Kuomba Du'aa Kwa Lugha Yoyote Katika Swalaah Inajuzu?

SWALI:

Je inajuzu kuomba dua katika SIJDA kwa lugha yeyote kwenye Swalah ya SUNNAH?

 


 

JIBU: 

 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako zuri kuhusu mas-ala ya 'Ibadah na hasa ile ya Swalah ambayo ni nguzo muhimu na ya pili baada ya Shahada. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: "Swalini kama mulivyoniona mimi nikiswali" (Al-Bukhaariy). Hivyo, 'Ibadah zote ni tawqiifiyyah, yaani kufuata kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au kutuelekeza.

Wako Wanachuoni wanaoona kusoma du'aa kwa lugha isiyo ya Kiarabu kwa asiyejua Kiarabu inajuzu kwenye Swalah zozote. Lakini rai yenye nguvu ni kuwa Swalah za fardh ni bora kusoma Du'aa ndani ya Swalah kwa lugha ya Kiarabu. Ama Swalah za Sunnah, wametofautiana Wanachuoni; wengine wanasema inatakikana kusomwa kwa Kiarabu vilevile na baadhi wamesema kuwa inawezwa kusomwa Du'aa ndani ya Swalah kwa lugha isiyo ya Kiarabu kwa asiyeweza kabisa kusoma kwa Kiarabu au asiyejua. Hata hivyo asijiache mtu  kutokufanya bidii ya kujifunza Du'aa hizo kwa Kiarabu na akawa tu ametosheka kwa lugha yak kwani ni imemwajibikia kila Muislamu kujifunza lugha ya Kiarabu kwa kuwa ni lugha Aliyoichagua Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwa ni lugha ya Qur-aan.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share