06-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Abu Bakr ( رضي الله عنه ) Anaanza Kazi Ya Kuwasilimisha Watu

 

Siku ya pili yake Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) aliwasilimisha watano katika mabwana wa kabila la Kikureshi, nao ni 'Uthmaan bin Affan, Az-Zubayr bin 'Awwaam, 'Abdur-Rahmaan bin 'Awf, Sa'ad bin Abi Waqqaasw na Twalhah bin 'UbayduLLaah; akaja nao mpaka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na wote hawa ni katika wale kumi waliokwisha bashiriwa Pepo .

Siku iliyofuata aliwasilimisha vigogo wengine wanne na kuja nao mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), nao ni 'Uthmaan bin Madh'uwn, Abu 'Ubaydah 'Aamir bin Al-Jarraah, Abu Salamah na Al-Arqam bin Abi Al-Arqam.

Nguvu ya Uislamu ikaongezeka, na Abu Bakr aliitumia mali yake yote katika kuunusuru Uislam na pia nguvu zake na daraja lake mbele ya ma-Quraysh, na vyote hivi vilisaidia sana katika kuujenga na kuuendeleza Uislamu, hata watu wakawa wanasema;

"Wasingeshikamana wawili hawa kama hivi, kwa jambo la upotovu."

 

Share