12-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Makubaliano ya Hudaybiyah

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikua akimfahamu na akimuelewa vizuri sahibu yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kupita Maswahaba wote (Radhiya Allaahu ‘anhu), na alikuwa na uhakika kuwa yote anayoyasema ni Wahyi utokao kwa Mola wake (Subhaanahu wa Ta'aala.

Katika mwaka wa sita baada ya kuhamia Madiynah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhu) waliondoka Madiynah kuelekea Makkah kwa nia ya kufanya 'Umrah. Wakapiga kambi karibu na mji wa Makkah mahali panapoitwa Al-Hudaybiyah, kisha wakamtuma 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhum) ende Makkah kuwajulisha Ma-Quraysh juu ya nia yao hiyo na kwamba hawakuja kwa nia ya kupigana vita.

Ma-Quraysh wakapeleka majeshi yao kutaka kuwazuia, na baada ya majadiliano marefu yaliyopita baina yao, wakaamua kumtuma mjumbe wao aitwaye Suhayl bin 'Amr, aliyeweza kufikia makubaliano na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yaliyokuja kujulikana kwa jina la Makubaliano ya Al-Hudaybiyah.

Yafuatayo ni baadhi ya shuruti za makubaliano hayo;

·   Waislamu warudi Madiynah mwaka huu na wafanye 'Umrah mwaka ufuatao.

·    Waislamu wanalazimika kumrudisha kwa Makureish yoyote atakayeingia katika dini yao na kukimbilia Madiynah, lakini Ma-Quraysh hawalazimiki kumrudisha atakayetoka katika Uislamu na kukimbilia Makkah.

·   Wasipigane vita kwa muda wa miaka kumi, na wawe wanaendeana watakavyo.

 

Kabla ya mkataba huo kutiwa sahihi (saini), Waislamu walistukia kijana mmoja aitwae Abu Jandal aliyesilimu lakini alikuwa akiishi Makkah akipitishwa mbele yao akiwa amefungwa minyororo shingoni huku na kubebeshwa jiwe kubwa akipiga kelele akiwaomba Waislamu wenzake wamuokoe kutokana na adhabu hiyo.

Kijana huyu Abu Jandal ni mwana wa Suhayl, mjumbe wa Ma-Quraysh katika sulhu hiyo.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alimuonea huruma kijana huyo, akamtaka Suhayl amruhusu wamchukue kwa sababu mkataba ulikuwa bado haukutiwa saini wala haukupigwa mhuri, lakini baba yake alikataa na kutishia kuuvunja mkataba na kuanzisha vita ikiwa  watajaribu kumchukua kwa nguvu.

Abu Jandal alikuwa akipiga kelele huku akisema;

"Enyi Waislamu wenzangu! mnaniacha nirudi kwa washirikina hawa na mimi nataka himaya yenu?"

Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia ;

"Kuwa na subira, na Allaah atakujaalia utoke katika janga hilo".

'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuweza kuyastahamilia haya, akamuendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na kumuuliza;

"Ewe Mtume wa Allaah, wewe si Mtume wa Haki?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akamjibu;

"Ndiyo, ewe 'Umar".

Akauliza tena;

"Kwa nini basi tunakubali kujidhalilisha?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akamwambia;

"Ewe 'Umar, mimi ni Mtume wa Allaah, siwezi kumuasi, na Yeye ndiye atakayetunusuru".

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akauliza;

"Si ulituahidi kuwa tutakwenda Makkah na tutatufu katika nyumba kongwe?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akajibu;

"Nilikwambia kuwa ni mwaka huu ewe 'Umar?"

'Umar akajibu;

"La hukusema hivyo."

Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akasema;

"Utakwenda Makkah ewe 'Umar na utatufu penye nyumba."

'Umar pamoja na baadhi ya Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) hawakuridhika na baadhi ya masharti yaliyokuwemo ndani ya mkataba ule, wao waliona kuwa Waislamu wamekubali kujidhalilisha kwa kuyakubali masharti yote ya makafiri, na hii ni kwa sababu dhahiri yake mkataba huo si mzuri juu ya Waislamu, lakini kwa anayeona mbali mkataba huo ulikuwa ni ufunguzi mkubwa kwa Waislamu, kama alivyosema Allaah katika Suratul Fat-h aya ya mwanzo;

"Bila shaka tumekwishakupa kushinda kuliko dhahiri"

Allaah katika aya hii anatujulisha kuwa kuukubali mkataba huo ni ushindi mkubwa kwa Waislamu, juu ya kuwa dhahiri yake ni kukubali masharti yote ya makafiri, na hii ni inatokana na sababu zifuatazo;

1)      Kutokana na suluhu hiyo, makafiri walifungika wasiweze kupigana vita dhidi ya Waislamu muda wa miaka Kumi.

2)      Katika muda wote huo Waislmu wakawa na uwezo wa kujishughulisha na kuieneza dini yao miongoni mwa makabila mengine ya Bara Arabu, pamoja na nchi za Shaam.

3)      Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alituma ujumbe kwa wafalme mbali mbali

4)      Wale waliosilimu wasioruhusiwa kukimbilia Madiynah kwa ndugu zao Waislamu, ni bora kwao kubaki Makkah kwa ajili ya kuwalingania watu katika dini ya Kiislam huko Makkah.

5)  Makafiri watakaorudi Makkah iwapo watatoka katika Uislam, hawataudhuru Uislam.

Sababu hizi na nyinginezo ambazo si wasaa wake huu kuzitaja ni dalili kuwa mkataba huo undani wake ulikuwa na manufaa makubwa kwa Waislamu, juu ya kuwa dhahiri yake ni kusalimu amri na kukubali masharti yote ya Ma-Quraysh.

Na hii ndiyo sababu iliyomfanya 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) asiridhike nao, wala asisimame hapo. Kwani alimwendea pia Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumuuliza tena masuali yale yale;

"Ewe Abu Bakr, Muhammad si Mtume wa Haki?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu); "Ndiyo"

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu); "Tukipambana nao makafiri hawa, si atakayekufa upande wetu ataingia Peponi na wao wanaingia Motoni?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu); "Ndiyo".

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu); "Kwa nini basi tunakubali kujidhalilisha?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu);

"Ewe 'Umar, yeye ni Mtume wa Allaah na hawezi kumuasi, na Allaah ndiye atakayemnusuru, kamatana naye kwani Wallahi yupo katika Haki".

Majibu yale yale ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kayapata kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), na Allaah akawateremshia Waislamu utulivu nyoyoni mwao.

Allaah anasema;

"Yeye ndiye aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waislamu ili waongezeke imani juu ya imani yao".

Suratul Fat-h 4

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema baadaye;

"Nikatambua kuwa ile ndiyo Haki".

Mwaka wa tisa Hijri ndio mwaka ulioitwa 'Mwaka wa Wajumbe' na hii ni kutokana na wajumbe wa makabila mbali mbali ya kiarabu waliokuja kusilimu mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Share