04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mke Zaidi Ya Mmoja: Baadhi Ya Faida Za Kifiqhi Za Ndoa Ya Wake Wengi
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
تَعَدُّدِ الزَّوْجّاتِ
Mke Zaidi Ya Mmoja
04: Baadhi Ya Faida Za Kifiqhi Za Ndoa Ya Wake Wengi:
1- Inajuzu mahari kutofautiana kati ya mke na mke na hata chakula cha walima.
Nyuma tulieleza kwamba Mfalme Najaashiy (Negus) alimwozesha Ummu Habiybah kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akamlipia mahari ya dirham 4,000. Na mahari ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wakeze ilikuwa ni dirham 400 tu.
Anas akizungumzia walima aliofanya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwoa Zaynab binti Jahsh amesema:
"مَا رَأَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَوْلَمَ عَلَى أَحَدٍ مِنْ نِسَائِهِ مَا أَوْلَمَ عَلَيْهَا"
“Sikumwona Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimfanyia walima yeyote kati ya wake zake, kama aliyomfanyia Zaynab”. [Imetajwa nyuma]
2- Haijuzu mwanaume kuwaweka wake wenza nyumba moja ila kwa ridhaa yao.
Kila mke ni lazima awe na nyumba yake kando kama alivyofanya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Ta’aalaa Amesema:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ"
“Enyi walioamini! Msiingie nyumba za Nabiy isipokuwa mkipewa idhini ya kwenda kula, si kungojea kiive”. [Al-Ahzaab: 53]
Allaah Amezielezea hapa kama nyumba nyingi, na si nyumba moja, kama ilivyoelezwa kwenye milango ya nyuma.
3- Mgawo wa zamu kati ya wake.
Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba mtu akioa bikra kwa mke mkubwa “thayyib” (aliyekwisha ingiliwa), basi atakaa kwa bikra kwa muda wa siku saba, kisha baada ya hapo, atagawa siku za zamu za kulala kwao sawa kwa sawa.
Ama akioa “thayyib” kwa mke bikra, basi atakaa kwake kwa siku tatu, kisha atagawa siku za zamu za kulala kwao sawa kwa sawa.
Ni kutokana na Hadiyth ya Anas aliyesema:
"مِنَ اَلسُّنَّةِ إِذَا تَزَوَّجَ اَلرَّجُلُ اَلْبِكْرَ عَلَى اَلثَّيِّبِ أَقَامَ عِنْدَهَا سَبْعًا، ثُمَّ قَسَمَ، وَإِذَا تَزَوَّجَ اَلثَّيِّبَ أَقَامَ عِنْدَهَا ثَلَاثًا، ثُمَّ قَسَمَ "
“Ni katika Sunnah mtu akioa bikra kwa “thayyib”, akae kwa bikra siku saba, kisha agawe zamu (sawa kwa sawa). Na akioa “thayyib” kwa bikra, akae kwa “thayyib” siku tatu, kisha agawe zamu (sawa kwa sawa)”. [Al-Bukhaariy 5214) na Muslim (1461)]
Angalizo:
Baadhi ya watu wameifahamu vibaya Hadiyth hii. Wanadhani kwamba mume anapooa bikra, basi ajifungie naye ndani siku hizo saba na asitoke hata kwenda kuswali jamaa msikitini. Huu ni ufahamu batili usio na dalili yoyote. Hatakikani akose jamaa kama ilivyo kwa watu wengine.
4- Je, ni lazima mume afanye usawa kati ya wakeze katika penzi na jimai?
Penzi na mahaba mahala pake ni moyoni. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَلَن تَسْتَطِيعُوا أَن تَعْدِلُوا بَيْنَ النِّسَاءِ وَلَوْ حَرَصْتُمْ"
“Na wala hamtoweza kuadilisha baina ya wake japokuwa mtapania”. [An-Nisaa: 129]
Makusudio ya kutokuweza hapa ni katika mahaba, jimai na matamanio, haya ni mambo ambayo mtu hawezi kuyadhibiti.
Na katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas, ‘Umar aliingia kwa Hafswah na kumwambia:
"يَا بُنَيَّةِ، لاَ يَغُرَّنَّكِ هَذِهِ الَّتِي أَعْجَبَهَا حُسْنُهَا حُبُّ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِيَّاهَا ـ يُرِيدُ عَائِشَةَ ـ فَقَصَصْتُ عَلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَتَبَسَّمَ"
“Ewe binti yangu! Angalia sana usije kuhadaika na huyu anayeringia uzuri wake na kupendwa zaidi na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) -anamkusudia ‘Aaishah-. Nikamhadithia hilo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye akatabasamu”. [Al-Bukhaariy (49/3) na Muslim (1479)]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa:
"أَىُّ النَّاسِ أَحَبُّ إِلَيْكَ؟ قَالَ: عَائِشَةُ"
“Ni yupi kati ya watu umpendaye zaidi? Akajibu: ‘Aaishah”. [Sunan Ibn Maajah: 101]
Ibn Qudaamah amesema: “Hatujui mvutano wowote kati ya ‘Ulamaa kuhusiana na suala la kuwa si wajibu kufanya usawa kati ya wake katika tendo la jimai, kwa sababu, chanzo cha jimai ni matamanio na msisimko, na hili halina ujanja wa kuweza kufanya usawa ndani yake. Moyo wa mume unaweza kulemea zaidi kwa mmoja wao pasi na mwengine (bila kuwa na uwezo wa kudhibiti hilo)”.
Ama kwa upande wa matumizi ya kawaida, hilo bila shaka ni wajibu kwa mume kufanya usawa kati yao.
5- Haijuzu kwa mwanamke kumtaka mume amtaliki mke mwenzake ili abaki peke yake na mumewe.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَا تَسْأَلِ الْمَرْأَةُ طَلَاقَ أُخْتِهَا لِتَسْتَفْرِغَ صَحْفَتَهَا وَلِتَنْكِحَ فَإِنَّ لَهَا مَا قُدِّرَ لَهَا"
“Mwanamke asishawishi mwenzake atalikiwe ili yeye aolewe na atwaye nafasi yake, kwani hakika atapata kile tu alichokadiriwa (na Allaah)”. [Al-Bukhaariy (5152), na Muslim (1408)]
