13-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Vita Vya Badr

 

Imani ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)ilikuwa ikijitokeza na kueneza tumaini baina ya watu kila inapotokea shida au dhiki.

Katika vita vya Badr, jeshi dogo sana la Waislamu liliondoka mjini Madiynah kwa nia ya kuuteka msafara mdogo wa kibiashara ukiongozwa na Abu Sufyan unaotokea Syria na kuelekea Makkah, na Waislamu walitegemea kuwa bila shaka msafara huo utakuwa na watu wachache waliokwishachoka baada ya safari ndefu hiyo.

Allaah akawataka Waislamu wauachilie mbali msafara huo na wende kupambana na jeshi kubwa la Ma-Quraysh lililokwishaondoka Makkah kuelekea Madiynah likiwa limejitayarisha kivita na limejizatiti barabara. Na Allaah aliwaahidi Waislam kuwa watawashinda Ma-Quraysh hao juu ya wingi wao.

Idadi ya Waislam ilikuwa mia tatu na kidogo tu, na hawakuwa na silaha nzito isipokuwa panga zao.

Waislamu wakapiga mahema yao katika bonde la Badr na kumtaka Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asiondoke hemani pake iwe itakavyokuwa.

Jeshi kubwa la makafiri likaanza kuhujumu kwa nguvu, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihuzunika kila anapoona Muislam anauliwa, na mambo yalipozidi kuwa magumu hata akawa anasikia sauti za panga na kelele na mayowe zikikaribia, akaamua kutoka nje ya hema huku akinyanyua mikono yake mbinguni na kumuomba Mola wake kwa hamasa akisema;

"Mola wangu ikiwa kundi hili litaangamizwa, hutoabudiwa tena ardhini, Mola wangu nipe ushindi ulioniahidi Mola……"

Aliendelea hivyo mpaka  Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomwendea na kuiweka sawa nguo ya kujifunikia ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyokuwa ikimwanguka huku akimwambia;

"Ewe Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa Allaah inatosha kuomba, kwani Mola wako atakupa kile alichokuahidi".

Bila shaka Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anaamini kuwa kila alichoahidiwa na Mola wake atakipata, bali hata kabla ya vita hivyo kuanza, yeye ndiye aliyewaonesha Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) mahali watakapoanguka vigogo vya Ma-Quraysh. Aliwaonyesha mahali gani Abu Jahl atauliwa na kuanguka, na akawaonyesha mwahali gani watauliwa na kuanguka vigogo wengine mbali mbali wa ki-Quraysh, na  yote yalitokea kama alivyosema.

Lakini hisia yake juu ya uzito wa mzigo alioubeba na hofu yake katika pambano hili la mwanzo baina ya Imani na Kufru ndiyo iliyomfanya atoke nje ya hema lake na kunyanyua mikono yake juu akiomba kwa hamasa namna ile.

 

 

Share