11-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Kuhajir Pamoja Na Swahibu Yake

 

Juu ya kuwa hapana uamuzi mzito kuliko mtu kuamua kuihama nchi yake, kuwaacha watu wake pamoja na nyumba aliyozaliwa ndani yake, na kuyaacha nyuma yote yanayomkumbusha utoto wake, sahibu zake wa utotoni pamoja na kuwa mbali na ardhi aliyocheza na kugaragara juu yake, lakini Waislamu iliwabidi wafanye hivyo baada ya washirikina wa Makkah kuwaonjesha kila aina ya adhabu na kuwazuwia wasiifanye kazi waliyokabidhiwa na Mola wao ya kuilingania dini Yake, dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala).

Iliwabidi watafute ardhi nyengine, ardhi madhubuti itakayowawezesha kusimama imara juu yake kwa ajili ya kuifikisha kwa watu amana waliyopewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) na pia kuwawezesha kujilinda kutokana na maadui wa Allaah. Mahali watakapoweza kujitayarisha kwa ajili ya kupigana Jihadi.

Kwa ajili ya lengo hilo adhimu, watu wa Madina walikuwa wakiwasubiri kwa hamu kubwa sana ndugu zao kutoka Makkah, kwani wao ndio waliokuja mahali panapoitwa Mina kwa ajili ya kufungamana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Mafungamano mawili yaliyokuja kujulikana kwa jina la 'Fungamano la Aqaba' la kwanza na la pili na kumtaka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ahamie kwao na kumuahidi kuwa watamlinda na kumsaidia katika kuilingania dini hii kwa hali na mali.

Wakati wa kuhama ulipowadia, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alimwendea Sahibu yake Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumtaka wafuatane pamoja kuelekea Madina, akamwambia;

"(Assuhba ya Aba Bakr)”.

Kabla ya hapo ma-Quraysh walikwisha amua kumuuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakihofia kuwa akifanikiwa kuhamia Madiynah itakuwa rahisi kwake kujijenga na kuineza dini aliyokuja nayo na kuipiga vita dini yao iliyo baatwil.

Kwa kusudi hilo, wakatuma vijana kutoka matumbo mbali mbali ya kabila lao na kuwataka wote kwa pamoja wamchome Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa panga zao ili damu yake ichanganyike baina ya matumbo yote hayo, jambo litakalowazuwia jamaa zake wasiweze kudai kulipa kisasi cha mtu wao, na itawabidi waridhike  kwa kulipwa fidia tu.

Jibriyl (‘Alayhis Salaam) alimjulisha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yote hayo na akamtaka aondoke usiku huo huo kuelekea Madina.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwita 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumwakilisha jukumu la kurudisha amana za watu, akamtaka pia alale juu ya kitanda chake, kisha akatoka huku akiwasomea wale vijana waliokuja kumuwa waliokuwa wakimsubiri nje ya nyumba yake baadhi ya aya za Surat Yaasin, huku akiwanyunyizia mchanga juu ya vichwa vyao na kuwaacha hapo wakiwa wamelala usingizi mzito.

 

Alitoka na kwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu), na baada ya kumgongea mlango huku akiwa amejifunika uso wake, sahibu yake akatoka, wakaondoka wote kwa pamoja na kuelekea Madina kupitia njia ya pwani pwani kwa ajili ya kuwababaisha makafiri, kwa sababu njia hiyo kwa kawaida haikuwa ikitumiwa na wasafiri wanaokwenda Madina.

Walipowasili penye pango linaloitwa ‘Ghaari Thawr’ wakaingia humo kwa ajili ya kujipumzisha.

Alipokuwa akilichunguza pango hilo, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akagundua mashimo mengi ndani yake ambayo nyoka, nge au wadudu wabaya wangeweza kupenya kupitia humo. Akachana nguo zake za kujifunikia na kuanza kuyaziba matundu hayo, isipokuwa moja alishindwa kuliziba baada kuishiwa na nguo za kuchana, akakaa karibu yake na kuliziba kwa mguu wake haidhuri adhurike yeye, lakini chochote kisipitie humo na kumdhuru Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitaka kupumzika, akalala karibu na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa ameuweka uso wake mtukufu juu ya paja la Swahibu yake huyo, na haukupita muda wakaanza kusikia sauti za ma-Quraysh waliokuwa wakiwatafuta.

Sauti zikawa zinakaribia, na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), alipoinama na kutizama nje aliweza kuona namna gani maadui hao walivyo karibu nao, akamwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam);

"Mmoja wao akiinama tu, atatuona ."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;

"Usihuzunike ewe Abu Bakr, Allaah yupo pamoja nasi, Unaonaje ikiwa wawili, watatu wao ni Allaah?"

 

Allaah Anasema:

"Ikiwa nyinyi hamtamnusuru (Mtume), basi Allaah alikwisha mnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wapili katika wawili walipokuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: ‘Usihuzunike. Hakika Allaah yu pamoja nasi’. Allaah akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona, na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Allaah kuwa ndilo juu. Na Allaah ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima."

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatafunwa na nnge, katika mguu wake ule aliouweka juu ya tundu pale alipoishiwa na vitambaa vya kuzibia. Maumivu yakawa yanazidi, lakini alikhiyari kunyamaza na kustahamili asije akamshughulisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ingawaje alikuwa akijua kuwa sumu inatembea ndani ya damu yake na huenda ikamuua.

Maumivu yalikuwa makali sana hata chozi likamdondoka na kuanguka juu ya uso wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliyestuka na kuuliza:

"Kuna nini Abu Bakr, mbona unalia ?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Nimetafunwa na nnge ee Mtume wa Allaah" .

 Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akainuka na kuushika mguu pale ulipotafunwa, na kumuomba Allaah na hapo hapo sumu hiyo ikatoweka na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akapona.

 

 

Share