Ajiepushe Na Rafiki Asiyeswali Au Aendelee Kumnasihi?

 

SWALI:

A.Alaykum WarahmatuAllaahi Wabarakatuh,

Namshukuru Mwenyeezi Mungu kwa kunipa uwezo wakuisoma hii website yenu na kuwaezesha nyinyi kutuelimisha sisi.  Hii website yenu inatufundisha mingi sana, Alhamdullillaahi.  InshaAllaah jaza yenu iko kwa Allaah (S.W).  Kila nikisoma ninapata faida nyingi sana.

Swali langu hili? Nina rafiki yangu ambaye anaswali akitaka na saa ingine haswali kabisa.  Mume wake haswali kabisa.  Nimejaribu kumnasihi mara nyingi.  Mara ingine ananisikia mara ingine hanisikii.  Sasa mimi nimekuwa confused kidogo.  Nifanye nini? Nijiepushe naye ama niendelee kumnasihii. Na jee kama nimejiepusha naye nitakuwa nimefanya makosa? 

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu kwa swali lako hilo nyeti. Hakika tatizo hilo linatokana na uchaguzi mbaya wa mume kwa huyo rafiki yako wa kike. Pindi mwanamke anapokubali kuolewa na mume ambaye haswali moja kati ya mambo mawili hutokea. Ama huyo mwanamke ataweza kumgeuza mumewe awe ni wa kufanya Ibadah au atabadilishwa yeye awe asi. Mara nyingi wanawake hugeuzwa kuwa waovu na maasi kwa sababu ya kuzidiwa na waume zao na hivyo kufuata mkumbo.

 

Kwa hali zote kila mmoja wetu ana wajibu na jukumu la kuwalingania wenzetu kwa uwezo wetu kwa kuwa Allaah Aliyetukuka Anasema: “Allaah Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake” (2: 286).

 

Mwanadamu ni dhaifu sana na hukosea kila wakati hivyo kufaa kukumbushwa. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini” (51: 55).

 

Ushauri wetu kwako ni kuwa ni lazima uendelee kumnasihi kwani hujui ni wakati gani Allaah Aliyetukuka Atakutilia kabuli. Ni sifa ya Muislamu kuwa hafi moyo kabisa katika shughuli kama hii ya Da‘wah na nyinginezo.

 

Allaah Aliyetukuka Anaelezea Imani kabambe ya Nabii Ya‘quub (‘Alayhis Salaam): “Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yuusuf na nduguye, wala msikate tamaa na faraji ya Allaah. Hakika hawakati tamaa na faraji ya Allaah isipokuwa watu makafiri” (12: 87).

 

Zidi kumlingania kwa mawaidha mazuri kisha natija ya kubadilika ipo mikononi mwa Allaah Aliyetukuka, lakini ujira wako uko pale pale. Mchapishie makala muhimu kuhusu Swalah zilioko katika kiungo kifuatacho:

 

Swalaah - Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

Kwa sababu yake huyo rafiki yako kuendelea na maasiya mbali na kumnasihi inatakiwa umkate kidogo. Hii ni kumaanisha usiwe na urafiki naye kama zamani kwani ukiwa na urafiki wa karibu zaidi huenda akakuathiri kidogo kidogo. Hii ni kuwa ukaribu na umbali baina ya waja umewekewa mipaka na Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mja yuko katika Dini ya rafiki yake, hivyo achague mmoja wenu yule anayefanya usuhuba naye” (at-Tirmidhiy).

 

Kupendana na usuhuba unafaywa kwa ajili ya Allaah na kuchukiana hivyo hivyo kwa sababu Yake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anayependa kwa ajili ya Allaah na akachukia kwa ajili ya Allaah, na akatoa kwa ajili ya Allaah, na akazuia kwa ajili ya Allaah basi amekamilika Imani” (Abu Daawuud).

Pia miongoni mwa watu saba watakaokuwa chini ya kivuli cha Allaah Siku ya Kiyama siku ambayo hakutakuwa na kivuli ila kivuli Chake, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: Watu wawili waliopendana kwa ajili ya Allaah wakawa pamoja kwa hilo, na wakatengana kwa hilo” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Kwa muhtasari ni kuwa usiwe na urafiki kama zamani lakini endelea kumpatia nasaha. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupatie tawfiki katika hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share