09-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Wakeze Na Wanawe

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alioa wake wanne;

Wakati wa ujahilia (kabla ya kuja kwa Uislamu) alimuoa Qutaylah binti Sa'ad na akazaa naye 'Abdullaah na Asmaa (Radhiya Allaahu 'anhaa).

'Abdullaah aliingia katika Uislamu tokea siku za mwanzo na alifariki wakati wa ukhalifa wa baba yake.

Asmaa (Radhiya Allaahu 'anhu) ni maarufu kwa jina la 'Dhaat Nitwaqayn', na alipewa jina hilo baada ya kukata 'Nitaaq' mkanda wa kitambaa kinachofungiwa nguo kiunoni na kukifunika chombo kilichotiwa chakula alichokuwa akipelekewa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) walipokuwa pangoni wakati wa kuhajir kwenda Madiynah, na alikuwa mkubwa kwa umri kuliko Bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa).

Aliolewa na Az-Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhu) walipokuwa Makkah na alizaa naye watoto wengi mpaka alipomuacha akawa anaishi kwa mwanawe 'Abdullaah bin Az-Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhumaa) aliyeuliwa Makkah.

Bibi Asmaa (Radhiya Allaahu 'anhaa) aliishi miaka mia, na mwisho wa maisha yake alikuwa kipofu.

 

Wakati wa ujahilia Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuoa pia Umm Rumaan (Radhiya Allaahu 'anhaa) aliyezaa naye 'Abdur-Rahmaan na Bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na alifariki dunia wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliyeteremka kaburini kwake siku ya maziko na kumuombea maghfirah.

'Abdur-Rahmaan alipigana vita vya Badr na vita vya Uhud akiwa upande wa makafiri, na kabla ya kuanza vita vya Badr aliita kwa sauti kubwa akitaka mtu yeyote upande wa Waislamu aje kupambana naye na Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alipotaka kutoka na kupambana na mwanawe huyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimzuia na kumwambia;

"Tuache tukufaidi."

'Abdur-Rahmaan alikuwa shujaa na mtupa mshale mwenye shabaha aliyesilimu baada ya mapatano ya Hudaybiyah (Sulhul-Hudaybiyah), akawa Muislamu mwema aliyepigana vita mbali mbali akiwa upande wa Waislamu, alishiriki katika vita vya Al-Yamaamah chini ya uongozi wa Khaalid bin Waliyd (Radhiya Allaahu 'anhu) wakati majeshi ya Waislamu yalipopambana na majeshi ya Musaylimah Al-Kadhdhaab (Mtume wa uongo), na yeye ndiye mkubwa wa watoto wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) na alifariki dunia ghafla mahali panapoitwa Hibsh karibu na mji wa Makka katika mwaka wa 53 H.

Kitabu cha 'Abu Bakr al Siddiq – Muhammad Ridhwa

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuoa pia Asmaa binti 'Umays (Radhiya Allaahu 'anhaa) baada ya kuuliwa kwa mumewe wa mwanzo Ja'afar bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu 'anhu), wakapata mtoto waliyempa jina la Muhammad bin Abi Bakr.

Abu Bakr alipofariki dunia, Asmaa aliolewa na 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu 'anhu) akazaa naye mtoto waliyempa jina la Al-Qaasim.

 

Wakati wa Uislamu Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuoa pia Habiybah bint Khaarijah bin Zayd bin Abi Zuhayr Al-Khazrajiwakapata mtoto waliyempa jina la 'Aaishah Ummu Kulthuwm aliyeolewa na Twalhah bin 'Ubaydullaah (Radhiya Allaahu 'anhu).

Share