Nini Kazi Au Majukmu Ya Imaam Katika Uislamu

 

Nini Kazi Au Majukmu Ya Imaam Katika Uislamu

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Nataka nijuwe mtu anayeitwa imam ana kazi gani katika Uislam, ni hayo tuu.

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika majukumu ya Imaam yamebadika sana kwa kupitia na wakati na hasa kuwa hakuna dola ya Kiislaam kwa sasa. Wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa wake waongofu Abu Bakr Asw-Swiddiyq, ‘Umar bin al-Khatwtwaab, ‘Uthmaan bin ‘Affaan na ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wao ni Imaam wa kila kitu kwa Uislaam. Uimaam wao ulikuwa ni wa uongozi wa juu wa kijumla.

 

 

Wakati huo walikuwa wao wana Uimaam wa kuongoza watu katika Swalaah zote katika Msikiti mkuu wa makao yao makuu (mji mkuu wa dola). Na pia walikuwa viongozi wa mambo yote ya wananchi wao ya kidunia. Kwa hiyo, kwa muhtasari walikuwa wakifanya yafuatayo:

 

 

1.   Kuongoza katika Swalaah.

 

2.   Kuendesha Dola na siasa yake.

 

3.  Kuhakikisha ukusanyaji wa Zakaah umekwenda sawa na mali iliyo patikana imewekwa katika Baytul-Maal.

 

4.  Kuhakikisha biashara inakwenda kulingana na Shariy’ah.

 

5.  Kuhukumu kesi.

 

6.  Kuwa Amiri wa jeshi linalokwenda katika Jihaad.

 

7.   Kuwa kiongozi katika Shuwraa iliyokuwa ikifanyika.

 

8.   Na mengineyo.

 

 

Haya takriban yote yalikuwa zaidi wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ama wakati wa Makhalifa waongofu dola ilikuwa imepanuka kwa kiasi kikubwa na ujemadari wa majeshi walikuwa wakiachiwa watu wengine. Na majukumu ya hukumu na uliwali katika miji iliyokuwa mbali na mji mkuu yakaachiwa mahakimu na maliwali waliochaguliwa na Khalifah.

 

Ama kwa sasa, kwa kuwa Imaam anasaidiwa na kamati ya Msikiti, Imaam amekuwa na majukumu yafuatayo:

 

 

1).  Kuongoza Waumini katika Swalaah.

 

2).  Kutoa Khutbah Siku ya Ijumaa.

 

3). Kuandaa darsa na mihadhara ndani ya Msikiti ili kuwaelewesha maamuma wake kuhusu Dini yao.

 

4). Kufanya suluhu baina ya watesi wawili au makundi mawili au wanandoa.

 

 

5). Kuishauri kamati kuhusiana na kuendesha mambo kulingana na mfumo wa Kiislaam.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share