01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mke Zaidi Ya Mmoja: Uhalali Wake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

تَعَدُّدِ الزَّوْجّاتِ

 

Mke Zaidi Ya Mmoja

 

Alhidaaya.com

 

01:  Uhalali Wake:

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"وَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تُقْسِطُوا فِي الْيَتَامَىٰ فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَلَّا تَعُولُوا "

 

“Na mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu kwa mayatima, basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne.  Lakini mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki.  Hivyo ni karibu zaidi kwamba hamtoelemea kudhulumu”.  [An-Nisaa: 03].

 

Katika aayah hii, Allaah Ta’alaa Anawasemesha wasimamizi wa mayatima.  Anawaambia:  “Ikiwa binti yatima yuko chini ya ulezi na usimamizi wa mmoja wenu (naye akataka kumwoa), na akahofia kwamba hatompa mahari stahiki, basi ni vyema asimwoe, bali atafute mwanamke mwingine, kwani wanawake wa kuoa wako wengi tu.  Na Allaah Hakumbana, bali Amemhalalishia kuoa kuanzia mmoja hadi wanne.  Lakini ikiwa atakhofia kwamba hatoweza kuwatendea haki, basi ni lazima atosheke na mmoja tu, au vikajazi anaowamiliki”.  [Hivi ndivyo alivyoifasiri aayah hii bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) kama ilivyo kwenye Al-Bukhaariy (4576)]

 

Nyuma zimetajwa dalili nyingi zinazohimizia kuoa ili kuongeza kizazi na watoto.  Sa’iyd bin Jubayr anasema:

 

"قَالَ لِي ابْنُ عَبَّاسٍ: هَلْ تَزَوَّجْتَ؟  قُلْتُ: لاَ‏.‏ قَالَ: فَتَزَوَّجْ، فَإِنَّ خَيْرَ هَذِهِ الأُمَّةِ أَكْثَرُهَا نِسَاءً‏".‏

 

“Ibn ‘Abbaas aliniuliza:  Je, umeoa?  Nikamwambia:  Hapana.  Akaniambia:  Oa, kwani  mbora zaidi wa umma huu (Rasuli) ndiye aliye na wake wengi zaidi”.  [Al-Bukhaariy (5069)]

 

Dalili hizi na nyinginezo, zinathibitisha kupendeza mwanaume wa Kiislamu kuoa zaidi ya mke mmoja, lakini kwa kuchunga masharti na vidhibiti maalum.

 

 

Share