05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa:Hukumu Zinazohusiana Na Mtoto Anayezaliwa: Kumpa Jina

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

مِنْ أَحْكَامِ المَوْلُودِ

 

Hukumu Zinazohusiana Na Mtoto Anayezaliwa

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

05:   Kumpa Jina:

 

(a)  Baba ndiye mwenye haki ya kutoa jina la mtoto, na mama hana haki ya kupinga.  Lakini pamoja na hivyo, ni vizuri sana washauriane na wakubaliane jina.  Kama watavutana, basi haki inabakia kwa baba.

 

(b)  Baba anatakiwa achague jina zuri kwa upande wa maana na linavyotamkwa.  Liwe zuri, tamu kwenye ulimi, linakubalika kwenye sikio, na halikuharamishwa au kukirihishwa kwa mujibu wa maelekezo ya Allaah na Rasuli Wake.

 

(c)  Majina Mazuri Yanayopendeza:

 

Majina yanayopendeza ni mengi.  Tunaweza kuyaweka katika utaratibu ufuatao:

 

1-  ‘Abdullaah na ‘Abdulrahmaan.  Ni kwa neno la Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"أَحَبُّ الأَسْمَاءِ إِلَى اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ عَبْدُ اللَّهِ وَعَبْدُ الرَّحْمَنِ ‏"

 

“Majina yanayopendeza zaidi kwa Allaah ‘Azza wa Jalla ni ‘Abdullaah na ‘Abdulrahmaan”.  [Swahiyh Muslim]

 

2-  Majina yenye kuanziwa na ‘Abdu (Mja) na kufuatiwa na Jina lolote Zuri la Allaah kama ‘Abdul ‘Aziyz, ‘Abdul Kariym, ‘Abdul Malik na kadhalika.

 

3-  Majina ya Manabii na Mitume.

 

4-  Majina ya Waislamu walio wema wakiongozwa na Maswahaba.

 

Imepokelewa toka kwa Al-Mughiyrah bin Shu-‘ubah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (akiwazungumzia Baniy Israaiyl) amesema:

 

"إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَمُّونَ بِأَنْبِيَائِهِمْ وَالصَّالِحِينَ قَبْلَهُمْ ‏"

 

“Hakika wao walikuwa wakiita (watoto wao) majina ya Manabii na wema wao waliotangulia”.  [Swahiyh Muslim]

 

5-  Yenye kubeba sifa ya kweli aliyonayo binadamu kwa masharti yafuatayo:

 

(a)  Yawe na asili ya Kiarabu.  Yasiyo na asili ya Kiarabu kama vile Diana, Haidey, Sherihan na kadhalika hayafai.

 

(b)  Yawe na maana nzuri na muundo murua.

 

(c)  Yawe na herufi chache kiasi iwezekanavyo.

 

(d)  Yatamkike kwa wepesi.

 

Majina Yaliyoharamishwa:

 

(a) Kila jina linalotanguliwa na “Abdu bila kufuatiliwa na Jina la Allaah kama vile ‘Abdul Rasuwl"عَبْدُ الرَّسُول" , ‘Abdul Hasan  "عَبْدُ الحَسَن"na kadhalika.

 

(b)  Kila jina linalohusiana na Allaah Pekee kama Ar-Rahmaan"الرَّحْمن" , Al-Khaaliq "الخَالِق"na kadhalika.

 

(c)  Majina ambayo ni mahsusi kwa makafiri kama George, Diana, Suzan na kadhalika.

 

(d) Majina ya masanamu yanayoabudiwa badala ya Allaah kama vile Al-Laata, Al-‘Uzza na kadhalika.

 

(e)  Majina yasiyo ya Kiarabu ambayo hayana nafasi katika Lugha ya Kiarabu kama Neriman, Jehan, Nevin na kadhalika.

 

(f)  Majina yenye kubeba sifa njema au mbaya asiyokuwa nayo mwitwaji.

 

(g)  Majina ya mashetani kama Khinzab"خِنْزَب" , Al A-’awar"الأَعْوَر"  na kadhalika.

 

Majina Yaliyokirihishwa:

 

1-  Majina yote yenye kuchukiza moyoni kutokana na maana zake au kutamkwa kwake kunakopelekea kuchezwa shere na watu, au wenye majina hayo kuhisi dhiki, au kuathirika vibaya kisaikolojia.

 

Majina hayo ni kama Khan-jar  "خَنْجَر"(aina ya kisu), Faadhwih  "فَاضِح"(mtovu wa hishma), Huyaam na Suhaam  "هُيَام" "سُهَام"(magonjwa ya ngamia) na kadhalika.

 

2-  Majina yenye maana laini yenye kuchemsha matamanio kama Ahlaam"أَحْلَام"  (ndoto), Ghaadah "غَادَة"  (msichana mzuri laini), Faatin "فَاتِن" (msichana mzuri anayevutia) na kadhalika.

 

3-  Majina ya waigizaji, waimbaji na wasanii wasio na chembe ya hofu kwa Allaah.  Na hii ni kwa kukusudia kumpa mtoto jina la watu hao kwa kuwa mtu anawapenda na kuwashabikia.

 

4-  Majina yenye kubeba maana ya dhambi na maasi kama Dhalimu "ظَالِم" , Mwizi  mbobezi  "سَرَّاق"na kadhalika.

 

5-  Majina ya mafirauni, madikteta, watawala madhalimu na watu makatili kama Firauni, Haamaan, Qaaruwn na kadhalika.

 

6-  Majina ya wanyama wenye sifa za kuchukiza kama punda, mbwa, nungu na kadhalika. 

 

7-  Majina yenye kuegemezewa kwenye dini au Uislamu kama vile Nuwrud Diyn  "نُوْرُ الدِّيْن"(Nuru ya dini),  Shihaabud Diyn "شِهَابُ الدِّيْن"  (Kimondo cha dini), Sayful Islaam "سَيْفُ الإِسْلَام"(Upanga wa Uislamu) na kadhalika.

 

8-  Majina ambatano (mawili kwa mpigo) kama Muhammad Ahmad na kadhalika.  Majina haya huchanganya watu.

 

9-  Majina ya Malaika kama vile Jibriyl, Miykaaiyl na kadhalika.

 

Share