapa ni:
1- Kumtosheleza mke na watoto mahitaji yao kwa mujibu wa ada, na hili linatofautiana kwa kupishana hali za watu, mwahala na zama.
2- Uwezo wa mume na wasaa wake:
‘Ulamaa (Rahimahumul Laahu) walizamia sana suala la kuainisha kiasi kilicho wajibu katika matumizi. Wakachanganua kwenye hilo, na sisi tukaweza kuliona wakiwa wamelibainisha kwa mujibu wa ada na desturi za nyakati zao.
Katika suala hili la matumizi, je linalozingatiwa humo ni hali ya mume, au mke, au hali zao wote wawili? Kwa mujibu wa aayaat zilizopita nyuma, linalozingatiwa ni hali ya mume; kama ana uwezo au hana uwezo. ‘Ulamaa wa Kimaalik na Kishaafi’iy ndivyo wanavyoona.
