05-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Abu Bakr ( رضي الله عنه ) Anazitamka Shahada Mbili

 

Yote haya yalikuwa yakimpitia Abu Bakr akilini mwake huku akielekea nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kutua mizigo yake, na baada ya kusalimiana na watu wake.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposikia mlango unagongwa akamtaka mkewe Bibi Khadija (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatizame nani aliye mlangoni.

Bibi Khadija (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema; "Abu Bakr huyo"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Mfungulie".

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaingia, na baada ya kusalimiana akaanza kuuliza;

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu): "Ni kweli wanayosema juu yako?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Wanasema nini?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu): "Wanasema kuwa wewe unasema umepata Utume na kwamba unapata

habari kutoka mbinguni."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Na wewe uliwajibu nini?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu): "Niliwaambia; Ikiwa kweli umesema hivyo basi mimi nasadiki."

Furaha ilimjaa Bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na machozi kumlengalenga. Akamkumbatia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kukibusu kipaji cha uso wake, kisha akakaa na kuanza kumhadithia namna alivyojiwa na Jibriyl katika Pango la Hiraa na jinsi alivyobanwa na Malaika huyo na kumtaka asome aya tano za mwanzo za Suratul 'Alaq:

"Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Aliyemuumba mwanadamu kwa pande la damu. Soma, na Mola wako mkarimu sana. Ambaye amemfundisha (binadamu ilimu zote hizi kwa msaada) wa kalamu. Amemfundisha mwanadamu (chungu ya) mambo ambayo alikuwa hayajuwi ."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akiyasikiliza yote hayo kwa utulivu mkubwa, akatizama chini kwa khushuu, kisha akatamka;

"Ash-hadu al-laa ilaaha Illa Allaah wa ash- hadu annaka RasuluLlaah".

(Nashuhudia kuwa hapana mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, na nashuhudia kuwa wewe ni mjumbe wa Allaah).

Hivi ndivyo alivyosilimu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Share