Anaweza Kuwa Imaam Ikiwa Hajaoa? Vipi Watafute Qiblah?

 

SWALI:
 


ASALAM ALAYKUM WARAHMATULLAHI WA BARAKATUHU KWANZA NATOWA SHUKRAN ZADHATI KWA ALLAH KUNIWAFIKISHA KUPATA WEB YENU PILI NIKUWAPONGEZENI KWA KAZI NZURI MNAYO IFANYA KWA KUMTUMIKIYA ALLAH.  NAYE ATAKULIPENI KWA KAZI HIYO YAKUELIMISHA UMA.

MIMI NINAISHI BURUNDI BUJUMBURA NA NI MKURUGENZI WA MASDJID TAWHID MUSKITI WAPILI KUJENGWA BURUNDI NA WAPILI KWA UKUBWA HAPA BUJUMBURA NA UNAPATIKANA BUYENZI 19/22 SWALI LANGU NIKUHUSU IMAMU JE IMAM MWENYE HANA MKE INAKUBALIWA KISHERIYA KUONGOZA IBADA TENA KUPEWA UIMAMA MKUU? NAOMBA NIJIBUNI NA HILI VIPI TUTANAWEZA KUKITAFUTA KIBLA? kwakutumiya qurani na hadithi?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mas-ala ya kuimamisha Swalaah hayana ulazima kuwa mwanamume lazima awe ameoa, bali hata alsiyekuwa na mke anaweza kuwa Imaam.

 

Tumepata mafunzo katika Siyrah ya Mtume (Swalla-Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba mtoto mdogo aliwahi kuwa Imaam kwa vile yeye ndiye aliyekuwa mwenye kujua Qur-aan zaidi ya wengineo. Na hili ndilo sharti au sifa anayomiliki Imaam kutokana na usimulizi ufuatao:

 

عَنْ أَبِي مَسْعُودٍ الْبَدْرِيِّ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((يَؤُمُّ الْقَوْمَ أَقْرَؤُهُمْ لِكِتَابِ اللَّهِ وَأَقْدَمُهُمْ قِرَاءَةً فَإِنْ كَانُوا فِي الْقِرَاءَةِ سَوَاءً فَلْيَؤُمَّهُمْ أَقْدَمُهُمْ هِجْرَةً فَإِنْ كَانُوا فِي الْهِجْرَةِ سَوَاءً فَلْيَؤُمَّهُمْ أَكْبَرُهُمْ سِنًّا وَلَا يُؤَمُّ الرَّجُلُ فِي بَيْتِهِ وَلَا فِي سُلْطَانِهِ وَلَا يُجْلَسُ عَلَى تَكْرِمَتِهِ إِلَّا بِإِذْنِهِ))  

 

Kutoka kwa Abu Mas'uud Al-Badriyyi akisema: Mtumeصلى الله عليه وسلم amesema: ((Awaswalishe watu yule mwenye kujua kusoma zaidi Kitabu cha Allaah na mwenye kutangulia zaidi kwa kisomo. Ikiwa visomo vyao ni sawa, basi aswalishe yule aliyetangulia kuhama (Hijrah), na ikiwa wako sawa katika kuhama, aswalishe mkubwa wao kwa umri. Wala asiswalishe mtu katika nyumba yake (mgeni asiswalishe kwenye nyumba ya mwenyeji isipokuwa hadi aruhusiwe na mwenyeji wake) wala katika mamlaka yake wala asikae kwa heshima yake isipokuwa kwa ruhusa yake))) [Muslim na Abu Daawuud]      

 

Na katika riwaaya nyingine imeongeza kusema ((Na yule mwenye elimu ya Sunnah zaidi ya wengine))

Kwa hiyo, ikiwa mwenye kutaka kuswalisha anamiliki sifa hizo basi inampasa yeye aswalishe. Na hili halihusiani na mtu ikiwa mtu huyo ameoa au hakuoa, maadam ana sifa hizo, basi ni waajib yeye aswalishe.

Inapasa kujua kwamba haifai kuswalisha mtu ambaye hana elimu ya Qur-aan japokuwa ana cheo fulani kinginecho, kwani hivyo itakuwa ni kuswalisha makosa na kwa vile Imaam anabeba mas-uliya ya thawabu za wote anaoimamisha na hali kadhalika kosa lolote dhambi zote zitakuwa ni juu yake. Mara nyingi watu hushikilia kuwa Imaam bila ya kuwa na elimu au bila ya kustahiki na hali wako waliomshinda yeye kwa kustahiki kuswalisha. Hivyo ni muhimu hili kuzingatiwa.  Hata ikiwa ni kijana mdogo zaidi yake ni vizuri apewe huyo kijana kutokana na mafunzo tuliyopata katika Sunnah.

 

Ama kuhusu kutafuta Qiblah ni kwamba bila shaka huko kuna Misikiti mingine na hivyo itakuwa Qiblah kinajulikana kilipo. Basi ni kuuliza na kisha nanyi kufuata baada ya kuhakikisha. Pia ni kufahamu kutokana na Waislamu waliokuwepo maeneo mengine ya kwenu ni wapi wanafuata; Kaskazini au Kaskazini Mashariki n.k. Na njia nyingine ni kutumia dira (compass) inayoonyesha Qiblah. Dira hizo zinapatikana kwa bei hafifu kabisa. Njia nyingine ni kutumia nyenzo za kisasa kama tovuti mfano wa hii http://www.qiblalocator.com ambayo inaweza kukujulisha Qiblah kilipo katika mji wenu. Na katika nyenzo nyingine ambayo ni hii http://www.qiblahfinder.com/ tumetafuta na imetupa majibu kuwa Bujumbura Qiblah chake ni Kaskazini Mashariki. Hakikisha nanyi kwa upande wenu kama ni sahihi. Na pindi ikiwa mmeshindwa kabisa kujua Qiblah kiko wapi basi ni kukisia na huku mfanye juhudi kubwa sana kutafuta dira hizo ili muweze kuziswali Swalah zenu kikamilifu.

 

Mas-uliya haya ya kutafuta Qiblah yameshakuwa ni yako wewe Mkurugenzi wa huo msikiti, wewe na wahusika wote wa hapo. Hivyo basi ni wajibu wako kufanya chini juu kujua Qiblah cha msikiti huo.

 

Na Allaah Anajua zaidi   

 

 

 

Share