Anafanya Kazi Ya Ulinzi Hapati Kuswali Je, Anaweza Kuswali Huku Ameketi?

SWALI:

 

Kwa uwezo wake ALLAH KARIM natumai mnaendelea vizuri na shughuli za kuwaelimisha waislam. Mimi nafanya kazi katika duka moja la kuuza germstone ikifika muda wa sala ya Adhuhuru naenda kuswali kwa kigezo kuwa natoka kwenda kwenye lunch, lakini muda wa laasiri ni ngumu kutoka kabisa naomba kuuliza je naweza kuswali nikiwa nimekaa kwenye kiti kwani hapa nilipo nipo kwenye mtihani. Nawatakia kila la kheri.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuswali ukiwa unaswali unapokuwa kazini.

Awali ya yote hukutueleza mwenye duka hilo ni nani – Muislamu au asiyekuwa Muislamu. Kwa hali zote, mwanzo unatakiwa ufanye bidii na juhudi ya kuzungumza na mwenye duka umuhimu wako kuswali wakati huo wa Alasiri. Unatakiwa uweke wazi kuwa Swalah ya Kiislamu haichukui muda mwingi na hata wanaweza kukupatia sehemu ya kufanyia ‘ibaadah hiyo.

 

Jambo hilo ni muhimu sana kwani ikiwa hukuwaelezea unaweza kuwa unaswali kwa kuketi wakati huo akaja mteja na ukashindwa kumfungilia ikawa ugomvi baina yako na mwenye duka. Ikiwa mwenye duka hakukubali kuhusu hizo dakika 5 zako kuswali, hata ukisema uswali kwa kukaa bado itakuwa tatizo kwako endapo atakuja mteja na hali wewe uko katika Swalah, sasa sijui umelitazama vipi hilo la kuswali kw akukaa ukaona lina tofautiana na la kuswali kwa kusimama katika mazingira uliyonayo?

Hata hivyo kwa dharura unaweza kuswali Swalah ya faradhi kwa kukaa, ama Swalah ya Sunnah haina tatizo kuiswali kwa kukaa.

 

Hata hivyo, jitahidi ulirekebishe hilo kwani huwezi kuswali hizo faradhi kwa kukaa siku zote kwani asli ni kuswali kwa kusimama na ndio ina daraja kubwa mara ya mbili ya anayeswali kwa kukaa.

 

Jitahidi uzungumze na wahusika kwa njia nzuri ya heshima na upole na inshaAllaah huenda wakaitikia maombi yako na kukupa wasaa wa kuifanya ‘Ibaadah hiyo kwa ukamilifu wake.

 

Tunakutakia kila la kheri uwe utafanikiwa kupatiwa ruhusa ili kusiwe na zogo wala kero kutoka kwa mwenye duka, na Allaah Atakulipa kwa juhudi zako hizo za kutaka kumtumikia Yeye vyema katika ‘Ibaadah zako

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo na faida ziada kuhusu mas-ala haya:

 

 

Kuswali Swalah Ya Safari Kwa Sababu Ya Udereva

 

 

Vipi Kukidhi Swalah Kama Shida Kuswali Kazini?

 

Hapati Kuswali Kwa Wakati, Kila Siku Anakidhi Swalah

 

Anaweza Kulipa Swalah Ya Magharibi Kila Siku Inayompita?

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share