03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mke Zaidi Ya Mmoja: Dhana Ya Kuoa Mke Zaidi Ya Mmoja

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

تَعَدُّدِ الزَّوْجّاتِ

 

Mke Zaidi Ya Mmoja

 

Alhidaaya.com

 

 

 

03:  Dhana Ya Kuoa Mke Zaidi Ya Mmoja:

 

 

Hakuna shaka yoyote kwamba kuoa mke zaidi ya mmoja ndio njia nyoofu zaidi kwa mwanaume kutokana na mambo ambayo yako wazi kabisa kwa kila mwenye akili.  Mambo hayo ni:

 

1-  Mwanamke kimaumbile hupata hedhi na nifasi, huugua na kupatwa na mengineyo yanayozuia tendo la ndoa.  Na mwanaume wakati wote anakuwa hana kizuizi cha tendo hilo ila kwa nadra sana, na anakuwa tayari kwalo wakati wowote, saa yoyote.  Sasa ikiwa mke ni mmoja, bila shaka inakuwa ni uzito sana kwa mume. 

 

2-  Allaah Amepitisha Qadari Yake ya idadi ya wanaume kuwa kidogo kuliko ya wanawake katika mataifa yote.  Wanaume ndio wanaokabiliwa zaidi na vifo kwenye medani nyingi za maisha na hususan kwenye vita.  Ikiwa mwanaume atatosheka na mke mmoja tu, basi idadi kubwa mno ya wanawake watabakia bila ndoa, na matokeo yake ni kufanya machafu.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelihesabu hilo kuwa moja kati ya alama za kukurubia Qiyaamah.  Anasema:

 

إِنَّ مِنْ أَشْرَاطِ السَّاعَةِ، أَنْ يُرْفَعَ الْعِلْمُ، وَيَكْثُرَ الْجَهْلُ، وَيَكْثُرَ الزِّنَا، وَيَكْثُرَ شُرْبُ الْخَمْرِ، وَيَقِلَّ الرِّجَالُ، وَيَكْثُرَ النِّسَاءُ حَتَّى يَكُونَ لِخَمْسِينَ امْرَأَةً الْقَيِّمُ الْوَاحِدُ ‏

 

“Miongoni mwa alama za (kukurubia) Qiyaamah, ni kuondoshwa ‘ilmu (ya dini kwa kufa ‘Ulamaa wachamungu), kukithiri ujinga (wa mambo ya dini), kukithiri zinaa, kukithiri unywaji pombe, wanaume kupungua na wanawake kuwa wengi hadi kufikia wanawake 50 kusimamiwa kwa huduma na mwanaume mmoja”.  [Al-Bukhaariy (5231) na Muslim (2671)]

 

3-  Wanawake wote wako tayari kuolewa, lakini wanaume wengi kutokana na umasikini, hawana uwezo wa kupata mahitajio ya ndoa.  Hivyo basi, wanaume walio tayari kwa ndoa ni kidogo kulinganisha na wanawake walio tayari kwayo.  Na hawa walio tayari, ni vyema waongeze wake ili kupunguza pengo la idadi.

 

4-  Kuna baadhi ya wanaume ambao kwa mujibu wa maumbile yao ya kisaikolojia na kimwili, wana kiu kali sana ya tendo la ndoa, mwanamke mmoja hamtoshelezi.  Hivyo sharia imemfungulia milango ya kuwa na mke zaidi ya mmoja ili kushibisha utashi wake kwa njia halali badala ya kuhangaika na wanawake wa pembeni watakaomharibu tabia na kumletea maafa.

 

5-  Kunaweza kuwa ni msaada mzuri kwa mmoja wa jamaa au ndugu ambaye amefiliwa na mumewe au ametalikiwa.  Kumwoa huyu kutamwokoa na mahangaiko ya kimaisha, na atakidhiwa hitajio lake la hamu ya tendo la ndoa.

 

Ninasema:  “Ingawa jambo hili limesuniwa na linapendeza, na ni sehemu ya sharia samehevu ya Kiislamu, lakini kutokana na kutumiwa vibaya na baadhi ya watu, limekuwa kwenye mwono wa watu wengi kama ni uhalifu, uovu na utovu wa wema pamoja na tuhuma nyinginezo nyingi batili”. 

 

 

Share